Ufugaji kisasa si wa kupuuza tena

19Aug 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ufugaji kisasa si wa kupuuza tena

UFUGAJI wa kisasa unaweza kufungua milango ya ustawi kiuchumi kwa kuzalisha mazao yenye ubora kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.

Kufuga kisasa kunawaongezea wafugaji mapato kwa vile wanatumia teknolojia ya uhimilishaji (kupandisha majike kwa chupa), unaowezesha kuchagua mbegu bora ya ng'ombe anayetoa maziwa mengi.

Ukweli huo unatokana na ukweli kwamba, teknolojia ya uhimilishaji inaboresha mbegu za wanyama na kumpatia mfugaji rasilimali za kuendesha viwanda vinavyotengeneza bidhaa zitokanazo na maziwa au ngozi. 

Kuna haja ya wafugaji wa ng'ombe kubadili mtazamo na kuanza kufuga kibiashara, kwa kutumia teknolojia hiyo ya uhimilishaji, ambayo inaelezwa kuwa ni mkombozi kwa kuleta mapinduzi  kwa wafugaji wengi. 

Iwapo mfugaji atakuwa na ng'ombe bora anayetoa wastani wa lita 20 kwa siku, na kuwa na uwezo wa kupata shilingi 20,000 kwa siku, Shilingi 600,000 kwa mwezi, kuna haja gani ya kumiliki ng'ombe wengi wasiolishwa kikamilifu? 

Kiasi hicho cha lita na fedha, kwa mfugaji anayeanza na ng'ombe mmoja, akiwa na ng'ombe watano, anaweza kupata Shilingi 100,000 kwa siku, ndiyo maana  kubadili mtazamo ni jambo muhimu.

Pamoja na kuingiza fedha nyingi kupitia ng’ombe wachache, mfugaji anakuwa na uhakika wa kupata nyama na ngozi bora baada ya ng'ombe wanapofikisha umri wa kuuzwa. 

Kwa maelezo hayo  ni wazi mifugo michache ni utajiri, hivyo, kilichobaki ni wafugaji kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Mifugo, ili kuanzisha miradi ya ufugaji wa kisasa wa ng'ombe bora.

Hatua hiyo inaweza kusaidia kuachana na mtindo wa kuhama huku na kule wakati wa kiangazi na kusababisha migogoro kati yao na wakulima, kwani watakuwa na mifugo michache yenye faida kubwa inayozalishwa kwa ghrama ndogo. 

Ikumbukwe, wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961, ilikuwa na ng'ombe milioni tisa, lakini hadi sasa wameongezeka hadi kufikia milioni 30.5, huku idadi ya watu ikiongezeka kutoka milioni 10 wa wakati huo hadi milioni 55. 

Takwimu hizo, ziliwahi kutolewa na serikali ya awamu  ya tano ya Hayati  John Magufuli, katika moja ya mikutano yake ya hadhara na kufafanua kuwa pamoja kuongezeka ng'ombe na watu, ukubwa wa ardhi ni ule ule hauongezeki. 

Katika ushauri wake, alisema mifugo inaongezeka, watu wanaongezeka, shughuli mbalimbali zikiwamo za kilimo, zinaongezeka, na kwamba mtindo wa kuwa na ng'ombe 5,000 na kuzunguka nao,umeshapitwa na wakati.

Hivyo, akashauri wafugaji kufuga kisasa ili kuepuka migogoro kati yao na wakulima, ambayo wakati mwingine inasababisha maafa kutokana na kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.Akawataka wenye ng'ombe wengi wavune wachache wajenge hata nyumba za mabati na kuchimba bwawa la maji, kwa ajili ya mifugo yao badala ya kuendelea kuishi maisha ya kutangatanga.Ninadhani kwamba, kama wafugaji watazingatia ushauri wa viongozi wa serikali, ni wazi itakuwa ni fursa nzuri ya kiuchumi ambayo inaweza kuwafanya wapige hatua kwenda mbele katika maendeleo.

Vilevile mifugo mingi inapokula nyasi nyingi, kucheua , kuzalishaji samadi, na mkojo huongeza hewa ukaa inayochangia uharibifu wa mazingira hasa hewa na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.

Wanyama wachache wanaolishwa kitaalamu tena vyakula visivyotoa gesi nyingi na hewa ya ukaa ni tija pia, kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi.