Tena vina majukumu mengi ikiwamo kuelimisha, kushawishi watu kushiriki michakato ya kisiasa, kutafuta wanachama pia kuandaa viongozi wa kila wakati.Kwa mantiki hiyo, ili viweze kufanikiwa katika shughuli hizo, havina budi kujipanga kama taasisi, hasa kuanzia ngazi za msingi, kwani huko ndiko kwenye ushawishi mkubwa wa wanachama lakini kuwa na safu imara inayoviongoza.Kwa Tanzania vyama viko katika muundo wa kuanzia ngazi ya mashina hadi taifa, ambapo tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, baadhi yake vimeendelea kuimarika na kusonga mbele.Vyama ambavyo viko imara vimekuwa vikifanya uchaguzi wa viongozi wake kila muhula wa uchaguzi unapowadiwa ambapo uchaguzi huo huanzia ngazi ya chini hadi taifa ukihusisha pia jumuiya za vyama husika.CCM ni miongoni mwa vyama hivyo, ambapo kwa sasa kinaendelea na uchaguzi wa viongozi wake kikiwa kinaelekea kwenye ngazi ya mkoa, huku kukidaiwa kuwa na 'figisu', katika baadhi ya uchaguzi.'Figisu' hizo zinathibitishwa na Katibu Mkuu CCM, Daniel Changolo, akisema kwamba moja ya shida zinazowakabili ni kuwapo baadhi ya wanachama ndani ya chama hicho wanaotengeneza anachokiita miundombinu haramu ya kuwadhibiti watu wazuri kupata nafasi za uongozi.Akiwa wilayani Kigamboni, anasema chama kina watu wazuri na bora wenye nia njema, ila wanatengenezewa mazingira ya kuwakosesha dhamana na kwamba kutokana na hilo, anatoa angalizo wanachama kuacha mara moja vitendo hivyo, na kwamba kwa idadi ya mikoa 32 iliyopo ni michache, ambayo chama kitapitia kila jina katika orodha ya walioomba kuchaguliwa.Lengo la kufanya hivyo kwa mujibu wa maelezo yake ni kutazama maelezo binafsi na mengine na kujiridhisha kwa kila mtu, ili kupata viongozi ambao wanafanana na mazingira na wana dhamira ya kweli ya kuendeleza utumishi na uhai wa chama hicho.Kiongozi huyo anafunguka kwamba, chama hicho kinataka viongozi bora na siyo bora viongozi, na kubainisha kuwa mwaka 2025 makada hawatachaguliwa kwa sababu wana sare nzuri ya chama.Badala yake watachaguliwa kutokana na jinsi watakavyofanya kazi kwa kiwango chenye tija na kutatua shida za wananchi, na kwamba kila mtu achaguliwe kwa kuomba ridhaa mwenyewe na hakuna mtu anayefuatwanyumbani achukue fomu ya kugombea.Ingekuwa vyema kama makada wa CCM wangechukua hatua tangu zilipotokea figisu katika uchaguzi wa ngazi ya chini ambao kiongozi huyo aliamuru fomu zigawiwe upya kwenye baadhi ya maeneo.Hatua hizo zilichukuliwa baada ya kubainika kuwapo kwa fitina na mazingira ya kuwanyima fomu za kuwania uongozi baadhi ya makada waliojitokeza kusaka uongozi na kusababisha malalamiko.Mambo hayo yasingekuwa sehemu ya chama, kwani yanasababisha makada wenye uwezo wa kuongoza wakate tama, hali inayochangia kuchaguliwa wale wasio na sifa za kuongoza chama, badala yake wanakuwa na malengo binafsi.Chongolo pia, analia na rushwa ndani ya chama hicho, na kwamba katika ngazi ya wilaya, walibaini baadhi ya watu kufanya rafu na kukiuka taratibu katika uchaguzi na kusababisha kufutwa kwa uchaguzi kwenye wilaya 21.Kutokana na mazingira hayo, anabainisha kuwa macho yao yanatazama mchakato kwa karibu na hawatasita kuchukua hatua popote watakapoona kuna jambo lisilokuwa na heri kwenye chama hicho.Ni jukumu la makada kuzingatia maelekezo ya viongozi wa chama, kwani uongozi unatumia muda mwingi kuimarisha chama, lakini wanajitokeza watu wanaotaka nafasi za uongozi kwa njia zisizo halali na kukwamisha jukumu hilo.
Figisu hizi zitakwamisha kupata viongozi mahiri
26Oct 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Figisu hizi zitakwamisha kupata viongozi mahiri

VYAMA vya siasa ni nguzo muhimu katika ujenzi wa demokrasia ya uwakilishi.


.jpg?itok=nfwjwDzv)






