Wahamiaji haramu wadhibitiwe kikamilifu

16Feb 2016
Lulu George
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wahamiaji haramu wadhibitiwe kikamilifu

KWA muda sasa hapa nchini wimbi kubwa la ukamataji wa wahamiaji haramu hususan kutoka nchi za Ethipia na Somalia linakupwa hapa na pale.

Baadhi ya wahamiaji hao kwa mujibu wa madai yao, huitumia nchi hii kama njia ya kupita kuelekea Afrika Kusini.

Watu hawa huwa wamevunja sheria kwa kuingia nchini bila ya kibali halali hivyo hawana budi kukamatwa na sheria kuchukua mkondo wake. Utekelezaji wa jambo hilo hauna mjadala.

Ukamataji wahamiaji haramu ni dhahiri kwamba serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa gharama kubwa za kuwafikia na kuwatunza hadi wanapokamilisha adhabu zao kisha kuwagharamia kuwarudisha kwao.

Wakati hayo yakifanyika, hali ya magereza yetu ni mbaya sana.Yanahifadhi wafungwa kuliko uwezo wake, yaani kuna mlundikano.ambao ni changamoto kubwa kwa serikali. Gharama za kuwalisha na kuwatunza ni kubwa na ikitokea mmoja wao amefariki jukumu la mazishi pia linabebwa na serikali ya Tanzania. Nchi ya asili inatoa kibali tu cha kumzika muhusika.

Ombi langu kwa mamlaka husika kwa jambo hili kuanzia serikali na vyombo vinavyotunga sheria hususan Bunge ni kuangalia upya sheria na uhalisia wa namna hatua zinavyoweza kuchukuliwa katika kukabiliana na wahamiaji hawa ili kupunguza kiasi fulani cha gharama zinazotumika ikilinganishwa na sasa .

Magereza zetu zina changamoto kubwa sana hata bajeti inayotengwa na serikali kwa ajili ya kuzihudumia haitoshelezi, sasa kwa nini tuwahudumie wageni kwa gharama kubwa sana ikiwemo kuwarudisha kwao kwa usafiri wa ndege ikizingatiwa kuwa kila mwezi kwa nchi nzima wanaokamatwa ni idadi kubwa ya wahamiaji haramu.

Yawezekana mamlaka husika hazijasugua vichwa sawa sawa katika kuliangalia na kulichambua jambo hili, kwa kina ikibidi kuna haja ya kuzungumza na serikali za nchi hizo, ili kama watu wao wataingia bila vibali na kuvunja sheria za nchi zetu wahusike katika kuchangia gharama.

Kwa kufanya hivyo, pengine itasaidia kuwabana watu wao huko waliko na balozi zao ndio zihusike na gharama hizo moja kwa moja.

Watanzania sasa wanahitaji kuona maendeleo ya haraka na si kuendelea kubebeshwa mizigo kwa sababu ya makosa ya wengine. Fedha inayotumika kuwatunza maelfu ya wahamiaji haramu wanaoingia nchini, ingeweza kutumika katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii hapa nchini.

Si lazima kuiga mifano ya nchi nyingine kama vile Kenya ambao wao sheria inawaruhusu watu hao kupita bila kikwazo pengine kiundani ina changamoto zake, kwani wahamiaji hawa baadhi ni wahalifu waliokimbia vita huko kwao, wanaweza kutumika katika usafirishaji wa silaha za kivita na hata dawa ya kulevya.

Baadhi yao ni watu hatari ambao hawastahili, lakini hoja yangu ya msingi kutafuta namna madhubuti ya kuwabana na kuhakikisha serikali yao inawajibika kuhakikisha kuwa watu wake wanaishi ndani ya mipaka yao licha ya dhoruba walizonazo. Huu mzigo wa gharama usibaki kuwa wa kwetu peke yetu.

Naamini Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bunge, Vyombo vya sheria na dola kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watafute mawazo ya pamoja katika kukabiliana na hali hii.

Kiuchumi Tanzania bado ni nchi changa sana kubeba mzigo mkubwa kama huu.

Naheshimu sheria za kimataifa kuhusu upokeaji wa wakimbizi,lakini hili la wahamiaji haramu linafaa kutazamwa kwa jicho la uangalifu na umakini wa hali ya juu.Hatuna budi kuonyesha msimamo katika hili kwa watu kutoka nchi nyingine vinginevyo tutaendelea kubeba mzigo utakaokuwa unatulemea siku hadi siku