Ni taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi imeitaka kanuni hiyo kuwa ni ya 19 kuhusu Ngao ya Jamii.
Kwenye taarifa yake, Bodi ya Ligi ikabainisha kuwa endapo bingwa wa Kombe la Shirikisho atakuwa miongoni mwa washindi wa nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, timu iliyoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi itashiriki shindano hilo.
Wadau mbalimbali wa soka wameyapokea kwa mawazo tofauti mabadiliko ya kanuni hiyo.
Wapo wanaoonekana kama wamechanganyikiwa na haelewi ni kwa nini Bodi ya Ligi imeamua hiyo, badala yake wameona ingeachwa vile vile tu.
Binafsi naona ni kama kuboresha timu zetu ambazo mara nyingi hazipati mechi nyingi, hasa za kirafiki.
Ukiangalia shindano hili, utagundua kuwa litachezwa kipindi ambacho ligi inakaribia kuanza, kama vile Simba na Yanga zilivyocheza mechi ya Ngao ya Jamii hivi karibuni.
Naweza kusema shindano hili linaweza kabisa kuzisaidia timu kuangalia wachezaji ambao wamewasajili, pamoja makocha kuangalia mapungufu.
Linaweza kuzifanya timu zikapata muunganiko kabla hata ligi haijaanza.
Pia timu inaweza kuona mapungufu na kocha akaamuru kufanya mabadiliko ya usajili, yaani kuongeza wachezaji wengine baada ya kuona kuwa eneo lina mapungufu kabla kuanza kwa ligi na mechi za kimataifa.
Hizi ni baadhi ya faida zinazoweza kupatikana michuano hiyo itakapoanza msimu huu utakapoamalizika.
Yaani timu nne, tatu za juu kwenye ligi na moja bingwa wa FA zinacheza ligi ndogo kusaka mshindi wa FA, badala ya kanuni ya zamani ambayo inamtaka bingwa wa Ligi Kuu kucheza na wa Kombe la FA.
Na kama bingwa wa Ligi Kuu na huyo huyo ni wa FA, basi atacheza na mshindi wa pili wa Ligi Kuu kama ilivyokuwa kwa Yanga na Simba zilivyocheza.
Hata hivyo, niwape ushauri Bodi ya Ligi ili michuano hiyo iwe ya kufana na isiwe bora liende.
Ukiangalia sana kwa jicho la tatu utaona tatizo la michuano hiyo ni muda. Msimu uliopita Ligi Kuu ilichelewa kumalizika na kama ingeamriwa ichezwe michuano hiyo, basi saa hizi hata ligi ingekuwa haijaanza.
Pamoja na matatizo mengi, ikiwamo ushiriki wa michuano ya kimataifa, ugonjwa wa UVICO na kuipa nafasi timu ya taifa, Taifa Stars kujiandaa, lakini mechi za mchujo zimekuwa nyingi sana ambazo hazina ulazima wowote.
Bodi ya Ligi ingepunguza mechi za mchujo ili kutoa muda wa ligi kumalizika mapema kwa ajili ya kupata muda wa kucheza michuano hiyo mifupi.
Haingii akilini, timu za Ligi Kuu zinacheza mechi za mchujo mechi mbili, halafu inayofungwa inakwenda kucheza tena mechi mbili za mchujo na timu za Ligi ya Championship.
Haya ni matumizi mabaya ya muda. Ili michuano hiyo ipate nafasi na ligi ianze mapema, nashauri kuwa timu itakayoshika nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara zikicheza mechi ya mchujo nyumbani na uganini, itakayopata matokeo mabaya ya jumla ishike moja kwa moja daraja ili tusipoteze muda.
Na timu inayoshika nafasi ya tatu na ya nne kwenye Ligi Kuu zicheze na itakayoshinda ipande moja kwa moja Ligi Kuu badala ya kuwa na mlolongo wa mechi nyingi ambazo ukija kuziunganisha na michuano ya Ngao ya Jamii ligi inaweza kuchelewa kuanza bila sababu maalum.
Vinginevyo inaweza kuwafanya hata wachezaji wakose muda wa kupumzika ligi itakapomalizika, kwani zipo timu zinakwenda kucheza mchujo na hapo hapo zianze shindano hilo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







