Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo za kutaka kuinua makundi hayo kiuchumi, kumekuwapo sintofahamu ya kutorejeshwa fedha hizo kwa wakati au kutorejeshwa kabisa hali inayoweza kukwamisha wengine kukopeshwa.
Kwa mfano hivi karibuni, Mbunge wa Kinondoni Dar es Salaam, Abbas Tarimba, alisema katika kipindi cha mwaka jana, Halmashauri ya Manispaa Kinondoni ilitoa fedha za mikopo Sh. bilioni 3.5.
Akaeleza kwamba, kwa kuwa mikopo iliyotolewa kwa vikundi, asilimia 31 ya fedha hazijarejeshwa, anaishauri serikali kufanya ukaguzi, ili kujua mikopo hiyo inawafikia walengwa na kwa nini haijarejeshwa.
Urejeshaji mikopo katika halmashauri mbalimbali nchini umekuwa ukikumbwa na sintofahamu, hasa baadhi ya wanaokopeshwa kushindwa kurejesha. Ingependeza kama utaratibu huo ungebadilishwa.
Nadhani kwamba, badala ya kukopesha fedha, serikali ingeangalia uwezekano wa kununua vifaa na kukopesha vifaa kulingana na mahitaji ya vikundi, ili wahusika wavifanyie kazi ya uzalishaji mali.
Ukopeshaji fedha umeonekana kuwa na vikwazo vingi ikiwamo baadhi ya wakopaji kuzitumia kinyume na malengo na kujikuta wakishindwa kuzirejesha, hali ambayo inakwamisha mzunguko wa kukopesha wengine.
Imefikia wakati halmashauri zinatoa mikopo hiyo bila riba kama njia ya kuhamasisha makundi hayo yakope na kurejesha kwa wakati ili wengine walio kwenye foleni nao wakopeshwe, lakini bado kumekuwapo na ugumu.
Hivyo, nadhani njia nzuri ni kukagua vikundi na kuangalia mahitaji na kisha kuvigawia vifaa vya kufanyia, kama mafundi seremala wakopeshwe vifaa vinavyoendana na kazi yao, na kama ni vya wakulima nao vilevile.
Kama ni mama lishe, baba lishe na wajasiriamali wengine wakiwamo wanaofuga kuku, nao wakopeshwe vifaa vya shughuli zao, kwani hatua hiyo inaweza kusaidia fedha za umma kupotelea mikononi mwa watu wachache.
Nitoe mfano maelezo ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI bungeni, Festo Dugange kwamba, mwaka 2015 hadi 2020, serikali kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ilitoa Sh. bilioni 133 kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Lakini akabainisha kuwa katika kipindi hicho, jumla ya Sh. bilioni 92.21 tu sawa na asilimia 69.32 zilirejeshwa kutoka kwenye vikundi vya wanufaika, hali inayoonyesha kuwa kuna kiasi kingine cha fedha hizo hakijarejeshwa.
Natambua kuwa serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kutoa mikopo na urejeshaji mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kutoka kwa vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Lakini pamoja na kwamba mfumo huo wa kielektroniki unasaidia kujua kiwango cha mikopo na urejeshaji wake kwenye halmashauri zote 184 nchini, ninadhani utaratibu wa kukopesha vifaa ungefaa zaidi.
Kwa njia ya utoaji wa mikopo ya vifaa vya kufanyia kazi na hata fedha kidogo za mtaji, inawezekana kukawa na nidhamu kwani imeonekana baadhi ya wanaokopeshwa wameshindwa kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha.
Ukopeshaji wa vifaa unaweza kusaidia vikundi vingi zaidi kunufaika na hata kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya wanaohitaji mikopo, kwamba kuna ukiritimba kuipata.
Waswahili wana msemo wao kwamba dawa ya deni ni kulipa, lakini kwa kuwa inaonekana baadhi ya wakopaji wamekuwa wakishindwa kurejesha mikopo kutokana na kuelekeza fedha kwenye matumizi mengine, suala la kutafuta njia nyingine ya kuwasaidia, ninadhani halina budi kubuniwa.
Njia hiyo ni kuwakopesha vifaa wavitumie kuzalisha mali na kurejesha kidogo kidogo fedha zilizotumika kununua vifaa hivyo, ili wanapokamilisha kulipa deni vinakuwa ni mali yao.