Vyoo vichafu sokoni chanzo cha magonjwa

28Oct 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Vyoo vichafu sokoni chanzo cha magonjwa

UKIPATA bahati ya kuingia kwenye vyoo katika vituo cha mabasi ya daladala na hata vya kusafiri mikoani na nje ya nchi, halafu ukaenda kuingia kwenye vyoo vya masoko utakutana na vitu viwili tofauti.

Cha ajabu ni kwamba vyoo hivyo vyote vinamilikiwa na Manispaa. Yenyewe hutoa tenda kwa kampuni za usafi kwa ajili ya kutunza na kusafisha.

Hata hivyo, utakachokiona kwenye vyoo vya masoko mengi nchini, si kile utakachokiona kwenye vyoo vya kwenye vituo vya mabasi.

Tukianza kwenye vituo vya mabasi, kwanza utakuta hata viwango vya utengenezaji ni tofauti. Ukiingia mara nyingi ni visafi na eneo karibuni lote ni kavu.

Utakutana na maji yakitiririka kwenye mabomba na hata kama siku hiyo hakuna maji utaona majaba yakiwa yamejazwa maji.

Ukiingia unapokewa na harufu ya dawa za kusafisha vyoo si harufu zisizoeleweka, ili mradi tu hata ukitoa pesa yako unaona kabisa kutokana na huduma iliyotolewa pesa zinakwenda kihalali.

Unatoka chooni hata kama ulikuwa unataka kwenda hotelini kula chakula, wala hupati shida kwa sababu mtu anakuwa hajachefukwa kutokana na mazingira aliyoyakuta ndani.

Naweza kusema kuwa asilimia 90 ya vyoo vilivyoko kwenye vituo vya mabasi, watunzaji au wabia wanaonekana kujitahidi sana.

Ni kwa sababu mtu anaweza kukutana na mwezake anayefahamiana naye wakasimama na kupiga stori hata dakika mbili tatu humo humo chooni kabla ya kutoka nje.

Shughuli ipo kwenye vyoo vya masoko. Hapa ndipo kwenye matatizo. Vyote vinamilikiwa na Manispaa, lakini huku ni kama vile wanaopewa tenda ya kuvilinda, kuvitunza kuvisafisha na kuviendesha, hawana utaalamu huo, na wanaviendesha kienyeji ili mradi tu.

Vyoo vya masoko mengi nchini ni vichafu na vimekuwa ni vyanzo vya magonjwa mengi ya kuambukiza. Magonjwa ya tumbo, kuhara na kipindupindu ukiangalia mara nyingi huanzia masokoni na hii inatokana na ubora hafifu wa vyoo.

Mara nyingi vyoo vya masoko mara zote utakuta vina unyevunyevu, ambao unatokana na uchafu wenyewe wa choo na hata wanaoviendesha na waliowaweka kusimamia kutojua wakati gani wa kusafisha na wakati gani wa kuwaacha watu wavitumie kwanza.

Muda wote utakuta wanamwagilia maji, kwa hiyo mtu anaingia mlangoni kuna sakafu imeloa hadi anapokwenda kujisaidia.

Usafi siyo kusafisha muda wa watu kuvitumia. Muda huo watumiaji wanatakiwa kuvikuta vyoo vikiwa vikavu, kinachotakiwa ni maelekezo tu kwa watumiaji jinsi ya kutumia kwenye haja kubwa, ndogo na jinsi ya kunawa baada ya kutumia.

Sisemi vikisafishwa asubuhi basi visisafishwe tena, la hasha, ila usafi uwe unafanyika kwa mpangilio kama inavyokuwa kwenye vituo vya mabasi.

Kwenye vyoo vya masoko hata miundombinu yake inakuwa ni tatizo. Unaweza kukuta hata koki zote hazifanyi kazi, badala yake kuna makopo mawili au matatu tu ambayo watu wote wanalazimika kuyatumia kitu ambacho ni hatari sana kiafya.

Sehemu ambayo wanaume wanapanda kwa ajili ya haja ndogo unakuta marumaru zimechoka mpaka zimebadilika rangi.

Pembeni ambako haja ndogo inamwagika, marumaru za ukutani zimebadilika rangi kiasi cha kutia mtu kichefuchefu.

Huko kwenye vyoo vya kinamama ndiyo kabisa, kiasi cha kuwafanya kuwapa magonjwa ya maambukizi ya mkoja au UTI. Unashangaa ni kwa nini vyoo vinakuwa vichafu wakati watu wanalipia?

Watu wote waliokusanyika kwenye soko hilo, ambao ni wafanyabiashara na wateja wao wanalipia huduma na hata wapita njia nao wanatumia, lakini unakuta watu waliopewa dhamana hiyo wanashindwa kufanya vyoo vya masoko kuwa salama kwa afya ya binadamu.

Ninavyojua miundombinu au vifaa vya vyoo havinunuliwi kila siku. Marumaru, koki za maji, taa, fagio, mabomba na vifaa vingine vinavyofanana na hivyo vikishanunuliwa huweza kukaa muda mrefu bila kununua, labda dawa za kuua wadudu na kukata harufu mbaya ndiyo zinawaza kununuliwa labda kila baada ya siku tatu, nne tano au wiki.

Kwa hili nawashauri baadhi ya Mwenyeviti wa Serikali za Mitaa, viongozi wa masoko kubadilisha mitazamo yao na kujali sana usafi wa vyoo kwani ndiko sehemu ambazo watu kutoka sehemu mbalimbali wanakutana.

Unapotokea ugonjwa wa kuambukiza sehemu kama hiyo, basi wanaweza kusambaza na kusababisha jiji au mkoa mzima kupatwa magonjwa ya tumbo na kuanza kushughulisha serikali kwa tatizo ambalo wangeweza kulizuia mapema.