Ndivyo sensa ilivyo muhimu kwa elimu

23Aug 2022
Pankras Luoga
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ndivyo sensa ilivyo muhimu kwa elimu

KUJUA idadi ya watu, viwango vya elimu na mahitaji yao kielimu ni msingi wa kufikisha huduma bora za elimu kwa kila mwananchi. Leo ikiwa ni Siku ya Sensa ya Watu na Makazi, ni muhimu kwenye elimu ili kukusanya taarifa mbalimbali zikiwamo uchumi, makazi, nishati na elimu kutoka kwa wananchi wote.

Ni muhimu wananchi wakazijua faida za takwimu zitokanazo na sensa katika kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma  zote zikiwamo za elimu.

Kwa kifupi kujua faida hizo ni muhimu ili kuongeza uelewa na hamasa ya wananchi kushiriki sensa kikamilifu na kutoa taarifa za kweli.

Baadhi ya faida za sensa katika kuboresha elimu ni pamoja na takwimu za sensa zitasaidia Wizara ya Elimu kujua viwango vya elimu vya Watanzania wote na kuandaa sera na mipango kulingana na idadi, viwango vyao na mahitaji ya kielimu ya watu.

Tukumbuke kuwa kipindi hiki Wizara ya Elimu ipo katika mchakato wa mabadiliko ya mitaala ya elimu ili kuendana  na maendeleo ya sayansi na teknolojia na mahitaji ya wakati uliopo.

Hivyo, takwimu hizi za sensa zitasaidia utekelezaji wa mchakato huo muhimu unaotegemewa kuleta mabadiliko na maendeleo makubwa katika sekta ya elimu. Mfano kwa kujua idadi ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika, wizara itandaa mpango maalumu kwa kuanzisha masomo ya watu wazima ili kupunguza idadi ya wasiojua kusoma na kuandika.

Pia, idadi kubwa ya watoto katika eneo flani itaonyesha uhitaji wa kuongeza madarasa na walimu zaidi kulingana na kiwango cha watoto waliopo.

Wananchi waelewe kuwa, mipango na utoaji huduma za elimu nchini hufanywa kwa kuzingatia takwimu za sensa.

 Mathalani, ujenzi wa shule ya msingi au sekondari iwe vijijini, kwenye kata, wilaya na mijini hutegemea idadi ya watoto wenye umri wa kuanza shule.

Na zaidi, takwimu hizi za sensa kuhusu idadi ya watoto itasaidia sekta ya elimu kupata uwiano wa mgao wa rasilimali kama vile fedha za kuendesha shule kwa ngazi au sehemu inayojengwa.

Mfano katika mgao wa fedha za elimu  huzingatia idadi ya wanafunzi katika eneo shule inapojengwa. Mfano shule ya msingi yenye jumla ya watoto 250 haiwezi kupata mgao sawa wa fedha na ile yenye watoto 500 hata kama zote ni shule za msingi.

Na mwisho upatikanaji wa takwimu sahihi za sensa utafanikisha kufanya tathimini na kufuatilia walimu katika jamii hasa kwa kulinganisha idadi ya wananchi waliofikiwa na huduma za elimu kwa kuangalia jumla ya wananchi wa eneo hilo.

Hivyo, takwimu za sensa zitasaidia wizara ya elimu kutoa huduma inayoakisi mahitaji ya elimu ya wananchi katika eneo lao.

Wito wangu ni kwamba, kutakuwa na faida nyingi zitokanazo na takwimu za sensa katika kuboresha elimu ya Watanzania.

Na baadhi ya faida hizo ni kufanya mgawanyo sahihi wa walimu, madarasa na fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za elimu ikiwa ni pamoja na manunuzi ya vifaa, ujenzi wa madarasa, na upanuzi wa shule kulingana na kuongezeka kwa idadi ya watoto.

Utekelezaji kikamilifu wa haya yote hutegemea upatikanaji wa takwimu za sensa, hivyo ni muhimu kila mwananchi ahamasike kwa kushiriki na kutoa taaarifa sahihi bila kuficha kitu chochote leo ili taifa liboreshe elimu.

 

Mwandishi ni Mhadhiri Msaidizi Usimamizi, Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Afya MUHAS

Maoni: 0757645746.