Yeye alisema alichoona ni kuwa wasomi nchi hii wamekosa uwezo wa kuanzisha mambo- lack initiative. Aligusia mambo mengi katika nchi hii kwamba, yanashindwa kwenda mbele kwa sababu wasomi wamekuwa watu wa kulalamika badala ya kuwa wabunifu na kutoa majibu ya matatizo yanayolikumba taifa.
Alishangazwa, kwa kauli yake, kuona wasomi wanakuwa walalamikaji kwa sababu ya kukosa ajira; “mbona tuna vijana waliomaliza darasa la saba na wanajiajiri na kuwa matajiri, inakuwaje wasomi washindwe kujiajiri na kubaki kulalamika?” Aidha alisema ni kwa sababu hiyo wasomi wanakosa uwezo wa kuwa wabunifu, hata wanapopewa majukumu katika serikali wanafanyakazi kwa mazoea zaidi kuliko kujenga msingi wa kuwa na majibu mapya.
Alidhani kuwa kuna tatizo katika mfumo wa elimu yetu unahitaji kufanyiwa kazi.
Nilikubaliana na msomaji huyu kwa kiasi kikubwa juu ya wasomi kushindwa kutoa majibu mapya kwa matatizo ya nchi yetu. Ila nilitaka kuongezea yangu kuhusiana na hilo.
Kwanza msomaji akubali kuwa, mfumo wetu wa siasa hautaki wasomi.
Ukiwa msomi na kutaka uongozi unaweza ukapigwa chini kwa hofu tu ya unaowakuta kuwa utawapiku, lakini unapokuwa na mfumo wa siasa ambapo ukimaliza darasa la saba tu unaweza kuwa mbunge, au mwenye cheo fulani kisiasa unadhani usomi hapo unaweza kuwa na nafasi?
Wasomi wote hawanyamazi kimya, wengi wanafanya tafiti, wanaandika vitabu lakini nani anasoma, nani anajali? Wasomi wanaopendwa ni wale ambao wanakuwa kasuku wa matamshi ya wakubwa wao katika siasa.
Wale ambao wako madarasani wakifundishwa wanaimba nyimbo za matokeo ya tafiti zao kwa wanafunzi wao, maana wananchi wengi kwa ujumla hawasomi, na viongozi hawajali.
Ukiwa msomi, ukawa unazungumza kwa hoja, na sio kwa kusema zidumu fikra za kiongozi wako unakuwa adui wa chama na wanasiasa. Ifike mahali lazima tuweke vigezo vikali vya kielimu kwa ajili ya ngazi mbalimbali za kiuongozi na utawala.
Lakini wasomi pia wanatakiwa kufundishwa kwa msingi wenye kuimarisha ubunifu tofauti na sasa ambapo wasomi wanapikwa kwa msingi wa kukariri, huku elimu kwa vitendo na elimu ya kumsaidia msomi huyu kumalizi matatizo ndani ya jamii yake na ayatolee majibu haitumiki.
Niliwahi andika kuwa, kwa mfumo wa elimu yetu, si jambo la ajabu kumuona msomi wa shahada ya uzamivu anashindwa kuwa bingwa wa jambo fulani na akatumia elimu yake kutatua matatizo ya jambo fulani.
Kwanza kuna tatizo kubwa la ukosefu wa miundombinu ya kielimu, pili serikali haiweki fedha za kutosha kwa ajili ya kusaidia tafiti za wanafunzi, na ndio maana kuna idadi kubwa ya wasomi waliosoma kwa fedha za nje na wanapomaliza hawana fedha yoyote ya kuchapisha tafiti zao katika vitabu na pia kuendelea na utafiti wao.
Msomi anakuwa mtatuzi bora wa matatizo ya jamii kama serikali inampa fedha za utafiti na kumpatia fursa. Kama una shahada ya uzamivu na umeajiriwa serikali unakuwa na mkosi mkubwa, kwa sababu hatimaye utaishia kufanya mambo kwa mazoea na sio kwa kusaidiwa na tafiti.
Wale wanaobaki vyuoni ufundishaji wao huwasaidia kujenga misingi ya utafiti lakini fedha za kuendelea na kazi zao za utafiti si rahisi kupatikana.
Hayo yote ukichanganya na kipato duni cha wasomi na fursa chache za kujifunza kutoka kwa wenzetu kunafanya wasomi wawe kama ambavyo msomaji wangu anawalalamikia- kukosa ubunifu.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








