Taarifa hizo ni muhimu kuandaa takwimu za mipango ya maendeleo kitaifa ili kuwezesha serikali kupanga, kuandaa na kufikisha huduma zote kwa kila Mtanzania.
Cha kufurahisha sensa ya mwaka huu ina vipengele mahsusi vinavyohusu sekta ya mawasiliano na matumizi ya huduma za kimawasiliano.
Aidha, sensa inafanyika kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kidijitali na karibu asilimia 28 ya maswali kwa wananchi yanahusiana ama moja kwa moja au kwa namna nyingine na eneo la mawasiliano; ambayo ni sekta wezeshi, inayochangia katika kukua kwa maeneo mengine ya kiuchumi na kijamii.
Kuna swali kuhusu umiliki wa simu na vifaa vya mawasiliano kama kompyuta. Linapohojiwa lengo ni kujua namba ya simu ya mkononi na kompyuta pia. Aidha, nia ni kuwa na kanzidata ya watumiaji wa simu hizo.
Kadhalika, hakuna swali kuhusu simu za mezani, labda ni kwa kuwa matumizi yake kwenye makazi yameshuka miaka ya karibuni na huenda yasiwepo tena.
Ni wazi kuwa majibu ya maswali kuhusu ulemavu yatafanikisha kuandaa mipango endelevu kwa makundi mbalimbali ya wenye mahitaji maalumu kwenye eneo la mawasiliano, hasa kujua aina ya vifaa saidizi wanavyohitaji, kama vile simu zenye sauti kubwa, visaidizi masikioni, mitetemo maalum na programu zinazowahusu.
Kwa Tanzania, huduma za mawasiliano ni pamoja na simu za mkononi na mezani, intaneti, utangazaji, posta na usafirishaji wa vifurushi na huduma zinazowezesha na matumizi haya.
Huduma nyingine ni kusafirisha fedha kupitia simu za mkononi, kuwasiliana mitandaoni ikiwa ni pamoja na mikutano na kupata matangazo ya televisheni na redio.
Taarifa inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), imebainisha kwamba hadi Juni 2022, kulikuwa na laini za simu za mkononi milioni 56.3.
Simu za mkononi zimeenea kwa asilimia 94 na matumizi yake kufanya miamala mbalimbali yamewezesha Watanzania wengi kujumuika katika mfumo wa kifedha wa kidijitali.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, anasema, pamoja na faida kwa watumiaji, wakala na taasisi za kifedha huduma za fedha kupitia simu za mkononi zimeiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na mfumo kamili uliowezesha mwingiliano wa mitandao ya fedha kupitia simu za mkononi.
Kuenea kwa matumizi ya simu kwa miamala ya kifedha kumekwenda sambamba na kukua kwa matumizi ya simu za mkononi.
Akaunti za pesa kupitia simu zimekuwa kwa kasi, taarifa ya mwaka 2019/2020 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kwamba miamala ya kifedha kupitia simu za mkononi imekuwa kwa asilimia 21.8 kwa ukubwa na asilimia 8.9 kwa thamani ya miamala ukilinganishwa na ile ya mwaka 2018/2019.
Kimsingi, ukusanyaji wa takwimu katika sensa una lengo la kuwezesha mipango ya taifa kwa lengo ka kuboresha maisha ya watu, kufanya uamuzi wenye ushahidi, kujua hali ya wananchi na uchumi kwa ujumla, kupata nyenzo za kutatulia matatizo ya maendeleo na kuhakiki utekelezaji wa malengo ya kitaifa ya kimkakati.
Vilevile takwimu zinaiwezesha serikali kulinganisha mipango yake na rasilimali zilizoko, kujua mahitaji ya wananchi, kupitia upya mipango na mikakati kwa malengo ya kuiboresha na kutumia raslimali kwa njia endelevu.
Tanzania inatelekeza mpango wa kujenga uchumi wa kidijitali, kuimarisha mawasiliano vijijini na kupunguza gharama za uendeshaji serikali na kuifanya kuwa kitovu cha biashara mtandao Afrika ya Mashariki na miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ushirikiano Kusini mwa Afrika (SADC).
Haya yanahitaji takwimu sahihi za mawasiliano ili kuwezesha huduma zinazotarajiwa kufikia malengo hayo kufanya kwa usahihi na usanifu.
Wananchi wakumbuke takwimu ni muhimu kwa watoa huduma kuchambua idadi ya watu, mahali walipo, umri wao, elimu zao na shughuli zao za kujikimu na kuandaa mikakati ya kuwafikia na kuendelea kuwahudumia.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







