Kwamba, kwa mfano ukiangalia idadi ya vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kwa kila wajawazito 100,000, unaweza ukapata jibu la moja kwa moja kama taifa lolote lile linaendelea ama la.
Kwamba kama kuna zaidi ya kinamama 200 kwa mfano wanaopoteza maisha wakati wa kujifungua, ni ishara wazi kuwa, nchi bado haijapiga hatua za kuonekana kimaendeleo.
Vivyo hivyo, unapokuta na idadi ya vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua iko chini ya 100, kwa kila wajawazito 100,000, ni dalili za wazi kuwa nchi inachanja mbuga kimaendeleo.
Si kwa upande wa vifo vya akina mama wajawazito tu wakati wa kujifungua kama kipimo pekee, bali hata kwa kuangalia idadi ya vifo vya watoto hai waliozaliwa chini ya umri wa miaka mitano, unaweza ukapata picha yenyewe.
Kwamba ukikuta kuna vifo vya watoto 200 na kuendelea kati ya watoto 100,000, chini ya umri wa miaka mitano, ni ishara wazi kuwa taifa hilo linatakiwa kufanya kazi kubwa, kwa ustawi wa wananchi wake.
Na kinyume chake, pale unapokuta kuna vifo chini ya 100 vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kati ya watoto 100,000, ni kipimo tosha kuwa nchi inasonga mbele.
Kwa maana nyingine, huhitaji mwanasiasa asimame barabarani, ama kwenye mikutano ya hadhara kutangaza kwamba taifa lake linaendelea.
Ni kuangalia maeneo fulani fulani tu kama kipimo, na mojawapo ya maeneo hayo ni hilo la afya.
Muungwana amevutika kuzungumzia suala la afya ya akina mama wajawazito kwa sababu ya kilichoripotiwa mwishoni mwa wiki iliyopita, juu ya namna wajawazito wanavyotozwa fedha kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Na kutokana na hatua ya kutozwa fedha, iliritopitwa kwamba, kuna baadhi ya akina mama ambao hufikia hatua ya kutekeleza vichanga vyao, wakikimbia madeni.
Ilisemekana, hospitali hiyo ya taifa ilitoa tangazo likifafanua juu ya hatua yake ya kuwatoza fedha wajawazito.
Kwamba imelazimika kuanzisha utaratibu wa kuwataka wajawazito kuchangia kupitia mpango maalumu uitwao ‘Drugs Revolving Fund’.
Walisema lengo lao ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za upungufu wa dawa na vifaa tiba.
Hata hivyo, wakati hatua hiyo ya kuwatoza malipo akinamama wajawazito wanaoenda kupatiwa huduma za uzazi kutoka katika hospitali hiyo kubwa na tegemeo nchini, Sera ya Afya iliyopitiwa mwaka 2007, inataka wajawazito wasitozwe fedha kwa ajili ya huduma za uzazi.
Inatamka kuwa ‘Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida, (i) na mashirika ya kimataifa, itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa wanawake wajawazito…’
Na hili la wanawake wajawazito kupatiwa huduma za uzazi bila malipo, limekuwa likisistizwa siku zote na serikali, kupitia kwa watendaji wake akiwamo Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu.
Lakini tofauti na sera hiyo, ripoti ikaeleza kuwa katika hospitali hiyo wastani wa gharama za mzazi kujifungua kawaida ni Sh. 125,000, huku yule anayefanyiwa upasuaji akitozwa kuanzia Sh. 250,000, na kuwa gharama hizo huongezeka zaidi, kulingana na matatizo ya mgonjwa husika, wengine ikizidi Sh. 500,000.
Muungwana anaamini kuwa, mojawapo ya hatua zilizochangia mafanikio katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito, ni hiyo ya kulipatia kundi hilo, huduma za uzazi bila malipo.
Pamoja na kuwa, Waziri Mwalimu amenukuliwa akisema hana taarifa za kutozwa malipo akina mama wajawazito katika hospitali hiyo ya taifa, nadhani mkanganyiko bado upo, na hili la kutoza fedha wajawazito hospitalini, hapo huenda likawaogopesha akina mama.
Kwamba wajawazito wakaogopa kwenda kutibiwa Muhimbili hata kama kwa hali zao, inabidi wapelekwe hapo, kwa kuogopa kuzuiwa kutoka wakishapata huduma.
Ni rai ya Muungwana kwa serikali, kutoa tamko la kueleweka kuhusiana na hili, kwa sababu bado wajawazito wanadai kuendelea kutozwa fedha hospitalini hapo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








