Sera mpya mazingira, iwe chachu kupambania mabadiliko tabianchi

10Feb 2022
Jenifer Gilla
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Sera mpya mazingira, iwe chachu kupambania mabadiliko tabianchi

FEBRUARI 12 au keshokutwa, ni siku muhimu kitaifa katika muktadha wa mazingira, kwa kuwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, anatarajiwa kuzindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021.

Sera hiyo imejumuisha masuala ya mazingira yaliyokuwamo katika sera ya mwaka 1977 na kuongeza mapya sita, ambayo ni udhibiti wa taka za kielektroniki; uchafuzi katika shughuli za utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi; usimamizi wa matumizi ya kemikali; mabadiliko ya tabianchi; kudhibiti viumbe hai; na usimamizi wa matumizi salama ya baioteknolojia ya kisasa.

Ni uzinduzi unaoambatana na shughuli mbalimbali za hifadhi ya mazingira hadi siku ya kilele hicho, kuanzia tarehe kama hiyo mwaka jana. Hapo ni sehemu ya kuonyesha masuala ya msingi yanayoelekezwa katika sera mpya, ikiwamo kupanda miti na kusafisha mazingira.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mary Maganga, anafafanua kuwa sera hiyo inaongeza wigo inakoshughulikia na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika, ili kuleta maendeleo endelevu.

Serikali inapaswa kupongezwa kwa uamuzi wa kuibadilisha sera hiyo na kuongeza maeneo muhimu, ikiwamo suala la kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwa ndio adui mkuu wa mazingira na kikwazo za maendeleo endelevu.

Kuwapo kipengele cha mabadiliko ya tabianchi katika sera mpya, kunaonyesha namna serikali imedhamiria kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoisumbua dunia kwa sasa.

Athari zinaoneka wazi kwa sasa, ikiwamo mvua isiyotabirika na ama kwa kiwango kikubwa au kidogo, tofauti na matarajio yaliyoko. Ni hali inayosababisha athari nyingi, moja kubwa ni shughuli za kilimo ama kusimama au kuyumba katika baadhi ya mikoa.

Mabadiliko ya tabianchi yanachangia kuwapo joto kali na linalovuka kiwango stahiki, kutokana na tabaka la juu la dunia (ozone layer) kuwa wazi na kuruhusu miale ya jua kupita moja kwa moja hadi duniani. Hapo inachangia kuwapo ukame, mazao kukauka kabla hayajakomaa na maradhi kwa viumbe hai.

Ni matumaini kuwa sera hiyo mpya itakuwa mwongozo kwa jamii, wa namna ya kupambana na athari ili utekelezaji wake uwe unaoleta tija kwa taifa kwa muktadha wa utunzaji wa mazingira yetu.

Shime wanajamii, tufuate maelekezo yanayotolewa kupitia sera hiyo na vyombo vya umma na wakala mamlaka binafsi katika kuhakikisha mazingira yetu tunayalinda na kuyatunza. Kama sera inataka kila mwananchi apande walau miti mitatu katika nyumba yake,basi na iwe hivyo.

Sote basi tufanye hivyo bila ya kusukumwa, kwa kuwa upo usemi ‘Tunza mazingira nayo yakutunze’. Kwa serikali na wadau wa mazingira, ni wajibu wao wahakikishe wanasimamia miongozo iliyoko katika sera.

Hiyo ni msaada kupambana na changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza, kutokana na mabadiliko ya mifumo kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani.

Walimu nao wapewe sura ya mtaala unaofundisha miongozo hiyo kwa wanafunzi, ili ufundishaji wao uwajengee watoto ari ya kutunza mazingira na kuona umuhimu wa mazingira bora tangu umri mdogo na kurejesha uasilia uliokuwapo kabla ya kuharibika, kutokana na shughuli za kibinadamu.

Ripoti zinaonyesha nchi zenye kiwango kikubwa cha uchafuzi wa hali ya hewa, ziko hatarini zaidi kuwa na viwango vikubwa vya magonjwa yasioyakuambukizwa na kuchangia asilimia 72 ya vifo vyote, asilimia 16 katika vifo hivyo vinachangiwa na sumu inayotokana na uchafuzi wa hali ya hewa.