Jibu la kitendawili nilichotumia kuandika kichwa cha makala haya ni mwavuli/mwamvuli. Mwavuli ukunjuliwapo huwa na faida au uwezo mkubwa. Humkinga binadamu na asipouhitaji huuweka mahali kama vile si chochote.
Huu ni uthibitisho mwingine kuwa lugha ya Kiswahili ina utajiri mkubwa wa maneno, tashbihi/tashbiha (usemi unaofananisha kitu kimoja na kingine kwa kutumia maneno. Mfano: kama, mithili au sawa.
Pia vitendawili (semi za mafumbo zinazohitaji majibu ya papo kwa papo). Milio (sauti inayotokana na mgongano wa vitu); sauti inayotolewa na mnyama au ndege na mishangao (hali ya watu kuhemewa na kubakia tuli bila ya kufanya kitu chochote).
Hebu sasa tuone maana ya baadhi ya maneno ya Kiswahili yasiyotumika mara kwa mara. Neno ‘dundu’ lina maana tatu: (i) buyu au boga lililokatwa sehemu ya juu likakaushwa na kuwa chombo cha kutilia kirowevu/kiowevu, kitu cha majimaji kinachomiminika.
(ii)Rundo la vitu, furushi la vitu na (iii) tutamavi yaani mdudu mdogo mwenye tabia ya kuviringisha uchafu; hasa kinyesi.
‘Dundiza’ au ‘dunduiza’ ni jipatia chakula kwa uchache kwa kufanya kazi ndogondogo. ‘Dundumio’ ni sehemu ya umio (njia inayopitia chakula kwendea tumboni na hewa kwendea mapafuni) iliyojitokeza n-nje ya koo. Huchezacheza mtu anapomeza kitu; koromeo, kongomeo, koo.
‘Dungu’ ni (i) kilingo kama cha kulindia ndege au wanyama wasiharibu mazao shambani; kilindo, ulingo. (ii) sehemu akaayo rubani ndani ya ndege; maskani ya hakimu mahakamani; (iii) ushindi katika mchezo wa mpira; bao, goli.
‘Dungudungu:’ (i) neno lielezalo kitu chochote cha ajabu: kioja, miujiza, kituko, ibra. (ii) mtu aliyeumbika vibaya; kitu kilichoumbika vibaya; dude, dubwana, nyangarika.
‘Dutu:’ (i) ni kilima kidogo, kichuguu. (ii) kipele cha mwilini au usoni; chunusi, chunjua, kidudusi, kiwe, kibuja. (iii) tokeza, binuka, kubaza na (iv) ni umbo, sura, gimba.
‘Nyondenyonde’ ni ugonjwa usiopona haraka; bila ya kupona. ‘Nyong’onya’ ni kuwa na maumivu ya mwili yatokanayo na uchovu. ‘Nyong’onyea’ ni (i) dhoofika mwili kwa sababu ya kuchoka au kuumwa; legea/regea, taabika na (ii) ni -kosa raha kutokana na kuwa na mawazo mengi.
Ingawa Kiswahili kina utajiri mkubwa wa maneno, wengi hushindwa kuyatumia ipasavyo ili kuwa na mtiririko mzuri wa sentensi kama ilivyo hapa chini:
“Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea mkoani hapa, imemuhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi wa Kata ya Matekwe, Isack Kalimbe (45) baada ya kupatikana na hatia ya kupokea rushwa ya Sh 10,000/-.”
Kati ya hukumu na mhukumiwa ni neno lipi lingetangulia? Ingeandikwa hivi: “Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea imemhukumu Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi Kata ya Matekwe, Isack Kalimbe (45) kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kupokea rushwa ya 10,000/-.
Kwa kuwa alama /- inamaanisha shilingi, hakuna sababu ya kuandika Sh. Kama inavyozoeleka kwa wengi. Kwa hiyo inapoandikwa Sh. 10,000 kisha ukaongeza alama ya /- mbele ya tarakimu ni kusema shilingi 10,000 shilingi!
Mathalan inapoandikwa ‘$’ maana yake ni dola (hela) ya Marekani. Kwa hiyo ni kosa kuandika dola $ 10,000. Ama unaandika dola kisha tarakimu au $ ambayo ni alama inayotambulisha dola ya Marekani na kufuata tarakimu inayoonesha thamani yake.
Kwamba Kiswahili kina utajiri wa maneno, isiwe sababu ya kuyatumia bila utaratibu kama ilivyo katika sentensi ifuatayo:
“Kikwete alisema hayo jana katika baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo huku akiitaka bodi ya kampuni ya Ranchi ya Taifa (Narco), kuwezesha wawekezaji wa ndani kufuga mifugo inayohitajika katika machinjio hayo kwa kunenepesha, ili waweze kupata idadi inayotakiwa kwa kila siku na machinjio hayo bila kukosa.”
Kitaaluma, kuna maneno yaliyotumiwa bila sababu. Matokeo yake Sentensi imekuwa ndefu (maneno 49) na kupoteza maudhui yake kwa msomaji. Ingeandikwa:
“Baada ya kuweka jiwe la msingi la machinjio hayo, Kikwete aliitaka Ranchi ya Taifa iwawezeshe wawekezaji wa ndani kufuga mifugo bora itakayotumiwa na machinjio hayo.” (Maneno 26).
Methali: Watetea ndizi mgomba si wao.
Marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96


.jpg?itok=nfwjwDzv)








