Lakini, mambo hayajakaa sawa kwa sababu vyote hivyo havijawa na mchango mkubwa kwa pato la taifa kwa vile huchangia asilimia 1.71 pekee ni kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2019 zinazotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Taarifa hiyo pia ina mambo mazuri kuwa kwa mwaka 2020, sekta hiyo ilitoa ajira za moja kwa moja kwa takribani 202,053 kwa zaidi ya watu milioni 4.5 katika shughuli za uvuvi ukiwamo wavuvi, wasindikaji, wafanyabiashara wa samaki na wachuuzi wa zana za uvuvi.
Sekta hiyo pia ni chanzo cha lishe bora, ajira na kuongeza kipato, burudani, utalii na kufanikisha mikakati ya nchi ya kufikia lengo namba mbili la maendeleo endelevu kutokomeza njaa, kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora na kukuza kilimo endelevu.
Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hiyo kwa jamii na taifa, serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuiboresha ikiwamo kuweka mifumo ya kielektroniki ya ufuatiliaji wa mazao bahari ili kuyaongezea thamani pamoja na kuandaa mazingira bora kwa wawekezaji.
Pamoja na juhudi zote hizo kuna kundi moja muhimu la wavuvi ambalo pamoja na juhudi kubwa linazofanya ya kuhakikisha samaki wanafika sokoni, serikali na wadau wa sekta hiyo hawajawapa kipaumbele cha kutosha.
Nasema hivi kwa sababu kwa muda mrefu wavuvi wamekuwa wakilalamikia kusahaulika na kutaja changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli zao ikiwamo kutowapatia vifaa sahihi vya uvuvi, hali inayowasababisha kupata ajali za majini zinazowasababishia vifo na maradhi ya kudumu.
Wavuvi hao pia wamekuwa wakisumbuliwa na ukosefu wa elimu ya uzamiaji kwenye hali inayowasababishia kupata maradhi ikiwamo kupooza na kutoka damu za puani.
Asilimia kubwa ya wavuvi hapa nchini hasa wale wanaozamia kina kirefu chini ya bahari wanafanya shughuli hiyo kwa mazaoea na kufundishwa na wazazi na walezi wao au washirika wao kwenye kazi na si kupatiwa elimu ya kitaalamu na walimu wanaofahamu fani hiyo hali inayosababisha kukosa ujuzi muhimu ikiwamo vifaa vya kuvaa na mambo ya kuzingatia wakati unazama chini na kupanda juu ya maji.
Licha ya hayo, wavuvi hao wamelalamika kuwa ikitokea wamepata madhara hakuna hospitali maalum za wakuwapa matibabu hali inayowafanya kuelekea kwa waganga wa kienyeji wakiamini kuwa huko ndiko wako salama zaidi hali inayochelewesha matibabu yao au kusababisha vifo.
Hivi karibuni mvuvi Shabani Ally wa Kigamboni, aliiambia Nipashe kuwa alipata ugonjwa wa kupooza akiwa katika shughuli zake za kuvua samaki mita 20 chini ya bahari jambo lililomfanya kupumzika kwenye shughuli hiyo kwa takribani mwaka mmoja.
Kwa mantiki hiyo hali ikiendelea kuwa hivyo taifa linaweza kupoteza nguvu kazi hii muhimu katika sekta ya uvuvi, hali inayoweza kudhorotesha shughuli za uvuvi nchini.
Hivyo basi, wakati serikali inaweka mikakati ya kuboresha mifumo katika sekta hiyo, haina budi kuliweka kundi hilo katika mikakati hiyo ili likue pamoja na kuliko kuliacha nyuma likiangamia wakati mifumo mingine inazidi kuboreshwa.
Ili kuweza kutatua changamoto hizo kwa ufasaha serikali haina budi kukaa pamoja na kundi hili na kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa kushirikiana na viongozi wao na wataalamu wa wazamiaji.