Kilichosaidia kidogo na kutuliza hali ya hewa Simba ili kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Red Arrows ya Zambia na ikaenda hadi hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, kabla ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Hiki ndicho angalau kilichowafanya mashabiki wa Simba watulie. Uchunguzi wangu mdogo umeonyesha kwa miaka ya karibuni, baada ya timu hiyo kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa, wanachama na mashabiki wa Simba hufurahia zaidi timu yao kuwa kwenye hatua za makundi za michuano ya kimataifa kuliko hata ligi ya Tanzania.
Wanaona huko ndiko wanakostahili, na ndiyo maana wanapotolewa mapema kwenye michuano hiyo kama ilivyokuwa dhidi ya UD Songo ya Msumbiji miaka kadhaa iliyopita, wanasikitika sana na uongozi unakuwa uko lawamani.
Wanaona timu yao imeshakuwa kubwa ya kushindana kwenye mechi za kimataifa zaidi.
Baada ya kukosa kila kitu na kuishia hatua hiyo, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo walitoa maoni kuwa baadhi ya wachezaji hawastahili tena kuichezea timu yao.
Wakasema ni kweli wameifanyia mema na makubwa, lakini kwa sasa hawana tena uwezo huo, hivyo wanahitaji wachezaji wengine wenye uwezo, vijana na wenye kuipambania timu.
Wakasema wapo wachezaji ambao wana umri mkubwa, hivyo hawawezi tena kuleta kitu kipya.
Kuna wachezaji ambao wameshapata mataji na mafanikio, hivyo wanaona ni kitu cha kawaida. Hawafanyi tena jitihada, hivyo wanatakiwa wachezaji wengine ambao watakuja kusaka sifa zao binafsi huku ikitaka kutwaa mataji wakiwa na klabu yao.
Wanachama na mashabiki wa Simba wakawataja majina wachezaji ambao hawapaswi kuwamo kwenye klabu.
Inawezekana ni uzito wa viongozi wao, au kwa kuona labda wachezaji wanaotajwa kuwa waondoke bado wana mikataba, waliamua kuondoka nao na kwenda nchini Misri kwenye kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Kuondoka kwao tu kulizua manung'uniko kwa baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wakisema pamoja na kwamba wamesajili baadhi ya wachezaji wapya, lakini haikutakiwa tena kuwa na wachezaji hao.
Viongozi wakaja na kauli kuwa wanamwachia Kocha Mkuu Zoran Maki ili kuangalia nani anamhitaji na nani hamhitaji.
Kama ilikuwa ni kuogopa kuvunja mikataba, kuogopa lawama, kocha amekuja na kile kile ambacho wanachama na mashabiki wa Simba walikuwa wanakisema na kukihitaji.
Tayari kocha ameshatamka kuwa hahitaji kuwa na wachezaji Thadeo Lwanga raia wa Uganda, Meddie Kagere, Mnyarwanda na Mkongomani Chris Mugalu.
Unaweza ukadhani kuwa kocha huyo ambaye yuko nchini Misri alikaa kikao na mashabiki wa Simba Dar na kumweleza. Nao baadhi ya wachezaji waliotaka waondoke ni hao hao.
Tayari kuna taarifa kuwa straika mwingine wa Simba John Bocco yuko kwenye uangalizi, naye panga laweza kumpitia.
Pia taarifa kutoka jijini Ismailia iliko kambi ya timu hiyo ni kwamba kuna wachezaji wengine watatu ambao kocha haridhishwi nao na amewaweka mategoni, hivyo chochote kinaweza kutokea.
Hili ndilo viongozi wa Simba walilishindwa kulifanya tangu mwanzo. Hata hivyo wasilaumiwe sana kwa sababu walitaka kumpa uhuru kocha aamue.
Sasa kama ameamua na atazidi kuamua, viongozi wa klabu hiyo wanapaswa kukubali matakwa yake hata kama yatawagharibu kuvunja kibubu kwa sababu ndivyo walivyohitaji.
Kama si hivyo wangefanya hivyo wao mapema. Yoyote atakayemwona hafai, basi aondolewe bila kumwangalia aibu mtu asoni, na atakayetaka asajiliwe au nafasi zinazotakiwa kusajiliwa basi apatiwe haraka.
Inawezekana kwa sasa hatoeleweka kwa baadhi ya watu, lakini kocha huyo anaweza kuwa ni msingi mzuri wa Simba kurudi kwenye makali yake yaliyozoeleka kwa kusajili wachezaji wenye uwezo na ubora mkubwa wa kuipambania timu, badala ya baadhi ya wachezaji wanaocheza 'kifaza', kimazoea, na walioshuka viwango.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







