Faini hazisaidii kumaliza makosa barabarani

12Oct 2016
Richard Makore
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Faini hazisaidii kumaliza makosa barabarani

ELIMU ya matumizi bora ya barabara inahitajika zaidi kuliko faini ambazo zimekuwa zikitolewa na askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Kama elimu na busara ya kawaida ikitumika itasaidia kuwaelimisha wananchi wanaotumia vyombo vya moto yakiwamo magari, bajaji na pikipiki.

Lakini kwa bahati mbaya hakuna mtu anayefikiria suala la utoaji wa elimu kuhusu sheria na taratibu za usalama barabarani, badala yake askari wa kikosi cha usalama barabarani wamejikita kukamata madereva wanaovunja sheria na kuwalipisha faini.

Kwa mfano dereva anakutwa anaendesha gari huku hajafunga mkanda, askari bila kumsikiliza kwa nini hali imetokea anamwandikia kulipa faini ya Sh. 30,000.

Katika hali ya kawaida askari angeweza kumkamata na kumuweka pembeni na kumkumbusha umuhimu wa kuendesha gari, akiwa umefunga mkanda na kumweleza kwamba kuendesha gari bila kufunga mkanda ni hatari kwa maisha yake.

Hapa simaanishi kwamba watu wavunje sheria, lakini pia busara za kawaida zinaweza kutumika na kumnusuru mtu kulipishwa faini ya Sh. 30,000.

Kwa namna ambavyo askari wa usalama barabarani walivyojipanga kuanzia asubuhi na kuwalipisha faini madereva mbalimbali, nadhani hilo lingetakiwa kwenda sambamba na utoaji elimu.

Nasema hivyo kwa sababu huenda kuna baadhi ya madereva wamepewa leseni bila kusomea wala kujifunza sheria za barabarani, na hawa watu wanajikuta wakiendelea kutenda makosa bila wao kujua kama wanakosea.

Faini lazima iwe adhabu mbadala, baada ya mambo yote kushindikana hata ikiwezekana itolewe na mahakama baada ya mtuhumiwa kufikishwa huko, badala ya sasa askari kutanda barabarani na kuwalipisha madereva kutokana na makosa mengine ambayo yangeweza kuepukika kupitia elimu ndogo ya usalama barabarani.

Wiki iliyopita katika jiji la Dar es Salaam, tumeambiwa mapato yatokanayo na faini za barabarani kwa siku saba ni zaidi ya Sh. milioni 400.

Hili siyo jambo la kufanyia mzaha, kwa kuwa tafsiri nyingine ni kwamba askari wamedhamiria kukusanya mapato na siyo kusimamia sheria za barabarani ndiyo maana waliweza kukusanya kiasi kikubwa cha fedha, kwa muda wa siku saba.

Kwa maoni yangu, siyo lazima dereva alipe faini kwa sababu askari anaweza kumpa elimu kuhusu matumizi bora ya barabara, na ikamsaidie kutorudia kosa lake siku nyingine.

Ni kweli kwamba fedha nyingi kwa sasa zinakusanywa na askari wa kikosi cha usalama barabarani, lakini bado madereva tunaona wanazidi kufanya makosa.

Kwa lugha nyingine ni kwamba faini siyo njia nzuri ya kukomesha vitendo vya uvunjifu wa sheria za barabarani, jambo ambalo linadhihirisha kauli yangu.

Wiki ya usalama barabarani, shughuli muhimu zingetakiwa kuwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa madereva wanaoendesha vyombo vya moto.

Kwa kweli wengi wa madereva wamepewa leseni ya kuendesha vyombo vya moto, lakini mbona kila siku wanaonekana kuvunja sheria za barabarani?

Majibu ya swali hilo ni kwamba, huenda bado wanahitaji kusaidiwa zaidi kwa kupewa elimu badala ya kuwakamata na kuwalipisha faini kisha kuwaachia.

Leo ukimkamata dereva aliyepita njia isiyoruhusiwa halafu ukamlipisha faini na kumuachia, utakuwa hujamsaidia na huenda kesho atarudia kosa hilo.

Askari wa usalama barabarani wajikite zaidi kutoa elimu kwa madereva badala ya kuendelea kuwatoza fedha hata kwa makosa madogo ambayo yanahitaji kuelimishwa.

Ingawa mara nyingi ili kumpatia mtu leseni ya kuendesha chombo cha moto ni lazima walau ajue sheria za barabarani, lakini naona mpango huo bado umeshindwa kuwasaidia ili kuachana na uvunjaji wa sheria za usalama barabarani.

Lakini pia askari wawe tayari kuwasikiliza madereva wanapowakamata barabarani badala ya kujikita kutafuta makosa ya gari ama chombo cha moto walichokamata.

Kwa mfano, askari anakamata dereva anamwambia piga honi, dereva anamwambia nilivyoruka pale kwenye tuta umeme umekata ndiyo maana honi haipigi, lakini bado hawezi kusikilizwa na anaandikiwa kulipa faini.

Huyu mtu ukishamwandikia faini akailipa na kumuachia hautakuwa umepata ufumbuzi wa tatizo, badala yake umechukua fedha zake na kumuacha aendelee kutenda makosa.

Bila kutolewa elimu ya kutosha hizi faini zitaendelea kulipishwa, lakini makosa yatazidi kuongezeka barabarani.

Hili jambo linahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha kila mmoja anapokuwa barabarani anakuwa huru huku akifuata sheria, lakini pia haogopi kulipishwa faini isiyokuwa ya lazima.

Kwa pamoja tunaweza kupiga hatua na kuhakikisha kila mmoja anatii sheria bila shuruti, lakini pia askari nao wajitahidi kujikita kusimamia sheria na kutoa elimu badala ya kujigeuza TRA.