Ulinzi wa mazingira uwe ajenda namba moja

27Oct 2022
Christina Haule
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ulinzi wa mazingira uwe ajenda namba moja

WATANZANIA wanalazimika kutambua wajibu wao wa kutunza na kuyahifadhi mazingira na kuachana na fikra kuwa ni jukumu la serikali na viongozi pekee yao. Wafahamu kuwa ni kazi ya wote ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayomtikisa kila mmoja.

uharibifu wa mazingira unapunguza maji ambayo ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu na yamekuwa tegemeo kubwa kwenye uzalishaji malighafi viwandani na ni kitu muhimu kwa uchumi wa nchi kuanzia shambani, nyumbani, hospitalini, vyuoni, shuleni hadi viwandani. Uchumi wa nchi unategemea maji, chakula pia kinategemea maji, ndiyo unaofua umeme, unaotumika viwandani na nyumbani, ujenzi unayategemea na vitu vyote hivyo ni muhimu jukumu kubwa likibakia kulinda maji na vyanzo vyake. Aidha, maji yakikosekana umeme unasumbua ukikosekana uzalishaji unayumba na kuyumbisha uchumi utakaoshuka na hakuna atakayekuwa na muda wakusikiliza siasa wala habari za vyama ikiwa uchumi unayumba na kukwamisha maendeleo, hivyo ulinzi wa mazingira ni kuanzia sasa uwe ajenda namba moja. Ni wajibu wa serikali zote kuu na mitaa kuendelea kuipa kipaumbele agenda ya mazingira kwa sababu ni mhimili wa unaotegemewa na watu, mifugo, kilimo na umeme na kwamba hivi karibuni zipo sehemu wafugaji wamelia kwa kupoteza mifugo kwa sababu ya ukame.

Juhudi ziende pamoja na kutoa elimu kwa umma kuwachukulia hatua wanaofanya uchafuzi wa mazingira hasa wanaoendesha kilimo kando ya maji, kulisha mifugo chini ya madaraja kwani kwa kuwapa elimu maeneo hayo yatakuwa salama zaidi kwa sababu ndiyo wakazi na walinzi wa rasilimali kuanzia maji, misitu na uoto wa asili. Aidha, wadau wa mazingira kama viwanda vya maji au juisi wanapaswa kujua kuwa wana jukumu zito la kuhifadhi mazingira kwa sababu chupa za plastiki zinazotokana na bidhaa zao ni nyingi tena zinazagaa mitaani hivyo ni lazima wakae na serikali ili kuona namna watakavyochangia kudhibiti uchafuzi huo.

Kama ambavyo mratibu wa kikundi kazi cha misitu Tanzania (TFWG) Casian Sianga, anavyosisitiza kuwa kuhifadhi mazingira na mimea pamoja na viumbe vilivyoko ndiyo roho za watu na ni jukumu la kila mmoja kuyalinda na kuyaendeleza. Kwa kauli yake jamii inapaswa kuelewa na kuzingatia utekelezaji wa sheria za mazingira zilizoko kwa sababu licha ya kuwa na sheria bora lakini utekelezaji na usimamizi wake umekuwa tatizo na hauonekani. Kwa mfano Sheria za Mazingira za Tanzania na nyingine ndogo za halmashauri ziendelee kusimamiwa kwa kupiga faini wanaoharibu misitu, vyanzo vya maji, kulisha mifugo barabarani na kuchoma mashamba na mapori. Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika jijini Dodoma ilikuwa na kauli mbiu “Tanzania ni moja tu, tunza mazingira”.