Waamuzi wasipewe presha nje ya uwanja

12Feb 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi wasipewe presha nje ya uwanja

KATIKA nchi za wenzetu kwa sasa mtu yeyote awe kocha, mchezaji au kiongozi atakayemsema mwamuzi vibaya basi atapigwa faini na kufungiwa mechi kadhaa.

Kwa sababu wanajua ukiruhusu watu kuanza kusakama waamuzi, basi kila mtu akikosa matokeo kimbilio linaweza kuelekea kwa waamuzi.

Bahati nzuri kwa sasa baadhi ya wenzetu wameendelea kwa kuwa na VAR, ambayo ni mashine ya msaada kwa waamuzi. Hii imekuwa kama mwarobaini wa waamuzi wengi nchi nyingi barani Ulaya na sehemu nyingine za dunia.

Afrika bado ni sehemu chache sana ambazo zina VAR. Sehemu kubwa ya soka la Afrika bado linachezeshwa kizamani.

Hivi majuzi, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli na Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara, waliitisha mkutano na Waandishi wa Habari, pamoja na mambo mengine walieleza kutoridhishwa na baadhi ya uamuzi wa waamuzi katika mechi zinazoihusisha timu yao.

Wakati wakidai wanachezeshwa vibaya, wakaenda mbali zaidi na kudai waamuzi hao wamekuwa wakiichezesha Simba kwa namna ya kuibeba.

Yaani Simba imekuwa ikinufaika na uamuzi mbovu wa waamuzi. Wakadai hawalalamiki, ila wanawakumbusha.

Kali kuliko zote, kesho yake wazee wa Yanga nao wakaibuka, nao wakaongea maneno yanayofanana na hayo hayo ya Manara na Bumbuli.

Ila wao wakaenda mbali zaidi na kudai kuna mkubwa mmoja serikalini amekuwa akilazimisha Shirikisho la Soka Nchini (TFF), kuwaambia waamuzi waibebe Simba.

Mkutano na maneno hayo ya wazee yanawafanya TFF nao kuibuka na kusema haichezeshi ligi kwa maelekezo ya mtu yoyote yule, bali inaendeshwa na Bodi ya Ligi chini ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.

Watuhumiwa wa kupendelewa, Simba nao wakaibuka na kuwataka watani zao wa jadi kucheza soka na si kutoa lawama kwao kwani wao hawahusiki na kupanga waamuzi.

Ilikuwa ni wiki ya mambo mengi sana, kwani Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, aliahidi kumtafutia fedha, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, kwenye bajeti ijayo kwa ajili ya kuweka mashine za VAR ili zitumike kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Na hiyo ni baada ya Yanga kutoa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City, akidai kama kungekuwa na VAR, basi Yanga ingeondoka na ushindi wa bao 1-0, kwani Fiston Mayele alikuwa kwenye nafasi ya kufunga bao na hakuwa ameotea kama mwamuzi namba moja alivyotafsiri.

Hata hivyo haya ni baadhi ya makosa mengi ambayo waamuzi wengi wanayafanya. Ni kwa sababu kuna timu hazina nguvu ya mashabiki wengi wafuasi ambao wana nyadhifa serikali.

Ukiangalia Ligi Kuu ya msimu huu sidhani kama kuna timu ambayo haijanufaika, au kuathirika na uamuzi mbaya, au makosa ya waamuzi.

Siwezi kuyaainisha hapa kwa sababu ni mengi sana. Nampongeza Nchemba kwa kutaka kuleta VAR. Lakini swali linakuja, kwa nini amesema hayo wakati tukio limeihusu Yanga?

Halikuwa tukio la kwanza, lakini ameonekana kuja na mpango mkakati huo baada ya Yanga kunyimwa nafasi ya bao.
Hata hivyo bado nimpongeze kwa hilo, lakini pia hata viwanja navyo virekebishwe ndivyo VAR ije kama alivyosema mwenyewe.

Ila nimkumbushe tu, klabu za Simba na Yanga ndizo zinazoongoza kwa kubebwa na makosa ya kibinadamu ya waamuzi.
Nadhani hata kimoyomoyo baadhi ya viongozi wa timu hizo watakuwa hawaitaki kabisa.

Najua kuwa VAR ikija, zitakazoathirika zaidi ni klabu hizo na zitaanza kutafuta sababu nyingine ili ziondolewe au kutiwa kasoro kwa sababu tu kila kitu kitakuwa kiko sawa.

Tukirudi kwa waamuzi, nadhani wasipewe presha sana. Kinachoonekana sasa ni kuna makusudi fulani ya kuwafanya wasitoe penalti kwa timu ambayo inapaswa kupata, na watoe pale ambapo haipaswi, ili mradi tu wasilaumiwe.

Na hata zinapotakiwa kuongezwa dakika nyingi kwa upotevu wa dakika zisiongozwe, huu sasa utakuwa si mpira.

Viongozi wasiwatie presha waamuzi wetu, badala yake wawaache wachezeshe hadi hapo VAR zitakapokuja.

Kama hata hao wa nje, wanafanya makosa na kusaidiwa na VAR, iweje leo hawa wa bongo wanaofanya makosa na hakuna VAR walaumiwe na kulalamikiwa kama wameua mtoto wa jirani?

Kabla Nchemba kushauri na kusaidia kuja kwa VAR nchini, niliwahi kushauri TFF kuleta waamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha baadhi ya mechi, lakini halikufanyiwa kazi.

Nadhani imefika wakati wa VAR na pia baadhi ya waamuzi kutoka nje kusaidia mechi kwenye kuamua kwa sababu wao wakikosea itaonekana ni makosa ya kibinadamu na hawapendelei. Hata hivyo kwa sasa tusiwatie waamuzi wetu presha kwa makosa ya kawaida kabisa.