Mjadala wa nishati safi ulete suluhisho kushuka bei ya gesi

30Oct 2022
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Mjadala wa nishati safi ulete suluhisho kushuka bei ya gesi

WIZARA ya Nishati imeandaa mjadala wa kitaifa wa siku mbili kuanzia Jumanne ijayo kujadili umuhimu wa nishati safi hasa wakati huu wa kasi ya mabadiliko ya tabianchi ambayo madhara yake yanaonekana dhahiri kwa sasa.

Mkutano huo utakuwa na mada za upatikanaji, upataji na unafuu wa nishati mbadala wa tungamotaka (kuni na mkaa), mtungi wa gesi ya kupikia kila nyumba, athari za kiafya zitokanazo na nishati ya kupikia na ustawi wa wanawake na ugharamiaji wa nishati safi ya kupikia.

Ni mjadala muhimu sana utakaofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hasa wakati huu ambao dunia inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku waathirika wakubwa wakiwa nchi za Afrika ambazo mchango wao katika kuzalisha hewa ukaa ni mdogo sana.

Mjadala mkubwa kwa sasa nchini ni namna ya kupata nishati safi kwa bei nafuu. Wengi wanatamani kuachana na matumizi ya mkaa watumie gesi lakini bei yake imeendelea kupaa kila uchao.

Idadi ya tani za mkaa zinazoingia Dar es Salaam kila siku zinatosha kuonyesha kwa kiasi gani tunakwenda kuwa na jangwa kubwa siku za usoni na tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeeleza kuwa mvua zilizotarajiwa kunyesha kwenye mikoa 14 hazitakuwapo tena, hivyo kutakuwa na ukame.

Aidha, athari zinaongezeka zaidi na sasa Dar es Salaam inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kutokana na kupungua kwa maji katika Mto Ruvu na vyanzo vingine. Vyanzo vingi vinaendelea kukauka huku mifugo na viumbe vingine vikiwa katika hatari ya kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa malisho.

Hali ni mbaya maeneo mengi ndiyo maana naona huu mjadala ni muhimu ili kupata suluhisho kwa mazingira yetu tunawezaje kuendelea na maisha katika wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi.

Ninafurahi mjadala huu unafanyika siku chache kabla ya mkutano wa dunia wa mazingira (COP270) unaoanza Novemba 6, mwaka huu nchini  Misri ambako kila nchi itatakiwa kueleza mipango yake ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Wakati mwingine mawazo kutoka kwa wananchi wa kawaida kabisa yanaweza kuwa na suluhisho kubwa kwa kuwa wanaeleza kutokana na mazingira wanayoyaishi kuliko kufuata yale yanayotakiwa na nchi wahisani.

Mada za mjadala huu ni nzuri kama washiriki watakuwa na 'free mind' kwenda kujadili tulikotoka,tulipo na tunakokwenda kwa kuangalia kwa jicho la pekee siasa za duniani kwenye kila jambo hasa nishati.

Mathalani, tunasema mtungi wa gesi ya kupikia kila nyumba tujiulize nyumba za kijijini zinawezaje kumudu kununua gesi kwa ajili ya matumizi yao yote ya kutwa, kipato chao kwa mwezi ni Sh. gapi, gesi mtungi mdogo ni Sh.25, 000 na mkubwa 55,000 bado hajalipia usafiri.

Ni kwanini gesi iwe ghali nini kinaweza kushusha bei ya gesi ili kweli ipatikane kila nyumba, ni kwa nini nyumba inatumia gesi kwa vitu vidogo vidogo na kuwa na mkaa au kuni kwa ajili ya kupikia vya muda mrefu.

Ni kweli kuna athari za kiafya lakini watu wanafanyeje kupata nishati safi kwa bei inayowezekana kwa kila mtu na kwa urahisi zaidi je kuna uwezekano wa kuondoa gesi,wasambazaji wa gesi ni wafanyabiashara kutoka wapi na je wanaona Tanzania inavyoendelea kuwa jangwa?

Naamini hakuna mtu anataka kutumia nishati ngumu na yenye madhara ya kiafya kwake,kama atapata nishati safi kwa wakati na bei nzuri,hivyo ni muhimu mjadala wa kina wenye kuruhusu mawazo kinzani ukafanyika kuwezesha mabadiliko halisi.

Haitarajiwi mkutano huu kuwa kama mingine kwamba watu wanakutana, inatumika gharama kubwa, wanatoka na maazimio ambayo yanakwenda kubaki kwenye makabati hadi wakati mwingine kutakapokuwa na mkutano mwingine.

 

Tunatarajia pamoja na mambo mengine wataiwakilisha nchi kwenye COP27 waende na mawazo yetu, maamuzi yetu kwamba Watanzania tunaona suluhisho kwa kadri ya mazingira yetu ni hivi na hivi,tufurahi tunapopewa misaada ya mabadiliko ya tabianchi lakini nasi tuna maisha kwa kadri ya mazingira yetu.