Kwani, inalenga kukamilisha na kuanzisha ujenzi wa miradi mingine mipya, ikiwamo katika sekta za maendeleo ya elimu, afya, barabara na miundombinu mingine kwenye jamii.
Hiyo kitaifa ni serikali inayoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuwanufaisha Watanzania wote katika kila kada na makundi ya kijamii, mtazamo ni kuondoa kero zinazowakabili wananchi hao, ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mipya ya kimkakati iliyoko katika utekelezaji.
Binafsi namuunga mkono sana Rais, kwa kuona umuhimu huo akachukua hatua za kuhakikisha anapambana ipasavyo akiamini itatoa fursa kila Mtanzania unufaike nayo pindi itakapokamilika kujengwa, akiendeleza nyendo za watangulizi.
Watanzania wenzangu, niseme Rais anajitahidi kuonyesha uwezo alionao wa kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele, hata anapoona watendaji wakienda kinyume na maadili ya utumishi wa umma, anawavurumisha, ili kutimiza azma ya kaulimbiu ya serikali yake ‘kazi iendelee.'
Wiki hii mboni yangu ya jicho imejisogeza wilayani Magu mkoani kwetu Mwanza, ambako halmashauri ya wilaya hiyo inakusudia kutenga fedha kwa ajili ya kuunganisha taa za barabarani mitaani ikitumia fedha za makusanyo ya ndani, ili kuwaondolea kero wananchi wake na wageni wao kutoka katika maisha ya kupita gizani nyakati za usiku.
Pia, najua halmashauri hiyo iko katika matarajio ya kutekeleza ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi mjini humo na stendi ya mabasi madogo, eneo la Kisesa ili kuondoa adha wanayoipata abiria wake wanaposafiri na wale wanaotoa huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo hayo.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, walitoa mapendekezo hayo katika mkutano wao wa baraza, walipopitisha bajeti yao ya mwaka wa fedha 2022/23 ya shilingi bilioni 50.662, iliyosomwa na Mchumi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Phabian Kabambara.
Wanasema hata miji mingine kama vile Kahangara, Nyanguge na Kisesa nayo itanufaika na taa hizo za barabarani, nami binafsi nawapongeza kuchukua uamuzi huo ili kuwaletea maendeleo wana Magu na vitongoji vyake, hivyo unahitajika usimamizi imara usiolega.
Siku zote mtu anaambiwa kupanga ni kuchagua. Anaweza kuamua, kila kitu ni mipango na uthubutu wa kutekeleza, hivyo nawapa hongera sana Halmashauri ya Magu hususani madiwani kuliona hilo la kukusudia kuujenga Mji wa Magu katika mandhari ya kisasa, ambao utakuwa mfano kwa wilaya nyingine mkoani Mwanza.
Hatua waliofikia ni njema kabisa, isipokuwa angalizo kutoka uzoefu ni tabia za baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu, ambao mradi unapoibuliwa, wao kazi yao ni kubadilisha matumizi yake bila ya kufuata taratibu, ili kuukwamisha, aweze kupata mwanya wa kufanya ubadhirifu. Hao tuwaogopeni kama ukoma kwenye miradi yetu.
Watendaji wa aina hiyo wana roho za tamaa ‘mtakavyote’, wahujumu uchumi, wanaotaka kunufaika binafsi badala ya jamii nzima. Nimewahi kushuhudia mradi mmojawapo hapohapo Magu wakati fulani uliokuwa tayari unaendelea, ukatekelezwa kwa kusambazwa mabomba ya maji.
Cha ajabu baada ya siku kadhaa mabomba hayo yalipotea ghafla kumbe mradi ulihamishiwa kata nyingine na wajanja, ambako haukuwa umepangwa kutekelezwa kwenye bajeti, hakuna kiongozi aliyeitisha mkutano wa hadhara wa kata wala kijiji kuelezea wananchi kilichotokea.
Kitendo hicho kilinipa maswali mengi ya kutafakari nakujiuliza kulikoni? Maana mahali hapo sikuwahi kusikia hata ufuatiliaji kutoka baadhi ya viongozi wao wa kuchaguliwa, walau wananchi kufahamishwa hata kama mradi wao umehamishwa.
Nawaambieni baadhi ya watendaji wa kata na watumishi wa aina hii, itakapotokea upotoshaji wa namna yoyote ni ukiukwaji mkubwa wa mali ya umma.
Wenye mamlaka katika maendeleo yetu iwe kwenye kata zenu na vijiji, mitaa au vitongoji. Katika siri yoyote kwenda kinyume na ilivyopangwa rasmi ni ukiukwaji na daima si vinginevyo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








