Waamuzi sasa ndio 'kirusi' cha soka letu

31Oct 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Waamuzi sasa ndio 'kirusi' cha soka letu

KWENYE mitandao ya kijamii nimekutana na sehemu ambayo waandishi wa michezo wa nchi za Ghana, Nigeria, Burkina Faso na Cameroon, wakipostiana video na picha za mechi kati ya Geita Gold dhidi ya Yanga, wakiulizana ni kwa nini mwamuzi aliamua iwe penalti?

Walikuwa wakiizungumzia mechi ya juzi kati ya Geita Gold dhidi ya Yanga iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ambapo moja ya tukio lililowaacha watu hoi ni mwamuzi wa kati, Florentina Zablon, kuamuru mkwaju wa penalti ambao mchezaji George Wawa alikuwa ameushika mpira nje ya eneo la hatari.

Kwa bahati mbaya sana penalti hiyo ya utata ndiyo iliyoamua mshindi kwenye mechi hiyo, Yanga ikishinda kwa bao 1-0.

Nilichofurahi ni kwamba kumbe Ligi ya Tanzania imekuwa ikifuatiliwa sana miaka ya hivi karibuni, tofauti na huko nyuma. Ilikuwa si rahisi kuona waandishi, wachambuzi na wadau wa soka kwenye nchi kubwa zilizoendelea kisoka kama hizo zikiifuatilia Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini kutokana na uwekezaji mkubwa wa pesa, ligi kuonyeshwa karibuni mechi zote za msimu, pamoja na wachezaji kutoka kila pembe ya Afrika na dunia, wakimiminika kucheza soka la kulipwa nchini, hivyo kuifanya Ligi ya Tanzania kufuatiliwa sana na kutajwa kama ni moja kati ya ligi bora Afrika.

Hata hivyo, nasikitika kusema kuwa ligi bora inachezeshwa na waamuzi ambao si bora. Tumeona kwa siku za karibuni waamuzi wamekuwa wakisimamishwa, kupelekwa kwenye kamati na kufungiwa kutokana na kuboronga.

Kwa kawaida mchezo wa soka ni wa makosa, na tunaona hata huko nje waamuzi wanakosea, lakini si kwa namna ambayo waamuzi wa Tanzania wanakosea.

Mfano tukio la juzi halikuwa ni la kutafsiri sheria, bali lilihitaji umakini tu kwa sababu ni kweli mchezaji wa Geita Gold alishika, lakini je, ni ndani ya eneo la 18?

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo, alishawahi kusema mwamuzi wa mpira wa miguu ni sawa na hakimu au jaji, hivyo anatakiwa kuwa makini sana.

Na tunaambiwa kwenye moja kati ya mafunzo yao wanaambiwa kuwa ni bora umuache mhalifu kama hakuna ushahidi uliokamilika kuliko kumfunga mtu ambaye hana kosa.

Hata kwenye uamuzi ni bora ukatae bao au penalti kama huna uhakika, kuliko kutoa vitu hivyo kimakosa. Ni kwa sababu mwamuzi anadhulumu haki ya mwingine.

Kwa leo inaweza kuonekana kama haina umuhimu, lakini ipo siku wanaweza kuja kuikumbuka. Geita Gold inaweza huko mbele kuhitaji pointi moja ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika au Shirikisho ama kujinusuru kushuka daraja, ndipo watu watakapokumbuka kuwa kuna siku walinyimwa pointi yao kwa kuruhusu penalti ambayo si halali.

Nilichoshangaa na kuona ni mwamuzi akitoa penalti hiyo akionekana kabisa kuwa na uhakika, kwani pamoja na wachezaji wa Geita Gold kumzonga hakustuka na kuamua kwenda kumuuliza mwamuzi msaidizi.

Mwamuzi msaidizi naye ambaye naye alikaa kwenye sehemu ambayo alitarajiwa kuona tukio hilo vizuri zaidi, hakujishughulisha hata kumsaidia mwamuzi wa kati licha ya kuzongwa na wachezaji.

Kwa tukio hilo na mengine yaliyotokea kwa waamuzi, iwe kwa makusudi au bahati mbaya hayaleti taswira nzuri kwenye soka la Tanzania. Wale waandishi wa Afrika Magharibi wanaweza kuona kuwa aina hiyo ya uchezeshaji ndiyo maana timu za Tanzania hazifanyi vizuri zinapokwenda kucheza mechi za kimataifa.

Imefika wakati sasa wadau wote wa soka nchini Tanzania tuone aibu na kukataa mambo haya ambayo sasa yameanza kuonekana kama ya kawaida kwenye soka letu.

Ama imefika kweli wakati wa kuletwa mashine za kumsaidia mwamuzi (VAR), au iwekwe kanuni ya kualika waamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha baadhi ya mechi za Ligi Kuu nchini.

Nadhani waamuzi wengine wanaweza kutusaidia kuonyesha hivi ni kweli waamuzi wetu tu wana matatizo au hata wengine.

Nasema hivi kwa nia njema tu kwa sababu kama likifumbiwa macho kuna siku yanaweza kutokea maafa viwanjani kwa sababu ya uzembe wa mwamuzi. Fikiria kama adhabu ile ingekuwa inaelekezwa upande wa pili, uwanjani kungekuwaje? Nawaza tu kama penalti ile ingekuwa dhidi ya Mbeya City kule kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Yaliisha salama kwa sababu mashabiki wa Geita Gold ni wastaarabu na wote walikuwa kama wapo ugenini kutokana na mchezo huo kuchezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa sasa kuchukua hatua nyingine stahiki kabla siku serikali haijaingia kati baada ya maafa kutokea uwanjani, hii haikubaliki kabisa na tulishaeleza kuna haja ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kumulika kwa umakini suala hili kwani huenda kuna mkono mzito unaotoka mfukoni kwa baadhi ya klabu na kuingia mifukoni mwa waamuzi kwa lengo la kubebwa.