Jamani,wakazi Mwanza tunapata tabu kinachojiri stendi mpya Nyamhongolo

02Sep 2022
Anthony Gervas
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Jamani,wakazi Mwanza tunapata tabu kinachojiri stendi mpya Nyamhongolo

MWEZI uliopita serikali jijini Mwanza, ilifungua mradi wa stendi kuu mpya ya mabasi yaendayo mikoani 'Nyamhongolo'.Awali hiyo ilikuwa Buzuruga.

Ukweli wa uhalisi wake imezinduliwa, huku ikibaki kuwa na kero mama za vumbi katika kituo kidogo cha daladala, ambacho kipo mahali hapo nyuma ya stendi. Si ajabu mtu kashuka kutoka  kwenye basi akiwa na ama kanzu nguo nyingine safi akaoga vumbi kibao!   

Ni stendi iliyofunguliwa na kuanza kutumika ikihudumia mabasi yaendayo mikoa ya Mara, Simiyu na wilaya mbalimbali za mkoa Mwanza. Sasa ni jambo linalozua malalamiko ya wananchi wasafiri jijini, kwamba wanapokuwa katika kituo hicho kidogo cha daladala, wanakabiliwa na shida ya vumbi la magari hayo madogo.

Abiria hao wamekuwa wakidai kupata mafua, vikohozi, kuchafuka nguo, majengo ya abiria kujaa vumbi, macho kuuma wakati wakiwa wanasubiria daladala katika kituo hicho, huku eneo lingine ambalo limeunganisha Barabara Kuu ya Nyerere, ambalo halijafanyiwa usafi wa mazingira muda mrefu, limejaa nyasi na halina mtaro wa kupitisha maji.

Pamoja na kufunguliwa stendi hiyo ya kisasa, lakini bado haijakamilika katika eneo hilo na kusababisha kero kwa wananchi wasafiri, wanaohoji kulikoni serikali inafungua mradi ambao haujakamilika kwa ujumla, jambo ambalo inaacha maswali kwa nchi yetu ambayo imeshaingia kwenye uchumi wa kati wa chini.

Iko bayana, watendaji wetu daima hawaishiwi sababu na visingizio katika miradi hiyo mbalimbali kushindwa kukamilika katika kiwango kinachotakiwa.

Ubabaishaji na sarakasi bado zinatawala, huenda na mengime mabaya zaidi ya hayo. Hapo ndipo   kunazua msamiati ‘mazoea hujenga tabia.’ Tuna watendaji wanaofanya kazi kwa mazoea na inawezekana yapo ya kifisadi ndani yake, ambao unapaswa kukatwa, ili kuondoa sababu na visingizio vingi kwa wahusika.

Mimi binafsi naunga mkono hoja za hawa wananchi kuhusu swali lao, kwanini miradi yetu Watanzania huwa haikamiliki katika kiwango kinachotakiwa na kwa wakati? Hivi kuna sababu gani za kufungua mradi mkubwa kama huo wa mabilioni ya shilingi ukiwa haujakamilika ipasavyo?

Ifike mahali sote tuone aibu, nafsi zao ziwakonge wakijua kwamba hiyo miradi Watanzania wote wanapaswa kunufaika nayo na wananchi wanapopaza sauti zao mjue serikali kwamba kuna jambo.

Wananchi wanalalamika kwamba miradi mingi ikiwamo masoko, maeneo waliotengewa Machinga, vituo vidogo vya daladala na stendi za mabasi, kwa asilimia kubwa hujengwa na kufunguliwa bila ya kukamilika ipasavyo, ikiwamo miundombinu kutokuwa rafiki katika kufanya biashara zao.

Jamani Watanzania tunajikwaa wapi? Tuna rasilimali nyingi za kutosha kutekeleza miradi yetu,  tuna madini ya kila aina, makaa ya mawe, mafuta, bahari, maziwa matatu yenye samaki wa kila aina, mito, milima na ardhi yenye rutuba ya kutosha.

Katika zama hizi za kuupiga mwingi, ghafla kunapokuwapo watendaji wanaosubiri wasukumwe na wakuu wao na hawawezi kujisimamia wenyewe, ni sawa kweli  hawaioni hii adha?

Stendi hiyo iko katika Manispaa ya Ilemela, ambako Mstahiki Meya wake  Renatus Mulunga, analipambania hilo kwamba wamepanga bajeti nyingine kuhakikisha vumbi hilo linatoweka mara moja, ili kuondoa adha inayowakabili wasafiri na abiria wanapokuwa wakisubiri magari.

Ninawashauri, wenye uamuzi waondoe fedheha kwa kuwezesha kufunguliwa stendi ninayoitaja ya ambayo sehemu zake zingine hazijakamilika, ujenzi wake hadi sasa bado unaondoa maana ya kuwa na hadhi ya jiji.

Ninashauri serikali ishinikize kukamilishwa mpango wa kukamilisha ujenzi huo haraka kabla ya kipindi cha masika hakijaanza, vinginevyo itaibuka kero nyingine ya kuwepo matope na kuangukia kuwa aibu kwa mradi wote huo.