Chanjo hiyo itakuwa ni ya awamu ya tatu kwa mwaka huu wa 2022 ikilenga kufikia watoto milioni 12. 3 ili kuwaepusha na ugonjwa huo unaotajwa kuathiri mfumo wa ‘neva’ na huweza kusababisha udhaifu wa misuli au kupooza.
Machi mwaka huu, chanjo hiyo ilitolewa mikoa minne inayopakana na nchi ya Malawi ambayo ni Mbeya, Songwe, Ruvuma na Njombe, watoto milioni 1.1 sawa na asilimia 115 wa chini ya miaka mitano walichanjwa.
Baada ya hapo, awamu ya pili ya chanjo ilitolewa nchi nzima kuanzia Mei 18 hadi 21 mwaka huu na kuwafikia watoto 12, sawa na asilimia 118.8 na leo inaanza chanjo ya awamu ya tatu.
Hapo namrejea Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika taarifa yake kwa umma alipokuwa akitangaza kuanza kwa kampeni hiyo, kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo uliotokea katika nchi za jirani.
Katika ufafanuzi wake ni kwamba, Februari mwaka huu nchi ya Malawi ilikumbwa na ugonjwa huo, kisha Mei mwaka huu Msumbiji nayo ikakumbwa, ambapo Tanzania imeamua kuchukua tahadhari.
Ninadhani kampeni hiyo si ya kukosa, hivyo ingekuwa ni vyema wazazi na walezi wakawapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea chanjo hiyo kwa ajili ya kuwanusuru dhidi ya ugonjwa huo.
Ikumbukwe, wataalamu wa afya wanasema maambukizi ya polio yanaathiri mfumo wa neva na huweza kusababisha udhaifu wa misuli au kupooza, ambapo ugonjwa huo huwapata zaidi watoto wa chini ya miaka mitano.
Hivyo, ili kuwanusuru na polio watoto wa chini ya miaka mitano, njia pekee ni kuhakikisha wanapata chanjo kama ambavyo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amekuwa akitangazia umma wa Watanzania.
Waswahili wana msemo wao kwamba; 'ukiona mwenzio ananyolewa na wewe tia zako maji'. Majirani zetu wamekumbwa na ugonjwa huo, hivyo nasi hatuna budi kujiandaa kukabiliana nao.
Kwa kuwa inaelezwa, maambukizi ya virusi vya polio huweza kuzuiliwa kwa chanjo, hivyo ninadhani ni muhimu wazazi na walezi kufuatilia ratiba ya chanjo, ili kuhakikisha watoto wao wanapata huduma hiyo.
Ummy anakumbusha kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO), limekuwa likielekeza kuwa unapotokea mlipuko au tishio la mlipuko wa ugonjwa, nchi yenye ugonjwa na ambayo iko jirani inapaswa kufanya kampeni ya chanjo.
Tayari kwa mwaka huu Tanzania imeshafanya awamu mbili za kampeni ya kutoa matone na chanjo na leo inaanza awamu ya tatu ambayo ninaona nikumbushe jamii kutambua umuhimu wake.
Pia muhimu wazazi na walezi wasikubali kupewa elimu potofu kuhusu chanjo hiyo kama ambavyo ilitokea kwenye chanjo ya UVIKO-19, badala yake wawapeleke watoto katika vituo vya kutolea huduma hiyo.
Kuwapo kwa kampeni ya chanjo ya polio, kumeshaelezwa kuwa ni kutokomeza na kuwakinga watoto na kuokoa gharama zinazotokana na matibabu ya ugonjwa huo, ambao inaelezwa kuwa unazuilika.
Ninagusia elimu potofu kutokana na kwamba imekuwa, ni kawaida kwa baadhi ya watu kuzusha taarifa zisizo na ukweli kwenye mambo ya msingi, hali ambayo inaweza kukwamisha huduma hiyo kwa waatoto.
Kwa mfano, baada ya ugonjwa wa UVIKO-19 kuingia nchini, kulikuwapo upotoshaji mwingi kuhusu ugonjwa huo, na hata chanjo ilipoanza kutolewa, bado kuna watu waliendelea kuipinga.
Inawezekana watu wenye mtazamo huo, wakaendesha kampeni ya kupinga chanjo ya polio na kusababisha baadhi ya wazazi na walezi wasipeleke watoto wao kupata matone ya chanjo hiyo.
Hivyo, ninadhani ni muhimu kila mzazi na mlezi kutafakari na kisha kuchukua hatua ya kumpeleka mtoto wake katika kituo cha kutolea huduma ya chanjo ya polio haraka iwezekanavyo.
Top of Form
Bottom of Form



.jpg?itok=nfwjwDzv)






