Alisema kwa sasa wamebaini wanaume wengi wanapitia ukatili kwenye ngazi ya familia na jamii lakini kwa sababu hakukua na mfumo wa kuripoti wamejikuta wanaendelea kuumia bila msaada.
Alisema mifumo hiyo itasaidia wanaume kusema madhila wanayopitia, kwa sababu imeonekana matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanatokana na uvumilivu kufika mwisho na kutaka kuonyesha mamlaka au misuli aliyonayo.
Kwa sasa ukatili wa jinsi umeongezeka kiasi kwamba kila siku kuna tukio la mtu kumuua mpenzi wake, kumjeruhi au kufanya lolote baya na chanzo kikielezwa ni wivu wa mapenzi.
Waathirika wakubwa ni wanawake na watoto kwa sababu anayevumilia huamua kushusha hasira yake kwa wanaomzunguka au waliomfanyia jambo lolote ambalo mbele ya jamii ameona amedhalilishwa.
Mwanaume amelelewa na jamii kama mtu wa kuvumilia,kutoonyesha machozi au maumivu yake mbele ya jamii kwa kuwa kufanya hivyo ni kuonyesha udhaifu wakati mwanaume ni mwenye misuli na nguvu nyingi.
Tupo kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili,ni muhimu kujumuisha jamii yote ili tuwe na kizazi endelevu na kinachoishi kwa amani na utulivu.
Mathalani, kwenye jamii inapotokea msiba mtu kaondokewa na mtu wake wa karibu sana anashindwa au kuzuiwa kulia huku akiambiwa yeye ni mwanaume hapaswi kuonyesha maumivu.
Pia programu nyingi zimeandaliwa kuwawezesha wanawake ambao kimsingi waliachwa nyuma na kunyanyaswa kiuchumi lakini kwa sasa wanawezeshwa kiasi kwamba wengi wanaweza kujisimamia kimaisha.
Wanaume watumie vyema mfumo huo ili tuwe na jamii yenye usawa kwa kuwa nao ni binadamu kama wengine wana haki zote za msingi.
Kwenye jamii yetu tunaona matukio mengi ya udhalilishaji wa watoto wa kiume ambayo lazima yachukuliwe hatua mapema,programu za uwezeshaji wanaume na wanawake ziwe endelevu na saidizi.
Hivi karibuni, mwanaume mmoja alihojiwa na chombo kimoja cha habari akieleza kwa uwazi madhila anayoyapitia kwa kuteswa na mkewe, alisema anapigwa sana na mara kadhaa wameenda kanisani wakaambiwa ndoa ni hadi kifo kiwatenganishe,kasoro zinazojitokeza washirikiane kuzitatua.
Hii inaonyesha kuna tatizo kubwa kwenye jamii ambalo lazima liangaliwe,kwamba tunavyowekeza nguvu kumwezesha mwanamke na mwanaume naye asiachwe nyuma.
Ni muhimu mpango kazi wa taifa kwenye eneo la uwezeshaji likajumuisha wanawake na wanaume, itasaidia kuwa na kizazi chenye usawa wa kijinsia.
Ni vyema kukawa na majukwaa ya wanaume kujadili ukatili wa kijinsia kwenye ngazi ya familia na mitaa,kwa kuwa jamii inayozungumza ndio yenye uhai.
Kuelewa madhila anayokutana nayo mtu sio udhaifu na hakutaondoa uanaume wake,bali ni namna pekee ya kuuponya moyo na akili yake.
Wanaume kwenye mtaa fulani wanaweza kuamua kuwa na vikao vya kila mwezi kuzungumza hali ya usawa wa kijinsia, lakini pia kufundisha vijana namna ya kuwa wanaume wawajibikaji na wajenzi wa familia.
Kwa kuzungumza kutasaidia watu kueleza hisia zao na kupunguza maumivu waliyonayo kwa kuwa inaaminika kwa kuzungumza mtu anatoa dukuduku na pia ni tiba nzuri kwa moyo unaoumia ndio maana nchi nyingine duniani kuna mahali pa kwenda kufunguka yote ya moyoni alafu unarudi nyumbani ukiwa umetua mzigo.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







