Ni siku muhimu kwa Watanzania na hasa wapenda amani na demokrasia, haki, usawa na wale wote tunaoheshimu haki za binadamu na wanaochukia ubaguzi wa kila aina. Oktoba 14 ya kila mwaka viongozi, mbalimbali wakiwamo wa serikali, dini na siasa, wamekuwa wakihimiza umuhimu wa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo ili kuendelea kuifanya nchi hii kuwa ya amani.
Hatua hii inatokana na ukweli kwamba, Baba wa Taifa aliheshimika katika ulimwengu na leo Tanzania inaitwa ‘Kisiwa cha Amani’ kutokana na jinsi yeye na wenzake walivyopambana na kila ya aina ya vitendo vinavyohatarisha amani.
Baba wa Taifa, alichukia ubaguzi, hivyo wanasiasa, wasomi, wananchi kwa jumla hawana budi kuweka kando tofauti zao za kiitikadi kwa kushiriki kila jambo linalohusu maendeleo ya nchi hii.
Haya na mengine mengi, ambayo ni muhimu yakifanyika kwa vitendo, itakuwa ni kumuenzi kiongozi wetu huyo shupavu. Nakumbuka hata aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, aliwahi kuwataja wanasiasa kuwa miongoni mwa watu wanaomsaliti Baba wa Taifa! Akasema kuwa, waliingiza kwenye Katiba, mambo yanayokinzana na makubaliano ya Muungano.
Kwa mfano, suala la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuondoa mamlaka ya Bunge la Muungano katika utungaji wa sheria na kuongeza mambo ya Muungano bila kufuata Katiba.
Aliwahi kukaririwa akisema hayo katika kipindi cha Dakika 45 cha Televisheni cha ITV na kukanusha tuhuma zilizoelekezwa kwake kuwa, anamsaliti Baba wa Taifa na kufafanua kuwa viongozi wa pande mbili za Muungano ndio waliouvuruga Muungano huo “Sasa kati ya mimi na wao ni nani msaliti kwa Mwalimu, angekuwapo (Mwalimu) ni yupi angeonekana msaliti wa Serikali ya Muungano? Wao ndiyo wameuvuruga, alichokiacha Mwalimu ni tofauti na kinachoonekana kwa sasa,” alisema Jaji Warioba.
Alitoa kauli hiyo kujibu mwendelezo wa lugha za kejeli na matusi alizorushiwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na baadhi ya viongozi wa serikali baada ya tume aliyoiongoza kupendekeza muundo wa serikali tatu.
Kuna mengi aliyozungumza kiongozi huyo, ila cha msingi ni kwamba Watanzania wanapoadhimisha miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa, hawana budi kutambua mchango wake na kuuenzi kwa vitendo.
Wote hawana budi kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa kujitoa aliokuwa nao ili kuliwezesha taifa hili kupiga hatua zaidi kimaendeleo, badala ya kulumbana kwa sababu ya tofauti za kisiasa.
Kuna haja ya kujifunza baadhi ya mambo aliyokuwa akiyafanya Baba wa Taifa kama sio yote na hasa uwajibikaji, uzalendo, uadilifu na nidhamu katika kulitumikia taifa la Tanzania.
Baba wa Taifa, aliwakumbusha wanasiasa kuwa demokrasia sio wakati wa uchaguzi tu, bali ni pamoja na kuheshimu watu wengine bila kujali itikadi za vyama vyao.
Nakumbuka mwanzoni mwa mwaka 1995, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwalaimu alikemea vikali tabia ya ubaguzi na akasema kuwa Makaburu wa Tanzania ni wale wanaojiita wazawa.
Hata Rais John Magufuli katika hotuba zake mbalimbali, amekuwa akihimiza Watanzania kushirikiana bila kubaguana kwa itikadi za kidini, kikabila ama kikanda, kwa kuwa wote ni wamoja.
Hii inaonyesha kuwa kiongozi huyu wa nchi, anaonyesha njia kwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo, hivyo wengine wanatakiwa kufuata njia hiyo ambayo italifanya taifa hili liendelee kuwa la amani.
Alitaka pia kila Mtanzania anufaike na rasilimali za nchi na alikuwa tayari kupunguza msafara wa magari pale anapokuwa na safari za ndani na hata mara nyingine hakutaka ving’ora viwapo katika msafara wake, akisema ni usumbufu na kujenga hofu kwa wananchi.
Rais wa Awamu ya Tano, Dk. Magufuli naye amekuwa akihimiza suala la amani na kuwahimiza viongozi wa dini kuombea nchi amani.
Anafanya hivyo kwa kutambua kwamba, bila amani kila kitu kitaharibika na utakuwa ni mwisho wa taifa hili. Aidha amekuwa akitaka kila Mtanzania afaidike na keki ya taifa.
Kwa lugha nyingine, ninaweza kusema kuwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo ni kuenzi amani iliyopo sasa, ambayo imewafanya Watanzania kuendelea kuwa wamoja bila kujali tofauti zao za makabila, dini, vyama wala ukanda.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







