Simba, Yanga wasinyimwe uhuru kutoa mawazo

26Nov 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga wasinyimwe uhuru kutoa mawazo

TUNAJUA kwa sasa wanachama wa klabu za Simba na Yanga hawana tena mamlaka ya kuamua mustakabali wa klabu zao kama ilivyokuwa zamani.

Tunakumbuka wakati ule wanachama wakiona mambo hayaendi vizuri, wanaitisha mkutano na kuamua kile ambacho wataona ni muhimu kwa manufaa ya klabu zao kwa wakati huo.

Ndiyo wakati tuliona mapinduzi makubwa ya viongozi. Timu ikifungwa, kesho yake tu wanachama wanaitisha mkutano, kama hawawataki viongozi wanapitisha maazimio ya kuondoa uongozi.

Baadaye nakumbuka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) liliingilia kati na kutengeneza katiba kuzipeleka kwa wanachama wake kuweka utaratibu wa kuwaondoa viongozi na si kiholela kama ilivyokuwa ikifanyika.

Tukaanza kuona sasa angalau viongozi wa klabu hizi wakikaa mpaka vipindi vyao vinamalizika, ingawa bado walikuwa wakiongoza kwa matatizo makubwa. Nia yangu si kuunga mkono yale ambayo yalikuwa yakifanywa na wanachama wa kipindi hicho la hasha kwa sababu kuna wakati pia baadhi yao walikuwa wakihongwa na baadhi ya watu walio nje ya madaraka kufanya vurugu ili kuuondoa uongozi na wao waingie.

Ni kutaka kuonyesha jinsi wanachama walivyokuwa na nguvu ya moja kwa moja ya kuwawajibisha viongozi wao, walikuwa na nguvu kuliko viongozi waliowaweka madarakani. Kwa sasa haipo hivyo. Mpira umebadilika. Mpira kwa sasa ni biashara ambapo inahitaji wawekezaji. Hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwekeza halafu bado eti wanachama wakaendelea kuwa na nguvu ya kufanya maamuzi. Dunia nzima kwa sasa mwekezaji ambaye anatengeneza watu wake anawaamini kwenye bodi kwa kushirikiana na wale wa upande wa  wanachama, au mfumo wowote ule wa uendeshaji wa soka la kisasa, watu wachache ndiyo wenye maamuzi.

Bodi ndiyo inawawakilisha wanachama wote, na ndiyo wanaoiendesha klabu. Aina hii ya uongozi wa soka la kisasa la wawekezaji limewanyang'anya wanachama maamuzi juu ya klabu zao. Binafsi wala sipingi kwa sababu kwa sasa lipo huko. Mwenye pesa ndiye anayeamua nini kifanyike.

Mimi nina wasiwasi pia inaonekana pia wanachama wanataka kupokwa hata haki yao waliyobaki nayo ya kutoa maoni yawe hasi au chanya juu ya klabu zao pendwa.

Nimemsikia kiongozi mmoja wa tawi  moja la Yanga akiwapiga mkwara wanachama wanaopenda kuongea na Waandishi wa Habari mara baada ya mechi zao. Akaenda mbali zaidi  kwa kutangaza kuwa watamsimamisha mwanachama wao mmoja kwa kosa hilo. Kisa eti alitoa maoni yake, na wengine wanawasema viongozi wao.

Akawapiga marufuku wanachama kuongea na waandishi. Hili halikubaliki hata kidogo. Wanachama wamenyang'anywa maamuzi kwenye klabu yao, sasa inataka kwenda mbali zaidi kutaka kuwapoka hata ile haki waliyobakia nayo ya kutoa maoni yao. Huu sasa hauwezi kuuzungumzia vingine zaidi ya udikteta. Iwe kwa Yanga au Simba viongozi waachane kabisa na jambo hili.

Tumeona hivi karibuni Simba haifanyi vema kwenye michezo ya ligi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa wakiwaonyeshea vidole vya shahada viongozi wao na wachezaji pia. Iwapo atatokea kiongozi yoyote wa Simba wa juu au matawi akawakataza wasiongee, litaendelea kuwa tatizo kubwa kwenye soka la Tanzania.

Hakuna kiongozi anayeweza kujitathmini, kuona anafanya vema au anakosea kama hataki watu waongee.

Halafu asili ya mchezo wa soka ni kuongea. Iwe kuongea kwa kufurahi, kulalamika, au kutoa maoni hata kama ataongea vibaya au jambo ambalo halipendezi. Hii ni haki ya kwanza ya binadanu anayopewa na Mwenyezi Mungu, haki ya kujieleza na hata kwenye Katiba ya Tanzania imebainishwa bayana kuwa wananchi wanayo haki hiyo. Kuwakatalia wanachama na mashabiki  kuongea ni kuwanyima uhuru wao, haki ya msingi na asili,  lakini pia itawahatarishia usalama wao.

Ni kwa sababu wapo wataokuwa na kazi ya kuhakikisha hakuna shabiki au mwanachama yoyote anaongea na vyombo vya habari, akionekana wanaweza kupata wakati mgumu sana kwa wenzake ambao wanaweza kumfanya chochote kile ambacho kinaweza kumhatarishia usalama.

Kiongozi jasiri na mwenye karama ya uongozi ni yule ambaye anawaacha huru anaowaongoza waseme. Wakati mwingine kuongea kwao kuna kitu ambacho anaweza kukiokota na kukifanyia kazi. Hata ukiwa na marafiki ambao kazi yao ni kukusifia tu ujue umepotea. Unatakiwa uwe na marafiki ambao watakwambia hapa umefanya vema, hapa hapana na kukupa ushauri.

Viongozi wakianza tena mambo ya kuwakataza wanachama na mashabiki kuongea hautokuwa mpira wa miguu tena.

Ladha ya soka ni kuongea timu inaposhinda, kutamba, kuchambua, kutoa ushauri, kuonyesha na kuelekeza uchungu timu inapopoteza, kuonya, kushauri benchi la ufundi, viongozi na wachezaji. Vinginevyo sasa utakuwa si mpira tena zaidi ya mambo ya jandoni ambayo ukitoka unakuwa nayo tu moyoni, hautakiwa kuyazungumza hadharani.