Mfanyabiashara chagua Hati fungani za kununua

14Oct 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Mfanyabiashara chagua Hati fungani za kununua

KATIKA safu hii wiki iliyopita, tuliangalia eneo ambalo wafanyabiashara wa ngazi zote wanaweza kulitumia kwa malengo mawili kwa mpigo.

Kwamba wanaweza kulitumia kama sehemu ya kuweka akiba ya fedha wanazopata kutokana na shughuli zao za kibiashara kwa sababu ni eneo lililo salama.

Na pengine ni salama zaidi kuliko hata kuhifadhi fedha zao kwenye benki ambazo wakati mwingine hufilisika na kuleta adha kubwa kwao.

Tulilitaja eneo hilo kuwa ni la kwenye hati fungani za serikali, ambako serikali huuza dhamana zake kwa wananchi, wakiwamo wafanyabiashara.

Sasa mfanyabiashara anaponunua dhamana hizi za serikali ambazo ziko za aina mbili, yaani za muda mfupi na zile za muda mrefu, huwa kwanza ameweka akiba ya fedha zake hizo kwa kipindi chote kile hadi pale zitakapoiva.

Lakini faida ya pili ni kuwa anaponunua dhamana hizo za serikali, anakuwa amewekeza kiasi cha fedha alizotumia kwa manunuzi ya dhamana hizo na mwisho wa siku hupata riba ama faida kulingana na fedha alizowekeza.

Nimesema hapo juu kuwa eneo hili ni salama pengine kuliko hata kuweka fedha kwenye benki kutokana na ukweli kuwa, serikali haitarajiwi kushindwa kulipa wadai wake wakati dhamana zinapoiva.

Dhamana za serikali za muda mfupi (Treasury Bills) huiva baada ya siku kadhaa, kuanzia siku 35, 91,182 na siku 364.

Hivyo ni juu ya mfanyabiashara kuchagua awekeze fedha zake ama anunue dhamana za serikali za siku ngapi kati ya hizo.

Lakini kwenye dhamana za serikali za muda mrefu (Treasury Bonds), zenyewe huiva kuanzia kipindi cha miaka miwili, mitano, saba, 10 hadi 15.

Aidha kama ilivyo kwenye dhamana za serikali za muda mfupi, ni juu vilevile ya mfanyabiashara kuamua anunue dhamana za miaka mingapi kati ya iliyoanishwa hapo juu.

Sasa katika ununuzi wa hati fungani za serikali, hakuna kiwango cha mwisho cha uwekezaji ambacho mfanyabiashara amewekewa cha kununua dhamana za serikali, ziwe za muda mfupi ama zile za muda mrefu.

Lakini kuna kiwango cha chini kilichowekwa cha kushiriki kwenye ununuzi wa dhamana hizi za serikali.

Kwa zile dhamana za muda mfupi,kiwango cha chini kilichowekwa kwa mfanyabiashara ama mtu mwingine kushiriki kwenye ununuzi ama uwekezaji wake ni shilingi 500,000.

Hivyo mfanyabiashara aliye na kiasi cha kuanzia kiwango hicho, anaweza kabisa kushiriki kwenye ununuzi wa dhamana za serikali za muda mfupi.

Na kwa upande wa dhamana za serikali za muda mrefu, kiasi cha chini kilichowekwa kwa mfanyabiashara na mwananchi mwingine yeyote ni shilingi 1,000,000.

Hivyo mfanyabiashara mwenye kiwango kinachoanzia shilingi milioni moja na kuendelea, anaweza kabisa kushiriki kwenye ununuzi wa dhamana za serikali za muda mrefu.

Sasa sehemu ambako mfanyabiashara anaweza kununua dhamana za serikali ni kwenye masoko ya fedha.

Haya ni masoko kama yalivyo masoko mengine ya kawaida, ambako katika masoko haya bidhaa kuu inayouzwa ni fedha, tofauti na ilivyo kwenye masoko mengine ambako huuzwa bidhaa kama vile mchele maharage, ndizi, dagaa na zinginezo.

TUKUTANE WIKI IJAYO KWA UFAFANUZI ZAIDI