Rais Magufuli anapongezwa kwa sababu sehemu kubwa ya tathmini ya siku 100 tangu aingie madarakani, inaonyesha ongezeko la watu wenye imani kwa serikali yake.
Ingawa ni hivyo, wapo wachache wanaopata ujasiri wa kumjadili na kukosoa baadhi ya mambo, tena kwa nia njema.
Wanayaona mazuri anayoyafanya kuwa yalistahili, bali changamoto zilizopo zinahitaji ushiriki katika kuelekeza na kushauri. Hawafanyi kosa.
Mjadala kuhusu Rais Magufuli unakuwa wenye kupongeza zaidi kutokana na sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni mfumo wa utawala unaogusa hitaji la umma hasa uwajibikaji na udhibiti wa aina tofauti za ufisadi dhidi ya mali za umma.
Rais Magufuli amejipambanua kwa ‘kujitoa sadaka’ ili atekeleze wajibu wake kwa umma. Kujitoa sadaka kuna maana kubwa na pana.
Hitimisho la kujitoa sadaka ni juu ya ‘liwalo na liwe’ ama ‘ikibidi hata kufa’, lakini jambo fulani hasa lenye maslahi kwa umma lifanikiwe.
Kwa hiyo umma kwa sehemu kubwa unajiridhisha, unashangilia, unafurahia utendaji kazi wa Rais Magufuli. Na kwa hakika inastahili.
Lakini inapaswa kueleweka kuwa hatua anazozichukua Rais Magufuli zilikuwa sehemu ya azma yake katika nafasi mbalimbali alizozitumikia serikalini.
Kila wizara aliyopangiwa wakati wa awamu mbili za marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, Magufuli alionyesha uwezo wake kwa yale aliyoyayaamini na kuyasimamia.
Kwamba yalikuwa kwa maslahi ya umma. Kwa hiyo anapochukua hatua zaidi kutokana na kuwa na mamlaka ya juu ki-utawala, haipaswi kuwashangaza wengi.
Kwa sababu anayafanya hayo kwa utayari, dhamira, utashi na kusudio binafsi. Ukweli ni kwamba walikuwapo marais watatu baada ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, lakini hawakuyafanya hayo.
Wapo viongozi wengine wa aina ya Rais Magufuli katika ngazi tofauti ambao wana uthubutu kwa uongozi wao.
Viongozi hao akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, wanatekeleza wajibu na majukumu yao(zaidi) kwa utashi binafsi. Wana nguvu za ndani zinazowaongoza kuwaongoza watu.
Hawana hofu, hawana uwoga, hawana unafiki. Sasa viongozi wengi serikalini wanaimba wimbo wa Rais Magufuli, ‘hapa kazi tu’.
Wengine wanaimba pasipokujua namna ya kuucheza. Wanaiga miondoko ya Kiongozi Mkuu. Inakuwa vigumu kuimudu. Wanaouimba `wimbo’ huo walikuwa miongoni mwa walioimba wimbo wa ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’.
Wakati ule wa utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Waliuimba wakiiaminisha jamii kwamba Tanzania yenye neema inawezekana na kuwa utekelezaji wa ilani ya chama tawala ulivuka asilimia 80.
Bila shaka mioyo yao iliwasuta. Wengine miongoni mwao hawakuonyesha ujasiri na ari ya kuleta mabadiliko. Sasa pongezi zinapotolewa kwa Rais Magufuli, si jambo baya wala la kukejeli.
Lakini ipo haja ya kuifanya Tanzania kuwa na mifumo endelevu itakayomfanya kiongozi ama mtumishi wa umma kulazimika kuyafanya mema anayoyafanya Rais huyo wa awamu ya tano.
Rais Magufuli atakuwapo na baadaye kuondoka madarakani. Utakapoingia utawala mwingine mambo yanaweza kubadilika na nchi ikarudi katika ‘biashara kama kawaida’.
Ndio maana ninapoandika makala haya, ninaamini kwamba pongezi pekee kwa Rais Magufuli hazitoshi. Kwa maana wapo wanaojua namna bora ya kuzitumia pongezi ili kutimiza matakwa binafsi.
Ni wajuzi wa kupanga mtiririko wa maneno, ni weledi wa kutamka kwa ufanisi na mvuto unaojenga imani kwa jamii, kwamba wanachokizungumza ni sahihi.
Wenye ‘utaalamu’ huo wanaweza kutokuwa miongoni mwa wanaoipita njia moja na Rais Magufuli, lakini ili kutimiza matakwa yao, wanalazimika kumsifia na kumpongeza.
Lakini ili ‘neema ya Magufuli’ idumu katika Tanzania, yapo mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika, ikiwamo kuweka mifumo katika nyanja tofauti.
Mifumo itakayoufanya utendaji kazi uwepo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi. Kwa upande mwingine, lazima raia watambue umuhimu wa kujenga hoja zikiwamo zinazokosoa, zinazofikirisha, zinazohoji ama kuibua mjadala kuhusu utendaji wa Rais Magufuli na mwingine yeyote.
Jamii nzima ikijikita katika kumpongeza, kumshangilia na kumpigia makofi na wasaidizi wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu, haitakuwa na manufaa sana.
Lazima wawepo watu watakaotekeleza wajibu huo pasipo kutafsiriwa kuwa ni wahaini, maadui, wachochezi ama wenye sifa hasi kwa nchi na watu wake.
Kuibua fikra na mitazamo tofauti inayojikita kwenye masuala, ukweli na uhalisia, kutamsaidia na kumuimarisha Rais Magufuli hasa anapojikita katika ‘kuyatumbua majibu’.
Wenye wajibu huo wanaweza kuwa watu binafsi waliokuwa katika tasnia na kada tofauti ama wawakilishi wa umma kama wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ama madiwani.
Kutimiza wajibu huo kwa kada hizo kutachochea ufanisi zaidi kwa serikali ya Rais Magufuli, vinginevyo wasioitakia mema nchi watafanya usanii wa ‘kumwagia sifa’ ili wapate mianya ya kutenda yasiyo mema kwa umma.
Kukosoa kwa nia njema ni kuijenga jamii. Ndio maana wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alizungumzia umuhimu wa upinzani, kwamba unachangia kuifanya serikali iliyopo madarakani isilale.
Serikali ya Rais Magufuli haipaswi kulala. Inapoelekea kulala wananchi wanapaswa waiamshe na namna nzuri ni pamoja na kuhoji na kuweka mifumo rasmi ambayo awaye yote akichaguliwa kuwa Rais, ataifuata, ataitii na kuitekeleza.
Mungu ibariki Tanzania.
Mashaka Mgeta ni mchambuzi wa masuala ya siasa.
Anapatikana kwa simu +255 754691540, 0716635612 ama barua pepe:mgeta2000@yahoo.com ama mashaka.mgeta@guardian.co.tz. Mwisho



.jpg?itok=nfwjwDzv)








