Hiyo ni taarifa ilitolewa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, wakati akizindua mbio za Mwenge mwaka huu wa 2022 mjini Njombe.
Kutokana na hali hiyo, akawaagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuharakisha uchunguzi, ili watuhumiwa wa kuchakachua kazi za ujenzi na miradi mingine wafikishwe mahakamani haraka na haki itendeke.
Kuchakachua miradi ya maendeleo, ufisadi na hata wahusika kutofanya kazi za kandarasi wanazopewa imekuwa ikiibuliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru kila mwaka, hali ambayo inaonyesha kuwa huenda wananchi hawajui wajibu wao na haki ya kufuatilia utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
Ikumbukwe kuwa, serikali imekuwa ikitafuta fedha hata za mikopo nje na ndani ya nchi na nyingine pesa zinazotolewa na walipa kodi ili kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake, hivyo hujuma zinazoibuliwa na Makamu wa Rais, zinaongeza uchungu.
Hivyo, wananchi kwa upande wao ni vyema sasa wakaamka na kujua kuwa ni nguzo muhimu ya kufuatilia na kuhakikisha miradi hiyo inalingana na thamani ya fedha iliyotumika badala ya kujiweka pembeni na kuacha wajanja wachache wajinufaisha kwa jasho la Watanzania wengi wakiwamo maskini wanaovuja jasho.
Ingependeza kuona kuwa wananchi wanashirikishwa na wanafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ili kodi ambayo wanaitoa iwe na matokeo chanya.
Watanzania iwe kijijini au mjini kwenye mradi wa umeme, maji, hospitali, shule au barabara kukaa kimya hadi uchakachuaji uibuliwe na Mwenge wa Uhuru, ni sawa na kuruhusu hujuma hizo ziendelee kuwapo bila kudhibitiwa.
Hujuma hizo zinaweza kusababisha serikali isifikie ilichokusudia kukifanya kwa ajili ya maendeleo hayo ya nchi na watu wake.
Uchakachuaji wa miradi ya maendeleo unaoongeza gharama zisizotarajiwa kwa kurudia upya ujenzi wa wake lakini pia kutumia fedha mara dufu.
Ninadhani kwamba, Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zisaidie kuwakumbusha wananchi kufuatilia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kuondolea dhana kwamba ufuatiliaji huo ni jukumu la serikali.
Pia ninaamini kuwa serikali inapotoa fedha kwa ajili ya maendeleo inatarajia kuona zinatumika ilivyokusudia, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi kulingana na thamani ya fedha iliyotumika.
Jambo hilo linahitaji usimamizi na ufuatiliaji wa pamoja kuanzia kwa wananchi na serikali, ili kuziba mianya yote ya uchakachuaji ambayo imekuwa ikitumiwa na baadhi ya wasimamizi.
Kimsingi, wasimamizi hawapaswi kutumia nafasi za kujinufaisha kwa kodi za Watanzania na kutekeleza miradi chini ya kiwango, jambo ambalo ni hatari, lakini ni kukosa hofu ya Mungu na hata kusababisha hatari na kutishia maisha.
Kwa mfano, daraja linaweza kujengwa chini ya kiwango na baadaye likabomoka na likasababisha maafa kwa watumiaji.
Hivyo, ni vyema wananchi wawe mstari wa mbele kufuatilia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao, kwa ajili ya maendeleo, lakini na usalama wao.
Utaratibu huo unaweza kusaidia kuziba mianya ya hujuma inayotumika kutekeleza miradi ya maendeleo chini ya kiwango na kuisababishia serikali hasara na kuongeza umaskini kwa taifa.
Viongozi wa CCM, serikali, vyama vya upinzani na asasi za kiraia washiriki kufuatilia na kupigia kelele kazi hafifu kwenye maeneo yao na kuiarifu TAKUKURU badala ya kusubiri Mwenge.
Heri kukinga ufisadi kuliko kuuacha ufanikiwe.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







