Wanaona kama hadithi inaweza kuwa ni ile ile ya kushindwa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON kwa mara nyingine tena.
Kinachowanyong'onyeza ni kuona ni kama hadithi inajirudia tena. Ya kutoka sare ugenini na kufungwa nyumbani.
Wanakumbuka wakati ule Stars ilipokuwa ikisaka tiketi ya kwenda kucheza fainali za Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini Qatar.
Ni kwamba ilikuwa inatoka sare na kushinda ugenini, huku ikipoteza nyumbani. Ilitoka sare ugenini dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kuifunga Benin nyumbani kwao, lakini tatizo ilikuwa haifanyi vizuri nyumbani, ndiyo maana ilifungwa na timu hizo mbili hapa nchini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Naona mashabiki wengi wameanza kukumbuka hilo baada ya mechi ya kwanza kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Niger, kabla ya kuchapwa dhidi ya Algeria.
Kwa sasa Tanzania ipo chini ya Algeria na Niger, ikiwa na pointi moja, sawa na Uganda kwenye Kundi F. Ni timu mbili tu zinatakiwa kufuzu kwenda kwenye fainali hizo zitakazochezwa mwakani nchini Ivory Coast.
Pamoja na yote haya, Stars bado haijapoteza na inaweza kufanya vema kwenye mechi zilizosalia ikakaa nafasi ya kwanza au ya pili.
Kikubwa ni maandalizi, pamoja na wachezaji kulinda viwango vyao. Ukisikiliza mashabiki wanavyolaumu, wanaongeza vitu vya juu juu tu ambavyo ni matokeo ya vitu vya msingi. Wengine wanalaumu kocha hasa kwenye upangaji, wengine wanalaumu baadhi tu ya wachezaji.
Ukweli tu ni kwamba ule ndiyo uwezo halisi wa wachezaji wa Tanzania ulipofikia. Na ukiangalia bado hawakucheza vibaya sana, ila kwenye mechi dhidi ya Algeria walikutana na timu yenye wachezaji wakubwa, wanaocheza timu kubwa barani Ulaya, ambao walicheza kikubwa.
Wakati Stars ikikosa mabao, wenyewe walizitumia nafasi chache tu walizozipata kupata mabao. Kuna walidai kuwa yote inatokana na nchi yetu kuwa na wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu, hivyo linapokuja suala la timu ya taifa tunajikuta hatuna wachezaji bora. Wale ambao tunawaona na kuwaimba kuwa ni bora kwenye ligi yetu ndiyo tunashtuka kuwa si Watanzania.
Hapa ndipo kuna mshangao kidogo, kwani wachezaji karibuni wote wa Algeria hawakutoka kwenye ligi ya nchi hiyo. Wengi wanacheza klabu kubwa barani Ulaya.
Ina maana siyo lazima uwe na wachezaji wa timu ya taifa wanaotoka kwenye ligi ya nyumbani. Unaweza wote ukawatoa nje ya nchi. Ndiyo timu za taifa za wenzetu wamefikia huko. Nilitegemea mashabiki wangewashauri wachezaji wa Kitanzania nao sasa wengi wao watoke nje ya nchi ili ikiitwa Stars, basi wachezaji wa ndani wawe wawili watatu wakujazia tu kama wanavyofanya wenzetu.
Pamoja na yote haya, mechi zijazo zitachezwa Septemba. Stars itakuwa ugenini Septemba 19 dhidi ya Uganda. Huu ni muda mrefu wa kujipanga kuanzia wachezaji wenyewe na Shirikisho la Soka nchini (TFF), kama kweli tuna nia ya kufuzu.
Kwa upande wa wachezaji wanatakiwa kujitunza na kujituma kwenye klabu zao. Itashangaza kuona mwezi huo unafika, nusu nzima au robo tatu ya wachezaji hawapo kwa sababu hawakuitwa kutokana na viwango vyao kushuka. Hili ndilo tatizo kubwa la wachezaji wetu. Stars inachaguliwa kwa viwango vya wakati huo na si vinginevyo.
Kwa upande wa TFF ni wakati wa kuangalia kuiwahisha Ligi Kuu msimu ujao ili ikifika Septemba 19 angalau wachezaji wawe kwenye fomu.
Ligi msimu huu imechelewa kumalizika, huku fainali ya Kombe la FA ikichezwa Julai 2, sasa kama mwezi Agosti utapita hivi hivi na ligi ikaanza mwanzoni au katikati ya Septemba, itakuwa ngumu sana kushinda mechi zinazofuata na kufuzu.
Wachezaji watakuwa bado hawako fiti, kwani wengi watakuwa wanajitafuta kwa sababu ya kutoka kwenye mapumziko marefu. Hata kocha jinsi ya kuchagua itakuwa shida.
Nashauri tu angalau ligi ianze katikati ya mwezi Agosti, ili mpaka mechi ya Uganda inafika, tayari wachezaji wameshaanza kuchanganya, na hata unaweza kuwapata wachezaji wapya ambao wameonyesha viwango bora.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








