Katiba mpya ikamalize utata usawa kijinsia

24Aug 2022
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Katiba mpya ikamalize utata usawa kijinsia

USAWA wa kijinsia unalenga kuhakikisha uwepo wa haki za  binadamu kwa wanawake na wanaume ili washiriki kikamilifu kwenye maendeleo ya taifa lao.

Halikadhalika kwa kuyaangalia makundi dhaifu kwenye uongozi yanayowekwa pembeni wakiwamo wanawake ili kuwawezesha na kuwapa nafasi kwenye kushiriki majukumu ya kuendeleza jamii zao.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, haki za binadamu ambaye ni mtafiti wa mambo ya maendeleo ya jamii, Deus Kibamba, anashauri kuwa usawa wa kijinsia uzingatiwe pale panapofanyika uteuzi wa aina yoyote ili kuyapa makundi yote wanawake, wanaume, wenye ulemavu na vijana nafasi.

Anashauri kuwa katika nafasi za kuchaguliwa kuna maeneo wanazingatia usawa wa kijinsia na kwamba yote yatatimia iwapo  katiba itaandikwa upya na ikitamka na kueleza maeneo ambayo ni lazima kuwepo na usawa huo katika uteuzi na kupendekeza hatua za kuchukuliwa kwa watakaopuuza.

Anasema katiba ina umuhimu wa kuainisha maeneo unapohitajika usawa kwa sababu bungeni leo,  idadi ya wanawake ni asilimia 39, viti maalumu asilimia 9, madiwani wakuchaguliwa Tanzania Bara ni asilimia 7 na wanawake waliochaguliwa kwenye serikali za mitaa ni asilimia 2.6.Ikiwa hali ndiyo hiyo kwa wanawake katika nafasi za kuchaguliwa ukweli ni kuwa ni wachache na kumekuwa na changamoto zinazosababisha hata masuala ya wanawake yasifanyiwe kazi hasa huduma za kijamii.

Ni ukweli kuwa zipo sehemu ambazo mamlaka na uongozi wenye usawa kati ya wanawake na wanaume unapatikana lakini  sehemu nyingine wanawake wanakosekana.

Ndiyo maana  kuwapo na vigezo ambavyo  vitaonyesha kipi cha kuzingatiwa kwenye katiba ili kuwa na  usawa wa kijinsia ni suala lisilokwepeka wakati huu wa kuandaa katiba mpya inayotegemewa kubeba maoni mbalimbali ya Watanzania wa jinsia zote.

 

Ni vyema pia kuwa na kampeni ya kuchagiza mamlaka zinazoteua ziwekewe vigezo na masharti ili kuwepo usawa katika kuwateua viongozi kiusawa. Wanawake wakitakiwa kuteuliwa kwa ulinganifu au uwiano sawa sawa na ule wa wanaume bila kuwasahau wenye ulemavu, vijana na makundi kama hayo.

 

Takwimu zinazotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi zinaonyesha kuwa  kipindi cha mwaka 2018 uteuzi uliofanywa na awamu ya tano ulifikia wateuliwa  463 na kati yao  wanawake walikuwa 37 sawa na asilimia 7.0 huku wanaume walioteuliwa  wakiwa 426 sawa na asilimia 92.01.

 

Liliana anaeleza kuwa uteuzi huo unaibua hisia kuwa hizo  hisani za kiongozi aliyepo madarakani kwa wale anaowapa majukumu, kinachotakiwa  ni kuwepo sheria ambayo itaelekeza kuwepo na usawa katika kuwateua watendaji na viongozi na kila atakayeingia madarakani afuate utaratibu huo ili kuendeleza usawa wa kijinsia.

 

Ili kuondoa fikra hizo yote hayo yatafanikiwa iwapo Tanzania itaandaa katiba mpya ambayo itabeba mambo mengi ya kuzingatia usawa, kuanzia kwenye ulingo wa siasa, uongozi wa taasisi za umma na binafsi. 

 

Ukiañgalia katika vyama vya siasa uteuzi wa wagombea, viongozi na wawakilishi mbalimbali unajaa ukakasi kwa kuwa ni kioo cha mfumo dume ambao bado inatamalaki katika nafasi za juu za uchaguzi wa viongozi.

Anasema sheria za vyama vya siasa zinawataka  kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia, lakini ni vichache vina katiba zinazozingatia suala hilo na vingine vingi vinaendeleza mfumo dume, hivyo dawa ni katiba na si vinginevyo.

 

Vyama vya siasa ifike wakati viachane na mfumo dume kutokana na ukweli kuwa mchango wa kila mmoja awe mwanamke, wanaume mwenye ulemavu, kijana na raia yeyote mchango wake unahitajika kwenye maendeleo ya taifa.

 

Yote hayo yanawapa wabunge jukumu la kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kisheria, kisera, miongozo ili kuwa na Tanzania yenye usawa na inayoshirikisha wadau na raia wake wote bila kujali changamoto za kimaumbile wala jinsi zao.