Litafutwe suluhisho la kudumu kukomesha mikasa moto sokoni

17Feb 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Litafutwe suluhisho la kudumu kukomesha mikasa moto sokoni

USIKU wa kuamkia Februari 13, moto mkubwa ulizuka kwenye soko la wafanyabiashara maarufu kama 'wamachinga' eneo la Mbagala Rangitatu, jijini Dar es Salaam.

Sehemu iliyoathirika zaidi ni wauza nguo za mitumba ambayo baadhi ya bidhaa ziliteketea. Tumshukuru Muumba hakuna ripoti za vifo.

Ajali hiyo ya moto imetokea ikiwa imepita takriban mwezi mmoja tangu kuungua Soko la Karume, Dar es Salaam hata kuteketezwa vibanda mali ya wafanyabiashara.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo, Jumapili iliyopita mbali na kuthibitisha tukio, akaunda tume kuchunguza akiipatia siku nne iwe imekamilisha uchunguzi huo, ambayo ilitarajiwa juzi ripoti yake kuwasilishwa kwa aliyeunda.

Hiyo si mara ya kwanza soko la Mbagala Rangi Tatu kuungua, kwani Machi 6, mwaka 2018, soko hilo liliwahi kushika moto.

Ni usiku na kuamkia Januari 16, Soko la Karume lililoko Ilala Mchikichini, nalo liliungua na kuharibu mali nyingi za wafanyabiashara zaidi ya 3,500, ikiambatana na hasara kubwa. Nako Mwenyezi, ashukuriwe hakuna kifo kilichoripotiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliunda tume na majibu yaliyotoka, chanzo ni vijana wa wasio na maadili maarufu ‘mateja’ ndiyo walisababisha ajali hiyo kwa kuwasha mshumaa walioutelekeza bila ya kuuzima.

Julai 11, mwaka jana, soko kubwa si Tanzania tu, bali la Afrika Mashariki na Kati, Kariakoo jijini Dar es Salaam na likateketea kwa moto uliozuka kuanzia saa tatu usiku.

Ingawa chanzo hakijajulikana, lakini ulidaiwa kuanza kwenye paa la juu la soko hilo na baadaye kusambaa kwenye maeneo mengine.

Hapa nimeorodhesha ajali za moto kwenye masoko ambayo kwa siku za karibuni, zimekuwa zikiibuka na kuacha maswali mengi kwa Watanzania.

Ingawa si mara ya kwanza kuwapo ajali mbalimbali za moto sehemu mbalimbali, ikiwamo kwenye masoko, hata mwaka 2017 soko la Sido Mbeya liliungua moto.

Sasa, umefika wakati wa kujiuliza kwa kina na kutafakari, sababu za masoko hayo kuungua, hasa kwa siku za karibuni.

Tuwapongeze viongozi wa serikali kwamba wamekuwa karibu na wananchi pamoja na waathirika wote wa majanga, ikiwa ni pamoja na kuunda tume. Niseme, umefika wakati hizi tume baada ya kutoa ripoti zao, ziende mbali zaidi na kutafuta suhuhisho la kudumu, maana inaonekana kuwapo dalili za matukio kuwa endelevu.

Tume ikija na majibu ni ‘mateja’ waliochoma isiishie hapo, bali hatua zaidi inahitajika. Nitapenda, ikiletwa majibu kuwa ni hitilafu ya umeme au kinamama walikuwa wameacha majiko ya mkaa yakiwa yanawaka, halafu ikaishia hapo, bado tatizo linaweza kuendelea kwingine.

Ni sawa na mzazi kufanya uchunguzi na kugundua mtoto wake amefariki na ugonjwa malaria, halafu ikaishia hapo bila kuanza kununua chandarua, kupuliza dawa na vitu vingine zitakavyosababisha mbu wasikaribie nyumba yake, badala ya kusubiri tena mwingine augue au afe, ili afanye uchunguzi mwingine.

Tusisubiri masoko mengine yaungue ili kuunda tena tume zingine. Matokeo ya tume zote yaangaliwe, na vyanzo zitakavyonekana ndiyo sababu kuu ya masoko kuungua, basi kazi ifanyike ili kuzua moto usitokee tena.

Kama ni mateja, basi mkakati ufanywe kuongeza walinzi masokoni, ili kutoruhsu mtu yoyote kusogelea maeneo hayo hasa linapokuwa limefungwa. Kama ni hitilafu ya umeme basi mifumo yote ya umeme kwenye masoko yote nchini yaangaliwe upya.

Yafumuliwe na kuanza kutandaza upya kisasa zaidi. Kama ni hujuma, basi nadhani wana usalama wetu wanajua nini la kufanya. Hii ndiyo maana ya tume ambazo viongozi wetu wanapendekeza. Wanataka sababu ikipatikana, basi wanaohusika sasa wafanyie kazi ili kuzuia lisitokee tena.

Hapa ni suala la uwajibikaji pamoja. Lisiachwe kwa viongozi tu, bali hata kada zingine kama wanausalama wote wakiwamo askari Polisi, Zimamoto na Uokoaji, na hata wadau wa umeme –Tanesco. Niseme tu, kinga ni bora kuliko tiba.