Wazazi tuwe mabalozi wazuri kutokomeza uhalifu nchini

22Sep 2022
Pilly Kigome
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazazi tuwe mabalozi wazuri kutokomeza uhalifu nchini

IFIKIE hatua wazazi wawe jeshi kubwa linalosaidiana na polisi nchini kukabiliana na tatizo la uhalifu unaofanywa na watoto wetu. Tuwe katika nafasi ya kuweza kukabiliana na hata kuondoa tatizo la uhalifu  ilikosimamia.

Wazazi inatupasa tuchukue hatua stahiki kuanzia ngazi ya familia, ili kuweza kutokomeza kabisa tatizo la uhalifu nchini, unaofanywa na watoto chini ya miaka 18 kwa kila namna na hata zaidi ya hapo, bado ni tegemezi kwa wazazi wao.

Makundi hayo yanavamia nyumba za watu usiku na kupora vitu mbalimbali kwenye nyumba hizo, kisha wanaondoka navyo, ikiambatana na vitendo vya kuua raia wanaoonekana kuonyesha ukaidi kwao.

Hivyo nasema, ni wakati wetu wazazi kuongeza nguvu katika upande wa malezi kuhoji na kudadisi kujua ama kazi au shughuli wanazojishuhulisha nazo watoto wetu, ili kwa pamoja waondoe tatizo hilo nchini, kwani kufanya hivyo kutarahisisha ama kujua au kugundua kiurahisi shughuli kama kazi anayofanya mwanao.

Inasemekana katika kuaminika, kuna baadhi ya wazazi wanapokea zawadi za thamani kutoka kwa watoto hao zikiwemo televisheni za kisasa na mzazi anapokea pasipo kuhoji, wakati akijua mtoto huyo hana kazi wala biashara na mbaya zaidi, wengine wanatakiwa kuwepo shule. 

Sasa inakuwa wazi zaidi, yameibuka makundi ya uhalifu yanayojihusisha na wizi, yakiwemo maarufu wa jina ‘panya road’ yanayoendelea kutishia maisha ya usalama wa raia na mali zao, hali inayozua hofu kubwa kwa wakazi na hasa mkoani Dar es Salaam.

Ni makundi yanayojihusisha na kunyang’anya, kujeruhi, kupora, kuiba na hata kuua, jambo linaloleta taharuki hata kuwafanya watu kupunguza saa za kufanya kazi na shughuli nyinginezo za kujiongezea kipato cha kila siku, wakijihami dhidi ya taharuki hiyo.

 

Tukiwa wazazi muda sahihi umefika tuwe mabalozi namba moja wa kutokomeza tatizo hilo nchini kote. Naamini, tukishirikiana pamoja tunaweza.

Inaaminika awali na hata sasa, kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakipokea zawadi kutoka kwa watoto wao na kupokea zawadi hizo bila kuhoji ama kudadisi imetokea wapi hali ya kuwa mtoto hana kazi au biashara yoyote.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ametoa wito kwa wazazi kuweza kufuatilia mienendo ya watoto wao na shughuli zao wanazozifanya za kila siku za kujiingizia kipato, ili kubaini na kujiridhisha kazi wanazofanya.

Makala anawataka wazazi kushirikiana waweze kuisaidia polisi kukabili tatizo kabla halijafika pabaya zaidi na kuna baadhi yetu wazazi tunaelewa mienendo ya watoto wetu.

Makala anasema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, imejipanga na kujiwekea mikakati madhubuti na tayari wameshawakamata watuhumiwa wa uhalifu 135, vijana sita wametangulia mbele ya haki katika mchuano na polisi.

Mkuu wa Mkoa, anasema vijana hao wote kwa pamoja, ni wale wanaojihusisha na uhalifu kama wizi, unyang’anyi wa mali mfano; televisheni, redio, simu na hata pesa kutoka kwa raia wema na wanaenda kuviuza.

Mbali na hilo, anafafanua kwamba tayari wameshaweza kuwatia mbaroni wanunuzi watano wakubwa wanaonunua bidhaa za wizi, kutoka kwa wahalifu hao maarufu kama ‘panya road.’

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, anatoa wito kwa wananchi kuweza kushirikiana pamoja kutoa taarifa kwa jeshi hilo na kuwatoa hofu kwamba, kutakuwa na usiri mkubwa kwa atakayetoa taarifa hizo.

“Jeshi la polisi halijawahi kushindwa na halitegemei kushindwa, wahalifu wakae chonjo na wale wote wanaojaribu kuchezea wasimamizi wa sheria,” anasema Muliro

Tayari tunaambiwa, jeshi la polisi limeshachukua hatua kwa mujibu wa mamlaka na wajibu wake, sita kati ya tisa wanaosadikiwa kuwa ‘panya road’  wamekufa, katika mapambano na polisi waliokuwa wanawakabili.