Aidha ukitaka kuona nguvu ya jamii inavyoweza kushinikiza hatua zichukuliwe mara moja kukomesha uhalifu, uovu, uonevu ama dhambi katika jamii, ni pale inapoungana na kushawishi mamlaka zinazohusika kuchukua hatua stahiki.
Hili linashuhudia na matukio mabaya mawili yaliyotokea nchini karibuni, na kuripotiwa na vyombo vya habari.
Ripoti ya vyombo vya habari, iliifanya jamii ya Kitanzania kutoka pande zote za nchi, kupiga kelele ikitaka mamlaka zichukue hatua dhidi ya matukio hayo.
Tukio la Kwanza lilitokea jijini Dar es Salaam, likimhusisha kijana Saidi Ally aliyevamiwa na kushambuliwa na mtu anayedaiwa kuwa ni Salimu Njwete, maarufu kama ‘Scorpion’ katika eneo la Buguruni.
Kijana Ally alishambuiliwa hadharani kwa visu, watu wakiangalia bila kufanya lolote, hatua ambayo iliathiri macho yake na kumuacha na kilema cha maisha, yaani upofu.
Mara baada ya taarifa hiyo kuifikia jamii kupitia vyombo vya habari, jamii iliungana pamoja na kulaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha kinyama alichotendewa binadamu, na binadamu mwenzake.
Juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika suala hili ziko kwenye rekodi, kwa kuwa alitumia mamlaka yake kuhakikisha mtu huyo anayedaiwa kufanya shambulizi hilo, anakamatwa na hivi sasa amefikishwa mahakamani.
Tukio la pili lililoonyesha kwamba jamii ya Watanzania ikiungana pamoja bila kujali tofauti zake inaweza ikabadili mambo, na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa, ni lile lililotokea jijini Mbeya.
Tukio hilo lilimhusisha mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mbeya, ambaye alishambuliwa na walimu wake wanne wanafunzi kwa fimbo, ngumi na mateke kwa sababu ya kutofanya kazi ya darasani aliyopewa na mwalimu wake.
Baada ya tukio hilo kuonyeshwa kupitia mitandao ya kijamii, tunaona namna jamii ilivyoamuka kwa nguvu na kushinikiza hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya walimu hao wanafunzi waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo.
Na kweli serikali kwa maana ya mamlaka, zilichukua hatua mara moja.
Nimeamua kuanza na mifano hiyo, ili kuonyesha namna jamii inapoungana pamoja inavyoweza kupambana na uovu na hata kushawishi ama kuishinikiza serikali, kuchukua hatua kwa ustawi wa jamii yenyewe, lakini pia taifa kwa ujumla wake.
Sasa kuna uovu, kuna dhambi, kuna uhalifu mkubwa unaoendelea kutokea kila siku nchini dhidi ya watoto wetu wa kike, ambao dunia ilisherehekea siku yao jana, kwa maana jana ilikuwa ni maalumu kwa ajili yao.
Uhalifu ninaoujadili hapa ni ule wa ndoa za utotoni, unaoambatana na mimba za utotoni, ambao kimsingi umekosesha haki ya kupata elimu kwa mtoto wa kike, karibu katika maeneo yote ya nchi, huku tukiwa na mikoa mitatu ambayo ni vinara wa uhalifu huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) mwaka 2010, mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni ya Shinyanga, asilimia 59, Tabora asilimia 58 na Mara asilimia 55.
Lakini utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), ulionyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/13, jumla ya matukio 228 ya mimba za utotoni na matukio 42 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa.
Aidha, tukizichukua takwimu za iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 3,045 wa shule za sekondari na za msingi nchini, waliacha shule kwa sababu ya mimba kwa mwaka huo wa 2013.
Sasa wakati dunia ilisherehekea Siku ya Mtoto wa Kike jana, pengine ni siku ya jamii ya Kitanzania, kuamua sasa kuungana kwa pamoja dhidi ya janga hili kubwa.
Janga lenye madhara makubwa kwa watoto wetu, kwa kuwa ukiacha yale ya kisaikolojia, kuna yale ya kiafya ambayo ni pamoja na maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Lakini pia ndoa na mimba za utotoni ni uovu, ni janga linalozima moja kwa moja ndoto za mtoto wa kike kufikia malengo yake ya kimaisha, na hivyo kumnyima fursa ya kutoa mchango wenye tija kwa ustawi wake, jamii na taifa kwa ujumla.
Ni kwa hali hiyo, ndipo ninapoiasa jamii kunyanyuka na kuungana pamoja kwa nguvu ileile, kama iliyoonyeshwa kwenye matukio ya kushambuliwa kwa Ally na ‘Scorpion’, na kwa lile la mwanafunzi aliyeshambuliwa na walimu wake.
Kwamba jamii ikaitumia nguvu ileile kupambana na ndoa na mimba za utotoni, ili kulitokomeza janga hilo kwa ustawi mtoto wa kike.
Ni vizuri sasa jamii tujitokeze kusaidiana na serikali kwa hili, kwa kuzikataa mila potofu na sababu zozote zinazofumbia macho uovu huu, kwa kuwa katika mezania yoyote ile, una madhara makubwa pengine kuliko maovu tunayoyavalia njuga kama jamii.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








