Kila la heri Simba Queens Ligi ya Mabingwa

27Aug 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kila la heri Simba Queens Ligi ya Mabingwa

KWA mara ya kwanza kwenye historia ya soka nchini, timu kutoka Tanzania Simba Queens inacheza fainali ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati kwa soka la wanawake, CECAFA, ikisaka tiketi pia ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hiyo imefanikiwa kuingia fainali na kuweka rekodi ya timu ya wanawake kutoka Tanzania kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kuchabanga AS Kigali mabao 2-1 kutoka nchini Rwanda, Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Leo hii inacheza fainali na She Corporate ya Uganda kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Bingwa wa michuano hiyo, atauwakilisha Ukanda wa CECAFA kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Iwapo Simba Queens itashinda basi itaweka historia ya kuwa timu ya kwanza kwa wanawake Tanzania upande wa soka kuiwakilisha nchi kwenye fainali hizo.

Simba Queens haitaiwakilisha Tanzania tu, bali ukanda wote wa Afrika Mashariki. Kwanza kabisa napenda kuipongeza timu hiyo kwa hatua ambayo wamefikia.

Ukikiangalia kikosi hicho tangu kilipoanza michuano hiyo unakiona kuwa si tu kama kina wachezaji wenye uwezo mkubwa, lakini wanajituma na njaa ya mafanikio.

Wanapocheza wachezaji wa Simba Queens unaona kabisa jinsi wanavyojituma kupambania jezi au nembo ya klabu yao.

Nilisikia hata baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba wakisema kuwa kama timu ya wanaume ingekuwa inacheza kama vile, basi kwa uwezo ilionao wasingefungwa na timu yoyote.

Wanasimba wenyewe wanaamini kuwa wana kikosi kizuri cha wachezaji, lakini tatizo ni kwamba hawajitumi kama ilivyo kwa timu ya wanawake.

Nirudie tena kwa kinadada ni kwamba baada ya kuishia nusu fainali msimu uliopita nchini Kenya, inaonekana viongozi walifanya tathmini ya kutosha na kugundua mapungufu kadhaa ambayo yamefanyiwa kazi.

Ni kwamba wamesajili wachezaji kadhaa kutoka nje ya nchi ambao wamekuja kuitoa pale ilipoishia na kuipeleka mbele.

Usajili wa kina Olaiya Barakat kutoka Nigeria, Vivian Aquino kutoka Kenya, Daniela Ngoi, beki wa kati ambao msimu uliopita aliichezea Yanga Princess raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,  Pambani Kuzoya ambaye ni raia wa Congo DR, kumeifanya timu hiyo kuimarika zaidi na kuifanya kuwa tishio.

Kuna wataalamu waliwaambia viongozi na benchi la ufundi Simba kuwa wana wachezaji wazuri, lakini inabidi watafute baadhi ya wachezaji wenye miili mikubwa hasa kwenye maeneo ya kiungo wa kukaba na mabeki wa kati. Na hilo limefanyika kwa kiwango kikubwa.

Uwekezaji uliofanywa kwa uongozi wa Simba unaonyesha kabisa kuwa unataka kufanya mapinduzi makubwa ya soka kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa upande wa wanawake.

Wakati wamepambana na kuifanya timu ya wanaume ya Simba kuwa moja kati ya timu kubwa na zinazoogopeka kwa sasa barani Afrika hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, sasa taratibu inaonekana wanaishika mkono timu ya wanawake nayo kuifanya kuwa tishio Afrika kwa upande wa wanawake.

Na nionavyo ni kwamba upande huu wa kinamama inaweza kupata mafanikio makubwa kwa muda mfupi kuliko hata timu ya wanaume.

Iwapo Simba itashinda kwenye mechi ya leo na kwenda fainali, ikifanya marekebisho madogo tu upande wa golikipa, inaweza kufanya makubwa, kwani inaweza kuwa timu ya kwanza kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kabla ya timu ya wanaume haijafanya hivyo.

Huu ni mfano wa kuigwa na klabu zingine nchini kuwekeza kwenye soka la kinamama kwani taratibu linaonekana kuanza kukua, na kujipatia mashabiki.

Tumeona jinsi wanachama na mashabiki wa klabu hiyo walivyojitokea kwa wingi kwenye mechi zao kama vile wanavyoenda kuishangilia timu ya wanaume.

Nina wasiwasi klabu zingine zikishtuka na kuona soka hilo limekuwa na mashabiki wengi na kuanza kuwekeza, tayari Simba Queens itakuwa ipo mbali sana.

Fainali ni fainali tu, chochote kinaweza kutokea, lakini kwa jinsi nilivyoiona Simba Queens tangu mwanzo, inaonekana ni timu bora zaidi kuliko zote msimu huu.

Imecheza mechi nne ikishinda zote, imefunga mabao 17 na kufungwa bao 1-0.

Hata timu inayocheza nayo She Corporate ya Uganda imeshacheza nayo kwenye hatua ya makundi, zote zikiwa Kundi B, lakini Simba ilishinda mabao 2-0.

Na nilivyoishuhudia mechi hiyo ni kwamba, Simba Queens ilikosa mabao mengi sana, kama ingekuwa makini, basi ingeibebesha mzigo wa mabao.

Pamoja na kwamba huwezi kutabiri fainali, lakini naipa nafasi kubwa Simba Queens ambayo pia inaonekana ina kikosi kizuri pia cha kwenda kupambana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.