AU yahofia kasi kurejea wimbi la mapinduzi

09Feb 2022
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
AU yahofia kasi kurejea wimbi la mapinduzi

MAPINDUZI ya serikali zilizochaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura, barani Afrika, yanaelekea kuwa kitisho kinachohofisha jumuiya ya kimataifa inapotizama hatima ya demokrasia kwenye mataifa hayo yanayojikongoja kimaendeleo.

Wiki iliyopita kwenye Mkutano wa 35 wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika makao makuu ya umoja huo, Addis Ababa, viongozi wa nchi wanachama, wanajadili suala la ongezeko la mapinduzi ya kijeshi.

Mapinduzi hayo yaliyojitokeza kwa kipindi kifupi yanatikisa ukanda wa Afrika Magharibi na viongozi waliohudhuria mkutano huo, wanalilalamikia wimbi hilo.

Kikao hicho kinasema ni mara tano sasa kwa mwaka uliopita, serikali zimepinduliwa na kuandika historia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, Februari 5, mwaka huu, akitoa hotuba kwa njia ya mtandao, kwenye mkutano huo, anasema AU ni chanzo cha matumaini duniani.

Anasema, ushirikiano kati ya UN na AU, una nguvu zaidi kuliko hapo awali, na kwamba ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na ya 2063 ya Afrika Tunayoitamani-‘The Africa We Watu’, ni nguzo kuu.

Wakati Katibu Mkuu wa UN, anasema hayo, wakuu wa AU wanahitimisha mkutano kwa kulaani wimbi la mapinduzi, wakisema limesababisha mataifa kadhaa kusimamishwa uanachama katika umoja huo.

Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo, anasema mapinduzi yaliyotokea nchini Mali yameambukiza nchi nyingine akisema maofisa wa kijeshi wa mataifa jirani za Guinea na Burkina Faso.

Wakati mapinduzi ya Afrika Magharibi, yakijadiliwa mkutanoni, hatua ya jeshi kuchukua madaraka nchini Sudan, Oktoba mwaka jana, pia ilisababisha maandamano makubwa mitaani ya kudai kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.

Ingawa inaelezwa, idadi ya mapinduzi barani Afrika, imekuwa ikipungua, kutokana na kuenea kwa uchaguzi na uhamishaji wa madaraka kwa njia ya amani, wimbi jipya linaanza kuleta hofu.

Nchi mbili ambazo jeshi limenyakua mamlaka hivi karibuni, Burkina Faso na Mali, zimekuwa zikijitahidi kuzuia uasi wa Kiislamu.

Aidha, wiki iliyopita, kulikuwa na jaribio la mapinduzi nchini Guinea-Bissau, ambalo Umaro Mokhtar Embaló aliyalaumu magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Nchi hiyo iko kwenye sehemu kuu ya usafiri kati ya nchi zinazozalisha dawa za kulevya katika Amerika ya Kusini na masoko ya Ulaya.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, anasema hali ilivyo inaleta hisia kuwa Afrika inarejea katika kipindi ambacho mapinduzi yalikuwa mambo ya kawaida, akisema ni jambo lisilokubalika.

Umoja wa Afrika, pia umelalamikiwa kwa kuchukua hatua zisizo sawa katika baadhi ya matukio, likiwamo la kutoisimamisha Chad, baada ya baraza la kijeshi kuongoza serikali, baada ya kifo cha kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo, Idriss Deby Itno, kilichotokea katika uwanja wa mapambano.

Tofauti na hayo, mjini Addis Ababa, Rais Uhuru Kenyatta amepongeza juhudi zilizofanywa na Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa malaria, miaka miwili iliyopita.

Uhuru, alikuwa akiwasilisha ripoti ya hatua zililizopigwa katika makabiliano ya ugonjwa huo.

Umoja wa Afrika ni muungano wa mataifa 54 ya Afrika yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa bara hilo.

Maamuzi muhimu ya AU yanafanywa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika ambao unawakutanisha wakuu wa mataifa na serikali za nchi wanachama unaofanyika mara mbili kwa mwaka.

AU pamoja Kamisheni ya Umoja wa Afrika makao makuu yake yako Addis Ababa nchini Ethiopia.