Wanafunzi kuhitimu bila kujua kusoma, kuandika kutufikirishe

29Nov 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanafunzi kuhitimu bila kujua kusoma, kuandika kutufikirishe

ELIMU ni mchakato wa kupata maarifa, ustadi, maadili, imani na tabia, inayopatikana baada ya wanafunzi kupelekwa shuleni ili kuvipata vitu hivyo muhimu kwa ajili ya kuwasaidia kumudu maisha yao ya sasa, ya baadaye na kuchangia maendeleo ya taifa.

Umuhimu wa elimu ulitiliwa mkazi tangu wakati wa nchi kupata uhuru, pale ilipotangazwa vita kwa maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini, ambapo elimu iliwekewa mkazi kufanikisha vita hiyo. 

Ili kuendelea kujiongezea maarifa katika elimu, baadhi ya wanafunzi huwa wanakwenda kusoma masomo ya ziada (twisheni), ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wanafanikiwa katika malengo yao ya kujielimisha. 

Wanafanya hivyo kutokana na umuhimu wa 'twisheni' ambao una utaratibu wake wa kurudia masomo ambapo wanapata fursa ya kuelewa vizuri zaidi masomo baada ya kuyarudia kwa mara ya pili. 

Hata hivyo, wakati juhudi za kupambana na adui ujinga zikiendelea, bado yapo maeneo nchini ambayo wanafunzi wanahitimu elimu ya msingi bila kujua kusoma na kuandika, kitendo ambacho ni kama kinakwamisha juhudi hizo. 

Kwa mfano, Mkoa wa Mara unatajwa kushika nafasi ya tano kitaifa kwa kuwa na wanafunzi wanaohitimu darasa la saba, bila kujua kusoma na kuandika. Ninadhani ni vyema chanzo cha hali hii kikatafutwa. 

Ikumbukwe kuwa serikali imeanzisha utaratibu wa kuwa na darasa la awali katika shule zake zote, ili mtoto aanzie huko na anapoanza darasa la kwanza awe tayari anajua kusoma na kuandika. 

Ofisa Elimu wa mkoa huo, Benjamin Oganga, anabainisha hali hiyo mbele ya viongozi wa elimu wa kada na ngazi tofauti, wa wilaya na mkoa muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi. 

Kwamba mkakati huo uliozinduliwa kimkoa na Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Suleiman Mzee, utakuwa mwarobaini wa changamoto hiyo na nyingine, zikiwamo zinazotokana na mafanikio katika sekta ya elimu. 

Ofisa elimu huyo katika ufafanuzi wake, anasema ufuatiliaji uliofanywa unaonyesha ndani ya miaka mitano, wanafunzi 350,000 katika mkoa huo hawakuhitimu elimu ya msingi. 

Lakini viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya shule mpaka mkoa wanatakiwa kushirikiana na mamlaka nyingine, kutafuta kila mwanafunzi aliyetakiwa kuwa shuleni, lakini hayupo, ikiwezekana wazazi wa wanafunzi hao wabanwe. 

Kwa mikakati hiyo na mingine mingi ninadhani kama mkoa umedhamiria kumaliza tatizo, inawezekana ukafanikiwa na kuondoa aibu hiyo ambayo haitakiwi kuwapo katika karne hii ya 21. 

Jambo lingine la muhimu ni ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wazazi na walezi na pia wangetambua juhudi zinazofanywa na serikali za kutoa elimu bure kuwa zinalenga kuhakikisha kila mtoto anapata elimu. 

Lakini bahati mbaya wapo baadhi na walezi hata wakiona watoto wao hawaendi shule hawawaulizi na pia hawafuatilii shuleni au hata kukagua madaftari yao, ili kujua kinachoendelea. 

Kwa mazingira kama hayo ni wazi mbumbumbu wataendeelea kuwapo iwapo kila mmoja hatatimiza wajibu wa kuhakikisha mtoto wake anakwenda shule na anapata elimu ambayo inatolewa bure. 

Sidhani kama bado kuna visingizio tena kuhusu masuala ya ada, kwani kinachotakiwa ni mzazi au kununua sare, madaftari na vifaa vingine vya shule ambavyo kimsingi ni vya muhimu katika elimu. 

Ushirikiano wa karibu ni wa muhimu kwa wadau wote wa elimu kwa jili ya kumaliza tatizo hilo, wazazi na walezi ni wadau mojawapo, hivyo sidhani kama itapendeza wakijiweka pembeni.

Lakini pia wanafunzi nao wasichukulie shule kama sehemu yao ya kukutana na kucheza tu, bali watambue kuwa hiyo ni sehemu ya kupata elimu ili kuondokana na adui ujinga ambaye anaweza kukwamisha ndoto zao na hata kuwatumbukiza kwenye shimo la kuangamia.