Wakuu wapya walioapa  tumikieni si kujikweza

03Aug 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wakuu wapya walioapa  tumikieni si kujikweza

KWA mara nyingine Rais Samia Suluhu ameteua na kuapisha wasaidizi wake kwa ajili ya kuiongoza mikoa, akiwaondoa baadhi yao na wengine kuhamishwa na pia wamo waliobakizwa katika vituo vyao vya kazi.

Katika uteuzi wa viongozi mbalimbali amewahi kusisitiza jambo moja kuwa anataka wafanye kazi kwa ushirikiano na kutoa onyo kuwa hatasita kumwondoa kiongozi yeyote ambaye atainua mabega.

Anawakumbusha kuwa asiwepo kiongozi wa kwenda kinyume na kuanza kuinua mabega yake au kufanya anavyotaka, bali kuwatumikia wananchi katika eneo lake la kazi, ili kuharakisha maendeleo.

Hapa inawezekana anawasisitizia kutambua kuwa cheo ni dhamana, uongozi ni utumishi, hivyo kiongozi asidhani cheo ni matokeo ya jitihada zake binafsi, akiamini anaweza kufanya lolote analotaka.

Kwa mantiki hiyo, si vibaya wakuu wapya wa mikoa walioteuliwa na kuapishwa juzi, wakiwamo waliohamishwa vituo vya kazi, wakazingatia maelekezo hayo ya mkuu wa nchi, ili walete matokeo chanya ya maendeleo katika maeneo yao ya utawala.

Labda nikumbushe kauli ya mwanasiasa aliyewahi kusema cheo ni sawa na koti la kuazima ambalo mtu unakuwa na mbwembwe akiwa amelivaa, lakini siku koti hilo linapochukuliwa, mtu anakosa mahali pa kuficha uso wake.

Kutokana na msemo huo, akawataka viongozi vijana kuelewa kuwa madaraka au vyeo walivyobeba ni kama koti la kuazima na kwamba ipo siku hawatakuwa navyo. Hivyo wawatumikie wananchi.

Anatoa  ushauri huo, kutokana na kile alichodai kuwa ameona baadhi ya nyadhifa au vyeo baadhi vya watu wanavichukulia kwa namna wanavyopenda na kutunisha misuli kuwa ni wakubwa.

Ninaamini kwa mfano huo na kile Rais amekuwa akihimiza kwa wataule wake, wanakwenda kutekeleza wajibu wao kikamilifu huku wakikumbuka ahadi za mwanachama hasa ya tano inayokumbusha kuwa 'cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu'.

Kimsingi, kiongozi anayezingatia ahadi hiyo, hawezi kujiinua atakumbuka kuwa cheo ni sawa na koti la kuazima ambalo wakati wowote mwenye nalo anaweza kulichukua.

Aidha, iwapo kiongozi atazingatia ahadi hiyo, atafanya kazi akigusa hata ile ya pili ambayo inamwelekeza kuitumikia nchi na watu wake wote' ili kuharakisha maendeleo.

Sasa kwa kuwa Rais alishasema kiongozi atakayekuwa anafanya apendavyo ataondolewa kwenye nafasi yake, basi ni vyema kila aliyeteuliwa, afanyie kazi ujumbe huo ili 'asisaidiwe kazi' au kutumbuliwa.

Ninaamini kiongozi akitimiza wajibu wake inavyopasa hakutakuwa na mtindo wa kujitwalia madaraka mikononi awapo kwenye kituo chake cha kazi, kwani hatua hiyo inaweza kuwa sawa na kuinua mabega.

Ikumbukwe, kuna wakati baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa waliwahi kusababisha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa (TAMISEMI), Selemani Jafo, kuingilia kati na kukemea mtindo huo wa kutumia vibaya madaraka kwa kuwaweka watu ndani.

Akafafanua kuwa, Sheria ya TAMISEMI ya Mwaka 1997, Kifungu cha 15 (1) inawapa mamlaka wakuu wa wilaya na mikoa kutoa amri  mtu kukamatwa na kuwekwa ndani saa 48 anapobainika mhusika ametenda kosa fulani.

Lakini, akatoa somo kwamba, tabia ya kuweka watu ndani ovyo, inasababisha wananchi waichukie serikali na kuwaagiza wakuu hao kuitumia sheria hiyo kama ilivyokusudiwa na si kwa kuonea watu.

Viongozi wasisubiri mpaka Rais au Waziri Mkuu atembelee eneo lao ndipo washtakiwe kwa mabango kuwa wameshindwa kumaliza kero za wananchi badala yake wajitume na kuwafikia wananchi na kushirikiana nao ili kuwaletea maendeleo.