Ilikuwa ya kipekee kutokana na simulizi ya Mtoto Elizabeth Sagati, ambaye alisimulia mapito aliyopitia katika masomo yake mpaka kumaliza shahada ya uzamili akisomea uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma
Taasisi hiyo inayodhaminiwa na Women Fund Tanzania (WFT), iliandaa kongamano lililowakutanisha watoto zaidi ya 781, wazazi na walezi 143 ambao walifunzwa namna ya kutumia teknolojia kupinga ukatili na rushwa ya ngono.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwamo Ofisa kutoka Idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, John Deogratius.
Katika kongamano hilo kitu kilichovuta taswira na kukonga mioyo ya watu ni simulizi ya Elizabeth Sagati, kama ilivyokaririwa na mwandishi wa makala haya akitamka:
“Mimi ni Mmasai, nimepitia magumu sana katika maisha yangu, kwa sasa mimi ni mwanafunzi katika chuo cha Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia, lakini hapo nyuma nilisoma uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma, mpaka kufika leo hii ni kwa neema ya Mungu kwa sababu nimepitia magumu mengi.”
Katika familia yake, anasema ni mtoto wa pili kuzaliwa upande wa mama, lakini kwa baba wako wengi, akiwa amesoma darasa la kwanza mpaka la saba na baada ya kumaliza, baba yake akataka kumuozesha akiwa na miaka 12, lakini mama hakukubali.
Kwa hiyo mama huyo akampa ujumbe huo, lakini yeye alikataa kushirikiana naye, yeye akisema hataki kuolewa anahitaji kusoma ili atimize ndoto zake, huku mama akimsihi bora akubali tu kwani angemfarakanisha na baba yake, wakashindwa kuelewana. Mtoto anasema akasimamia hoja, heri iwe hivyo, lakini abaki anasoma.
Anasema, wakakimbizana na baba yake, hivyo mpaka akafanikiwa kwenda shule, kitu ambacho anashukuru zaidi walikuja wafadhili kutoka Finland, wanaojihusisha na kuwasomesha watoto wa kimasai katika mazingira magumu.
Katika hao naye akawa mmoja wapo, wakamchukua akaanza kusoma wakati anasoma kidato cha kwanza hakurudi likizo nyumbani, kwa sababu kulikuwa na hofu akirudi wangemlazimisha aolewe. Kwa hiyo, lile shirika likamtafutia makazi mjini Morogoro, shule ikifunga akawa anaenda kupumuzika hapo, bila ya kwenda nyumbani maana ikafika ajenda ni lazima aolewe.
Eliza akaendelea kusimulia kuwa nilipomaliza kidato cha pili, kwa kuwa likizo ilikuwa ndefu nikasema ngoja niende nyumbani nikasalimie wazazi ndugu jamaa na marafiki, nilivyofika tu nyumbani wakanikamata wakanipeleka wakaenda kunificha huko wanakokujua wenyewe ili nisirudi shule niolewe wakaniwekea mdada wa kazi akawa ananihudumia.
Yule dada kwa sababu alishapewa mikakati asinipe simu lakini niliendelea kumlaghai baadaye akanipa nikampigia matroni wa shuleni nilikokuwa nasoma nikamueleza hali halisi ya kilichonikuta baada ya kwenda nyumbani kusalimia.
Akachukua timu ya Askari, wakaja mpaka nyumbani kipindi hicho wenzangu shule wanaendelea kusoma nikarudishwa shule na baba yangu akapewa onyo asirudie tena.
Nilipofika shule waliniambia wameshafanya usajili kwahiyo siwezi kuendelea na masomo labda nikae mpaka mwakani ndio nikajiunge tena ndio nitapata usajili na namba ya kufanyia mtihani kidato cha nne.
Kwa hiyo nyumbani nimekaa mwaka mmoja angekuwa ni mtoto mwingine angeshakata tamaa ya maisha na asingeendelea na masomo tena”
Aliendelea kuwa wakati huo tayari baba na mama yake walishatengana kupitia hilo baba alimwambia mama kwa sababu umekaidi amri yangu kakae huko peke yako na watoto wako
Baada ya kukaa huo mwaka mzima lile shirika likaniendeleza tena kielimu mpaka nikamaliza kidato cha nne, baada ya hapo nikaenda chuo cha uandishi wa habari Morogoro, nikasoma uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma sasa nimemaliza na naendelea na masomo mengine.