Nikisimamia taarifa kwa umma ya mwenendo wa ugonjwa huo nchini, iliyotolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, katika kipindi kama cha mwezi mmoja kuanzia Mei 5 hadi Juni 3 mwaka huu.
Waziri Ummy anasema katika kipindi hicho jumla ya visa vipya 161, vilithibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO-19, ikilinganishwa na visa 68 vya kipindi cha Aprili 2 hadi Mei 4, mwaka huu.
Anasema, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 137, na kwamba, katika kipindi cha miezi miwili mfululizo, hakuna kifo kilichoripotiwa na kufafanua kuwa, hali hiyo inaaminisha kuongezeka kwa maambukizi katika jamii.
Nadhani kwamba sentesi hiyo ya waziri isitutishe, kila Mtanzania akijiweka sawa kuchukua hatua sahihi zitakazomwezesha kujikinga na ugonjwa huo.
Hapo kuna kipengele cha kukumbushana kuwa makini na umuhimu wa kwenda mahali husika kupata huduma za chanjo, hata mtu awe katika usalama zaidi.
Mara zote katika utoaji chanjo na kumpatia mtu huduma inayomwezesha huwa salama, mwongozo sahihi unaelekeza uvaaji barakoa kwa usahihi wakati wote unapokuwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko au pindi unapojisikia dalili za mafua, ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi.
Aidha, unaelekeza pia kuuzingatia usafi binafsi, ikiwamo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, mara kwa mara na kuwahi katika vituo vya afya endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kuna mkazo unamuwia mtu kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara, kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora, kutoa taarifa za kuwapo watu wenye dalili za ugonjwa huo katika jamii kupitia namba ya simu ya bure 199.
Pamoja na kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya, ni vyema pia kukaongezwa kasi ya utoaji elimu na uhamasishaji jamii kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo, ili kuendelea kuwa mahali salama zaidi. .
Elimu na uhamasishaji vinahitajika, kwa sababu suala la chanjo liliingiliwa na wataalamu wa mitaani ambao nao wamekuwa wakielimisha jamii kinyume na kile kinachofanywa na wataalamu wa afya.
Mchanganuo wa waliothibitika katika kipindi cha Mei 5 hadi Juni 3, mwaka huu, unaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam uliripoti matukio 130; Arusha 10; Mwanza watano; Shinyanga wanne; Mtwara watatu; na Dodoma na Morogoro ni wawili kila moja.
Pia mikoa ya Morogoro, Simiyu, Katavi, Kilimanjaro, na Mbeya ikawa na mikasa mmoja kila mkoa, huku wagonjwa watatu waliothibitika kuwa na UVIKO-19 waliolazwa, wote walikuwa hawajapata chanjo.
Takwimu zinaonyesha kwamba, chanjo ni kinga dhidi ya madhara ya UVIKO-19, basi ni vyema kila Mtanzania awe tayari kuchukua hatua sahihi zitakazomwezesha kuwa salama zaidi.
Serikali inaendelea kutoa huduma za chanjo ya UVIKO-19 nchini, kwa lengo la kuwezesha wananchi kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo, kuanzia Mei hadi mwanzo wa Juni, watu 775,680 walipata dozi kamili.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







