Wakati uamuzi wa kuhusu mgogoro wa CUF ukiwa haujatolewa, ukaibuka mwingine ndani ya Chama cha NCCR- Mageuzi ambao nao umefikishwa katika ofisi hiyo na kuifanya iwe na viporo viwili vya migogoro.
Ucheleweshaji wa majibu wa mgogoro wa CUF, umesababisha kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wale walioupeleka katika ofisi hiyo wakidai kuwa kuna mchezo wa kutaka kuwalinda vigogo wa chama hicho.
Hata hivyo, majibu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara ni kwamba, inachukua kila hatua za kuhakikisha uamuzi unaotolewa unakuwa wa haki kwa pande zote.
Kwamba, ofisi hiyo ni mlezi wa vyama na wanachama wake, hivyo inafanya kazi wa kufuata, sheria, kanuni na tataribu zilizoipa jukumu hilo na sio matakwa ya kikundi au watu fulani, huku ikitaka wahuskia kuwa wavumilivu.
Ni kweli kinachosemwa na ofisi hiyo kina mashiko, lakini ingekuwa ni vyema kuongeza kasi ya kupitia malalamiko hayo ili kuondoa mawazo yaliyojengeka kwamba Ofisi ya Msajili inafanya hivyo kuwalinda vigogo wa CUF.
Ninadhani hatua ya kumaliza mgogoro huo zikichukuliwa haraka, itasaidia kupunguza viporo vya migogoro ya vyama katika ofisi, kwani mbali na huo wa CUF kuna mwingine wa Chama cha NCCR- Mageuzi.
Mgogoro wa NCCR- Mageuzi, unaelezwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kuwa anasubiri kwanza majibu ya Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene.
Akakiri kwamba, ofisi yake ilipokea mgogoro huo, lakini ghafla viongozi wa chama waliosimamishwa, wakaenda pia kwa Waziri, hali iliyomlazimu asubiri kwanza uamuzi wa Waziri huyo ndipo ajue pa kuanzia.
Hilo ninakubaliana naye kwamba, ofisi yake kwa sasa haina cha kufanya kuhusu mgogoro huo zaidi ya kusubiri maelekezo ya Waziri, lakini pamoja na hayo, ingeharakisha kumaliza mgogoro wa CUF.
Ninaamini kwamba, iwapo itafanya hivyo, inaweza kuwafanya wale waliofukuzwa ndani ya chama kujua hatma yao kama wanarudishwa au wanatoswa moja kwa moja, ili wajue ni hatua gani zaidi wachukue.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mlezi wa vyama, njia nzuri ambayo ingesaidia kuvifanya visiwe na migogoro, ni kuharakisha kutoa uamuzi inapofikishiwa malalamiko ya wanachama.
Ikumbukwe kuwa kumekuwapo na madai kwamba, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inalea migogoro ya vyama, hivyo ili kuondoa madai hayo, ninadhani njia nzuri ni kuhakikisha malalamiko yanashughulikiwa haraka.
Suala la kujipa muda kushughulikia migogoro ni la muhimu, lakini pia ninadhani isingefaa muda uwe mrefu sana kama ambavyo imetokea kwa mgogoro wa kiuongozi wa Chama cha Wananchi (CUF).
Wanachama waliofukuzwa, wanadai kuwa mgogoro wao umechukua muda mrefu bila kutolewa uamuzi na wakati wakiendelea kusubiri majibu, umejitokeza mwingine wa Chama cha NCCR- Mageuzi.
Meza ya mazungumzo inatajwa kama ndiyo njia nzuri ya kumaliza migogoro katika vyama vya siasa, hivyo ninaamini hatua ya wanachama kukimbilia ofisi hiyo, inalenga kutaka kumaliza migogoro katika vyama vyao.
Msajili wa Vyama vya Siasa alishawahi kutumia njia hiyo alipoitisha meza ya mazungumzo ya Baraza la Vyama vya Siasa kujadiliana na wadau wa siasa na maendelo nchini, baada ya kuwapo sintofahamu ndani ya vyama vya Siasa.
Ninadhani njia hiyo pia ingetumika kumaliza mvutano uliopo ndani ya CUF ulioanza Novemba mwaka jana, ingawa unaonekana kwenda kimya kimya, huku waliofukuzwa wakilalamikia ofisi hiyo, lakini na huo mpya wa NCCR.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







