Matokeo yake wanajikuta wakitumbukia katika maamuzi magumu na ya kikatili kama mauaji ya wenzao wao au wenyewe kujitia kitanzi.
Huenda wengi wamekuwa wakidhani ni udhaifu kusema matatizo yao binafsi na yale yanayowahusisha wenza wao na hapo ndipo kesi za mauaji zinapoleta simanzi kwenye mioyo yao na Watanzania wengine.
Matokeo yake hawatafuti ushauri na nasaha na kama wanavyosema mwanzo wa ngoma ni lee, mauaji haya yalianza kama kipele ila sasa ni jipu linalohitajika kutumbuliwa kwa upasuaji mkubwa.
Katika siku za hivi karibuni, ripoti na taarifa kuhusu kuenea kwa vitendo vya mauaji yanayohusishwa na wivu wa kimapenzi vimezua taharuki, mjadala pia hofu.
Siku za nyuma hayakusikika sana matukio hayo, ila kwa sasa yameonekana kushamiri. Swali la kujiuliza ni hili ni kwanini mauaji haya? Je, nini kinachoendelea kwenye jamii?
Kumekuwa na matukio ya kujiua, wanawake na wanaume wakijinyonga, lakini wanaume kuua wake na wapenzi wao, lakini kinamama kuua waume zao, kisa hisia za kuwapo harufu ya usaliti kwenye uhusiano au ndoa inaponukia.
Hili huenda linatokana na wanaume kushindwa kuongea matatizo yao kwa wanasihi au watu wa karibu ama wataalamu wa saikolojia kwa kuogopa aibu.
Ni kwa sababu wanaume ndiyo wanadaiwa zaidi kuhusika na mauaji hayo.
Kumekuwa na mifano kadhaa wa kadhaa, ya vitendo hivi mfano jijini Mwanza hivi karibuni mke na mume walikufa kwa risasi.
Tukio hili ni kama limeibua upya mjadala wa masuala ya mauaji kutokana na madai ya kuwapo wivu wa mapenzi.
Tukio lingine ni la Februari 24, mwaka huu, huko Mwanga, Kilimanjaro lilihusisha wanaume wawili waliokuwa na uhusiano na mwanamke mmoja, kuamua kula njama na kumuua kwa sababu ya wivu na aibu ya kuwachanganya kimapenzi.
Kabla ya kumuua kwa kumkatakata kwa mapanga kuna madai kuwa walimbaka na kumdhalilisha. Lakini pia tukio lingine ni la Desemba 27, 2021 mwalimu wa sekondari mkoani Singida, alidaiwa kuuawa kwa kuchomwa moto na mkewe baada ya kumtuhumu kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine.
Oktoba mwaka jana katika kitongoji cha Kanyabugulu mkoani Kagera, mwanaume alidaiwa kumuua mkewe kwa kumkata mapanga nyumbani kwake akishuhudiwa na mtoto wake wa miaka 14, kwa kile alichodai mwanamke huyo alikuwa na uhusiano na mwanaume mwingine.
Ukitazama kwa undani vitendo hivi vya mauaji ni suala la kisaikolojia zaidi, maana mtu anakuwa na imani kwamba akimuua mwenzake atafaidika. Kuua hakufanyiki kwa ghafla ni mtiririko wa matukio yanayoenda kupanga hadi kuamua mauaji.
Hivyo basi ili kuepukana na haya yote ni vyema kama wapenzi wakikaa na kutengeneza namna yao ya kuishi, wakubaliane walivyo na madhaifu yao na kukubaliana yale ambayo wanatofautiana.
Mpe uhuru mwenzio aishi maisha ayapendayo lakini heshimuni na kulinda mambo mliyokubaliana ili kuepuka mafarakano.
Na pia serikali iweke adhabu kali zaidi kwa watu watakaojihusisha na vitendo hivi maana isipoziba ufa itajenga ukuta.
Sio hivyo tu lakini ni vyema kuondokana na dhana inayowafanya wanaume wajione wadhaifu mbele ya jamii iwapo watasema matatizo wanayopitia hasa katika mapenzi wataweza kupata msaada wa afya ya kiakili na kuzuia maafa mengine.
Kutoa dukuduku au kufunguka kuhusu matatizo inasaidia kuachia mzigo uliobeba moyoni na huleta afya na faraja ya akili, moyo na mwili.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








