Wakumbusheni ‘imeandikwa usiue’ mauaji yanapotikisa taifa

15Feb 2022
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakumbusheni ‘imeandikwa usiue’ mauaji yanapotikisa taifa

TANGU kuanza mwaka huu, takribani matukio 30 ya mauaji yameripotiwa hadi jana, kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Februari leo imetimizi siku 15, lakini hadi jana, ni takribani matukio 10 yameshatokea na kuripotiwa kwenye vyombo vya habari likiwamo gazeti hili, kwa kuvinukuu vituo vya polisi.

Januari, mwaka huu, pekee, idadi ya matukio hayo yalitokea ni 20, kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari hivi karibuni.

Kituo hicho kinasema kilibaini matukio hayo kutokea hasa mikoa ya Mtwara, Rukwa, Njombe, Katavi, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Dar es Salaam na Mara.

Ongezeko la mauji nchini kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu, wanasheria na wadau tofauti yanahusishwa na sababu kadhaa zikiwamo mila potofu, imani za kishirikina pamoja na jamii kujichukulia hatua na sheria mikononi badala ya kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya haki na sheria.

Kwenye jamii kunakotokea matukio haya ni wakati wa viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini na serikali kuchukua hatua.

Hivi sasa wanahitajika zaidi viongozi kutoa elimu kulingana na imani tofauti za wananchi kwa kuwa kila dini katika maandiko inakataza mauaji.

Viongozi hususan wa kidini ambako kila mmoja kulingana na ratiba yake hufanya ibada wanatakiwa kuanzia sasa kutumia majukwaa yao kukemea vitendo hivi ambavyo vimegeuka kuwa ni mazoea kusikia au kusoma gazetini kuua bila kuwa na hofu ya Mungu.

LHRC, inakariri taarifa kuwa mkoani Mtwara, Januari mwaka huu kuliripotiwa tukio la polisi saba ambao walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Mussa Hamisi (25), mkazi wa Kijiji cha Ruponda Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Mark Njera, alithibitisha mauaji hayo yaliyofanyika Januari 5, mwaka huu.

Kadhalika, kituo hicho kinasema tukio lingine lilitokea mkoani Mwanza, liliripotiwa wanawake watatu kuuawa na miili yao kutupwa katika eneo la Mecco Kusini, wilayani Ilemela jijini Mwanza Januari 20, mwaka huu.

Pia mkoani Rukwa kuliripotiwa mauaji ya mama na watoto wake wawili wenye umri wa miaka mitatu na sita ambao waliuawa katika mazingira ya kutatanisha na watu wasiojulikana, huku miili yao ikikutwa imekatwakatwa sehemu mbalimbali, tukio lililotokea Januari 24, mwaka huu Kijiji cha Azimio-Katumba wilayani Sumbawanga.

Kituo hicho kinaendelea kutaja mikoa mingine, ikiwamo Dodoma, ambako Januari 23, mwaka huu, kuliripotiwa tukio la watu watano wa familia moja kuuawa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Zanka wilayani Bahi.

Pia mkoani Ruvuma, wilayani Songea mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Peace Lodge, Gema Haule (23), aliuawa kikatili na mteja katika nyumba hiyo ya kulala wageni ikidaiwa mteja huyo alikuwa anadaiwa Shilingi 50,000.

Yapo matukio mengi ambayo yanatokea ambayo mengine chanzo chake ni ukatili ambao umo kwenye jamii. Wadau tofauti ni wakati wa kuendelea kupaza sauti na kuelimisha umma kuachana na matukio hayo kwa kuwa haki ya kuishi ni namba moja na iliyo kuu, ikitambuliwa hata kimataifa.

Haki ya kuishi ni ibara ya tatu katika tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, inayosema: Kila mtu ana haki ya kuishi, haki hiyo inalindwa na sheria na hakuna anayepaswa kunyimwa haki hiyo.