Meya wa Manispaa hiyo ni Boniface Jacob ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ubungo ambaye siku chache baada ya kushinda nafasi hiyo alikabidhiwa ilani ya chama hicho ili aitekeleze kikamilifu.
Jacob alikabidhiwa ilani hiyo na Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Kasmil Mabina, aliyesema kuwa ilani hiyo imeorodhesha vipaumbele vya chama ikiwa ni pamoja na kushughulikia suala la bomoabomoa, maji na elimu.
Mabina alisema kuwa Meya Jacob ana jukumu la kushugulikia elimu katika manispaa yake na kuhakikisha anakusanya mapato ya kutosha kama chama kilivyokuwa kinaahidi.
Naye Jacob kwa upande wake akawatoa hofu wananchi kwamba, kukabidhiwa ilani ya chama haimaanishi atakuwa Meya wa Chadema ama Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa) tu, bali atayachukua mazuri yote kwa ajili ya manufaa ya wana- Kinondoni wote.
Nimeanza kwa kuelezea kidogo kile ambacho Meya huyo ameahidi nikiwa na lengo la kutaka kuzungumzia changa moto mbalimbali zinazoikabili Manispaa ya Kinondoni, ambazo zinahitaji kutafutia ufumbuzi haraka.
Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa maji ya bomba, maeneo ya kufanyia biashara ndogondogo wakiwamo machinga na mama lishe, migogoro ya ardhi, ukusanyaji wa mapato na mingine mingi.
Kwa ujumla, manispaa hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo hazina budi kutatuliwa haraka hasa kwa kuzingatia kwamba wakati wa kampeni, wagombea udiwani waliahidi kuzishughulikia.
Hivyo Meya kwa kushirikiana na timu yake ya madiwania bila kujali vyama wanavyotoka, waanze kushughulikia changamoto hizo ili kuboresha maisha ya wananchi.
Nakumbuka baadhi ya ahadi nyingine za Meya huyo alizowahi kutoa ni kuongeza ukusanyaji wa mapato mara tatu zaidi ya agizo la Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambalo ni Sh bilioni 48.
Fedha ndiyo kila kitu, kwa maana kwamba bila fedha manispaa hiyo haiwezi kusambaza maji kwa wananchi wake, haiwezi kuboresha shule, kuwaweka wamachinga na mama lishe katika mazingira rafiki ya kufanyia shughuli zao.
Ikumbukwe kuwa sio mikoani tu ambako wanasomea chini ya miti, bali hata jijini Dar es Salaam zipo shule za serikali ambazo wanafunzi wake wanasomea katika mazingira hayo ambayo hayawezi kutoa elimu bora.
Zote hizo na nyingine zenye changamoto kama za aina hiyo zinatakiwa kuboreshwa ili kusaidia kutoa elimu bora ambayo itawasaidia wanafunzi kufaulu na kusonga mbele zaidi kielimu.
Kwa kuwa meya ameshaahidi, basi ahadi zake sasa ziwekwe kwenye vitendo kwa kukusanya fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato katika manispaa hiyo na kisha zitumike kama ilivyokusudiwa.
Ahadi ya meya la kubana kampuni zote zinazokwepa kodi na kusababisha manispaa kukosa Sh. bilioni 10 kila mwezi itekelezwe kwa kutambua na kuzingatia kwamba bila fedha hakuna maendeleo kwani hakuna miradi itakayotekelezwa.
Ninatambua taka ni kero na sasa Manispaa imeanza mkakati wa kuondokana na uchafu huo kwa kuagiza malori ya kuzisomba kati ya 35 hadi 40 na kujenga dampo la kisasa Mabwepande na mashine za kushindilia taka hizo.
Cha msingi ni kwamba bila ukusanyaji wa kutosha wa mapato kwa ajili ya shughuli za maendeleo, madiwani hawawezi kutimiza ahadi walizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kwa maana hiyo, Chadema anzeni kutimiza ahadi zenu sasa na hasa kile ambacho Meya Jacob alichokisema cha kubana makampuni ambayo anadai kuwa yamekuwa yanakwepa kulipa kodi na kuikoseha Manispaa Sh. bilioni 10 kila mwezi.
ends



.jpg?itok=nfwjwDzv)







