Kama ‘kiroba’ kilivyokoma ukatili utokomezwe sasa

18Aug 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kama ‘kiroba’ kilivyokoma ukatili utokomezwe sasa

IWAPO serikali ilikomesha ufungashaji wa pombe kwenye mifuko ya nailoni almaarufu ‘kiroba’ ni wakati wa kubuni na kuibua mikakati mahsusi ya kukomesha ukatili wa kijinsia na kuwa historia.

Kuna haja kwa sababu matukio ya ukatili 11,499 yaliripotiwa kuanzia  Januari hadi Desemba mwaka jana, huku ubakaji ukiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya visa 5,900. Kingine kinachofuata ni mimba za utotoni 1,677 na ulawiti matukio 1,474, huku ikielezwa kuwa matukio mengi hayaripotiwi kwenye vyombo vya dola.

 Ni taarifa ya hivi karibuni ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, anayetaja mikoa inayoongozwa kwa ukatili kuwa ni Arusha, Tanga, Shinyanga na Mwanza.

Kwa taarifa hiyo, ni wazi kwamba kila mmoja ana jukumu la kufanya, kwa ajili ya kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia na kuvipunguza.

Kila mmoja akishiriki katika vita dhidi ya vitendo vya ukatili huo, jamii inaweza kubadilika na kuchukua hatua za kuvikomesha au kutoa taarifa kwa vyombo vya dola, ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watuhumiwa.

Waziri Gwajima, anasema serikali imejizatiti kumaliza vitendo vya ukatili kwa kutoa adhabu kali kwa wahusika, lakini kuhamasisha jamii na anaomba ushirikiano wa Watanzania ili kukomesha vitendo hivyo.

Kwa ombi hilo la serikali ni vyema hilo likafanyika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za kuwapo kwa vitendo hivyo au hata viashiria vyake kabla havijasababisha madhara kwa watoto wa kike na kiume.

Katika jitihada za kukabiliana na vitendo hivyo, Waziri anaeleza kuwa  milioni 119. 6 zimetengwa kwa ajili ya kampeni iitwayo "Twende Pamoja, Ukatili Tanzania Sasa Basi", yenye lengo la kujenga uelewa kwa jamii kuhusu usawa wa kijinsia na kupinga ukatili.

Hatua hiyo imekwenda sambamba na kampeni nyingine ya kupinga na kutokomeza ukatili inayoitwa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA), ambapo anafafanua kuwa kufikia Julai mwaka huu, watu 8,000 walikuwa wameshajiunga nchini kote.

Kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na serikali, inaelezwa kuwa imesaidia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa vyombo vya dola kwa kipindi cha mwaka 2020/21 ambapo matukio 20,025 ya ukatili yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 18,270 yaliyofikishwa polisi mwaka 2019/20.

Pia, imesaidia kuanzishwa kwa madawati ya jinsia yanayoshughulikia mashauri ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kufikia 420 katika vituo vya polisi na madawati mengine 153 katika Jeshi la Magereza.

Vilevile, zimeanzishwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 18,186 kitaifa, mkoa, wilaya, kata na kwenye baadhi ya mtaa, vijiji na vitongoji, zinazoendelea kufanya kazi.

Jambo la muhimu kama nilivyoeleza awali, ni kila mmoja wetu kwa nafasi yake kupiga vita vitendo hivyo, kama njia mojawapo ya kushirikiana na serikali, ili kuhakikisha jamii inaishi kwa amani bila vitendo hivyo.

Ikumbukwe kuwa, ukatili huo unatajwa kuwa ni kitendo ambacho mtu yeyote anaweza kufanyiwa, awe mwanamke au mwanaume, kwa lengo la kumdhuru ama kumuumiza kisaikolojia, kimwili, kiafya, kingono na kiuchumi.

Kwa mfano ukatili wa kimwili, ni pamoja na kupigwa, kusukumwa, kuporwa, kukeketwa na kadhalika. Lakini pia upo ukatili wa kisaikolojia, ambao ni vitendo anavyofanyiwa mtu ili kumwathiri kiakili.

Vitendo hivyo vinajumuisha kutukanwa, kufokewa, kutengwa, kudhalilishwa kwa maneno, vitendo vya ishara, gubu, kusingiziwa, kuaibishwa au kuhukumiwa bila kuwa na kosa.

Upo pia ukatili wa kingono, ambao unahusisha kubakwa, kukosewa uaminifu, kufanyiwa ngono bila kinga, kushikwa sehemu za mwili bila ridhaa, lakini pia kuna ukatili wa kiuchumi unaotokana na kukosa sauti katika mali inayokuhusu.

Ukatili huo wa kiuchumi unahusisha pia kufanyishwa kazi kwa malipo kidogo, kutomiliki mali inayokuhusu, usafirishwaji wa wanawake na watoto kwenda kufanyishwa kazi bila ridhaa yao.

Vilevile, kuna ukatili wa kiafya ambao unaambatana na kukosa haki ya uzazi ya kujifungulia hospitalini, mume kumnyima mke pesa ya kwenda hospitali. Mume kumzuia mke kutumia uzazi wa mpango.

Ikumbukwe unagusa matumizi ya mipira ya kiume (kondomu), mwanaume kutokuwa tayari kutumia mpira huo, wanaume kupimwa VVU na UKIMWI na kumficha mkewe matokeo au kumtuhumu kumwambukiza.