Tumeona baadhi ya rafu ambazo si za kiungwana, badala yake ni zile ambazo zinaweza kumfanya kumaliza kabisa karia ya mchezaji mwenzake.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha Jumamosi iliyopita, alilalamika kuhusu mwamuzi kutochukua maamuzi stahiki kwa baadhi ya matukio ambayo yalionekana ni ya kadi nyekundu.
Akasema si kwa wachezaji wa timu yake tu, bali kwa wachezaji wote wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara. Nabi akasema kuna baadhi ya rafu si za kiungwana, bali ni za kuumizana, lakini waamuzi wamekuwa wakishikwa na kigugumizi kutoa maamuzi.
Analozungumza kocha huyo ni kweli kabisa. Waamuzi wa Tanzania wamekuwa hawawalindi wachezaji, badala yake wamewafanya kuwa kama wanyama ambao hawahitaji kulindwa kwa kuchezewa rafu mbaya, kusukumwa na kufanyiwa kila aina ya vitimbi bila wao kuchukua hatua.
Hii haijaanza msimu huu. Hata msimu uliopita, wachezaji wa Simba walikuwa wahanga wa rafu zisizo na kichwa wala miguu kiasi cha hadi katikati ya msimu wakawa na majeruhi zaidi ya watano.
Imefika mahali sasa wadau wa soka waanze kupaza sauti kuwaamsha waamuzi wetu ambao inaonekana mpaka mtu apasuliwe na kutokwa damu ndiyo waone ni rafu ya kadi nyekundu.
Uchunguzi wangu mdogo unaonyesha waamuzi wengi wa Tanzania ama kwa kushindwa kutafasiri sheria, woga, au kwa kutaka kusawazisha mambo wamekuwa wakizihesabu rafu badala ya kutoa adhabu kulingana na aina ya faulo yenyewe.
Kuna faulo ambayo kwa wenzetu hata ikichezwa mara moja tu, moja kwa moja ni kadi nyekundi bila kuangalia mchezaji huyo ameifanya mara ngapi na wapi, lakini huku unaweza kukuta mchezaji hata kadi ya njano hapati.
Mchezaji anataka kumvunja mwenzake mguu, anapandisha mguu kichwani, anamkata kwa nyuma, au kumsukuma, hizi zote ni rafu za kadi nyekundu tu, na wala hakuna kupepesa macho.
Hata hivyo waamuzi wetu wamekuwa waoga sana kutoa kadi ya moja kwa moja, badala yake ataanza kumhesabia alifanya mara ngapi kwa hiyo aliyoifanya ni ya mwisho.
Hii ina maana waamuzi wetu wanahesabu faulo ili watoe kadi. Ya kwanza hawatoi, ya pili anaonya, ya tatu anatoa kadi ya njano, ya nne amfuaata na kumuonyesha vidole kukumbusha ni faulo ngapi, ili mradi tu mpaka akitoa nyekundu ujue huyo mchezaji ameshindikana.
Nina uhakika, kama mwamuzi anatoka nje umpe kuchezesha Ligi ya Tanzania, anaweza kutoa kadi hata nne nyekundu kwenye mechi moja.
Unachezwa mpira kama wa mchangani kabisa na waamuzi nao wamekubaliana na hilo. Cha ajabu ni kwamba baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakitoa video fupi kwenye baadhi ya mechi ambazo wao wanapenda kuzitoa.
Ifike wakati waamuzi sasa waanze kudili na wachezaji wakorofi ambao badala ya kuonyesha ufundi uwanjani wao wanakuwa na mikakati ya kuwaumiza wenzao.
Watu wameweka pesa kwenye ligi ili kuangalia ufundi na baadhi ya wachezaji, hivyo kukitokea wachezaji ambao hawatumii ufundi badala yake wanatumia nguvu zisizostahili waadhibiwe na waamuzi.
Na nikisema waadhibiwe si wa timu ndogo tu, hata kubwa kama za Simba, Yanga na Azam. Wakati mwingine waamuzi wamekuwa hawawachukulii hatua wachezaji wa timu ndogo kwa kucheza vibaya kwa sababu na wao wanachezewa na wachezaji wakubwa na hawaadhibiwi.
Haya yakiendelea yanaweza kusababisha maafa siku moja uwanjani, mchezaji akapoteza maisha au akapata ulemavu wa kudumu na baada ya hapo ndiyo kuanze kutolewa matamko na maagizo wakati tayari mambo yameharibika.
Nadhani waamuzi wenyewe wanajua kabisa rafu za kimpira na zisizokuwa za kiungwana, wanatakiwa watoe maamuzi sahihi bila ya kuogopa ni mchezaji wa timu gani au mashabiki. Sidhani kama kuna shabiki atalalamika kwa muda mrefu mchezaji wa upande wao atakapofanya faulo iliyostahili kadi nyekundu.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







