Viongozi wakisimamia  sheria wataokoa misitu

02Aug 2022
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Viongozi wakisimamia  sheria wataokoa misitu

VIONGOZI wa serikali kuanzia ngazi za mitaa, vijiji, wilaya, mkoa hadi taifa wakati umefika kuhamasisha na kusimamia jamii kufuata sheria za misitu zilizoko wanapoandaa mashamba ili kuepuka ukataji miti ovyo unaosababisha upotevu wa misitu, ukame na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

Mhifadhi mwandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Manispaa na Wilaya ya Morogoro, Faustine Msokwa anasema  kuwa jamii imekuwa haiangalii mambo ya maendeleo ya baadaye kwa ajili yao na taifa bali hukata miti kwa juhudi zote lakini bila kupanda mingine.

Miti inayokatwa ni kwa ajili ya kusafisha mashamba na kuanza kilimo jambo ambalo lina manufaa kifedha kwa muda mfupi, lakini likichangia ukame na athari nyingine zitakazolikumba taifa kwa muda mrefu.Suala la ukataji miti ovyo na uchomaji mkaa linasababishwa na viongozi wa vijiji ambao ndio wana umiliki wa ardhi za vijiji kutokuwa na makini tena bila kuweka msisitizo ikiwamo sheria ndogo na taratibu za matumizi ya ardhi hiyo ili kuendelea kubaki kuwa endelevu, anaonya Msokwa.Taasisi kama TFS zinasisitiza usimamizi shirikishi wa mazao ya misitu (USMJ) unaotaka ushiriki wa wadau wote wa misitu ambao ni pamoja na wakulima na wafugaji ambao wamekuwa wakivamia maeneo na kudai wanasafisha kwa kilimo au kukaa na mifugo huku wakikata miti ambayo inatakiwa kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.Anasema licha ya kukamatwa wahalifu hao wa misitu wanaofikia hata 50 kwenye  mashamba wanaodai wanaandaa mashamba kwa kuwa wana kibali cha kijiji, lakini ukifuatilia miti wanayoikata wanachoma mkaa pia hawapo wenye vibali vya kusafisha shamba au hata kama wapo ni wachache, jambo ambalo ni hatari kwa  uhifadhi wa misitu.

Yote hayo inaonyesha udhaifu wa viongozi vijijini katika kusimamia rasilimali mfano misitu, maji na ardhi mambo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya wanavijiji na taifa pia.

 

Ni ukweli kwamba ukataji miti ovyo na uchomaji wa mkaa bila kufuata utaratibu unazifanya hata manispaa na wilaya kushindwa kukadiria kiwango cha mkaa kinachohitajika kutumika kwa jamii hizo.Hata hivyo upo mkanganyiko unaorudisha nyuma suala la usimamizi shirikishi wa mazao ya misitu (USMJ) ikiwamo sera mtambuka za Wizara ya Maliasili na Utalii zinazohamasisha uhifadhi wa misitu wakati kilimo kinahamasisha wakulima kupanua mashamba kwa ajili ya kilimo endelevu.Aidha, ni vyema wanajamii wakahamasishwa kujitokeza kupata elimu ya ufugaji nyuki na kupata mizinga bure kwa sababu ufugaji wa nyuki una tija zaidi tena kubwa tofauti na ufugaji unaoweza kukaa na wanyama kwa miongo kadhaa lakini bila faida ya muda mfupi, lakini kwa kuvuna asali kila baada ya miezi mitatu au sita kwa mwaka na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi wakati wanyama hawana mavuno hayo. 

Ofisa wa TFS mhifadhi mwandamizi wa Manispaa na Wilaya ya Morogoro, Faustine Msokwa, anasema hamasa ya ufugaji nyuki katika wilaya ya Morogoro imekuwa ndogo kutokana na ukosefu wa elimu na kwamba TFS ipo tayari kumsaidia mtu mmoja mmoja au kikundi kielimu na mizinga bure iwapo atajitokeza ili aweze kufuga nyuki na kuhifadhi mazingira.

Hilo ni suala ambalo linapaswa kusambazwa kwa mikoa na maeneo mengi watu wanapong’ang’ania ufugaji kuachana na  kufuga wanyama kwa wingi na badala yake wajikite kwenye kuzalisha asali ambayo ina faida na ni rafiki wa mazingira na pia ni muhimu kwa afya ya binadamu na pia ni tiba.