Pia ikumbukwe hata katika msimu uliopita, nchi yetu haikupata mvua ya kutosha, ambayo imechangia jambo hilo ambalo unaweza ukaliweka kwenye matatizo ya tabianchi.
Ni wakati ambao viongozi wa serikali wanachukua hatua kadhaa kukabiliana na adha hiyo, ili kuwanusuru wananchi wao wasiendelee na adha hii ambayo imekuwa kero kubwa hasa kwa kinamama.
Siku zote ambazo maji yanakuwa ya shida, kwa asilimia 90 na zaidi wanaoteseka ni kinamama, kwani wao ndiyo wana matumizi makubwa ya maji kutokana na kuwa kiongozi wa familia.
Wanalazimika kuamka mapema kwenda bombani au visimani kwa ajili ya kuchota au kusaka maji, na huko wakati mwingine wasipate au wanakutana na foleni kubwa.
Wakati mwingine kutokana na kuamka alfajiri sana, wanakumbana na changamoto mbalimbali ambazo zinawakwaza na kuwasababisha matatizo mbalimbali.
Wanawake kuna wakati wanachelewa kurudi majumbani kutokana na kutafuta maji kwa umbali mrefu na kuwakuta waume zao wamenuna, au wamefura kwa hasira ambazo wanakuwa hawaamini kama kweli kipindi chote hicho alikuwa bombani, kisimani au alikuwa amepatia sababu.
Kutokana na hayo yote, niliyoainisha na mengine, imefika wakati sasa kuwa na matumizi bora ya maji kwa wakati wa kipindi hiki cha ukame. Maji yanapatikana, lakini kwa shida. Hivyo, kwa sasa matumizi yawe ya bajeti na si kama ilivyokuwa hapo mwanzo.
Ni sawa tu na wakati wa njaa, au uhaba wa chakula ambao familia inalazimika kupika kwa bajeti, ili kuweka akiba kinachobaki kwa ajili ya kutumika kwa muda mrefu.
Kama familia inakula mchana saa sita na saa mbili usiku, wakati wa njaa, inaweza kuamua sasa watakuwa mara moja. Wakishakunywa chai asubuhi, basi wanaweza kula saa 10 jioni hadi kesho yake mpaka kipindi hicho cha mpito kitakapopita.
Sitegemei kwa sasa mtu akipata ndoo moja, basi yote anakwenda kuoga mtu mmoja. Angalau basi ndoo moja aoge baba na mama, ili kumpa nafuu mwanamke ambaye, kila kukicha adamke asubuhi kusaka maji.
Kuna wakati mwingine maji yanapotea kwenye mabomba kwa ajili ya kumwagia bustani tu. Huo nao pia ni upotevu wa maji bila ya sababu yoyote ya msingi.
Maji, hasa ya bomba, kwa sasa yanatakiwa yatumike kwenye sababu za msingi tu ambazo ni lazima yatumike. Mtu anatumia maji ya bomba kuloweka tu nguo chafu na kuziweka siku nzima, wakati kuna wenzake wanakosa hata maji ya kunywa.
Kuna baadhi ya familia huwa na hazina kupitia vyombo vya kuhifadhi maji, wenyewe akichota wakioga, kupikia na kufua basi yakiisha wanakwenda tena kuchota. Hiyo siyo sahihi hata kidogo.
Ifike wakati Watanzania tuwe na utaratibu au utamaduni wa kuwa na vitu vya kuhifadhia maji, ili ikitokea dharura kama hii basi angalau athari wenye familia zetu haziwi kubwa sana.
Ni sawa tu na wale wanaonunua vyakula kama mchele, unga sukari, mafuta ya kupikia na kuweka ndani, hawa hata kama siku hana pesa, au anayo kidogo hawatolala na njaa.
Kwa sababu wana akiba ya chakula ndani, tofauti na wale ambao wanatafuta pesa kila siku kwa ajili ya kununua unga nusu au kilo moja ili wapike ugali. Familia hii siku ikikosa pesa, italala na njaa.
Akiba na bajeti ni vitu muhimu sana. Siku hizi kuna matangi ya kuhifadhia maji kwa wale wenye uwezo, lakini kwa watu wa kipato cha kawaida kuna vyombo vya kuhifadhi maji vinaitwa 'majaba'.
Haya yanaweza kusaidia kipindi ambacho maji yanatoka kujaza ya kutosha ili ikitokea hali kama hii yanasaidia kuondoa presha ya kusaka maji kwa nguvu zote na mahali popote.
Kwa hili lililotokea sasa liwe funzo, kwanza Watanzania kuanza kutumia maji kwa uangalifu na maeneo muhimu tu na si kumwagamwaga ovyo, pia tuwe na utaratibu wa kuhifadhi maji.