Kuna mengi ya kumzungumzia kiongozi huyu aliyeliasisi taifa hili, akajenga taasisi na mifumo mbalimbali ya kiutendaji, iliyoweza kuitofautisha Tanzania na mataifa mengine, hadi kuwa ya kupigiwa mfano barani Afrika.
Umoja, mshikamano na amani, tunayoendelea kuiimba hadi leo, ni matokeo ya jitihada za kiongozi huyo mpendwa.
Katika kuhakikisha wananchi wake wanastawi kimaisha, Mwalimu alitangaza maadui watatu ambao hadi anakufa, aliendelea kupambana nao.
Maadui hao ambao bado wanaishi hadi sasa, ni ujinga, umaskini na maradhi.
Na ndiyo maana katika kukabiliana nao alitoa elimu bure kwa maana kuwa, wazazi na walezi, hawakuchangia gharama yoyote ya moja kwa moja, kwa elimu ya watoto wao kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.
Ilikuwa ni uwezo wa mtoto mwenyewe tu kuchangamkia masomo, hadi pale uwezo wake utakapoishia.
Pale mwanafunzi wa shule ya msingi alipomaliza shule na kufaulu kwenda sekondari, Mwalimu Nyerere alikuwa akimsafirisha kutoka kijijini kwake hadi shule aliyopangiwa.
Ni kipindi ambacho wanafunzi walikuwa wakitoka Kagera kwenda kusoma Ruvuma, walikuwa wakitoka Mtwara kwenda kusoma Mara, na bado Mwalimu aliwasafirisha bure kutoka kwao kwenda shuleni na kurudi.
Na kutokana na sera yake hiyo ya elimu bure, ndiyo maana tuliweza kupata maprofesa kutoka hata kwenye familia maskini.
Muungwana anaona vyema kukumbuka kazi hii nzuri ya mwalimu kama kiongozi, kati ya nyingi alizozifanya katika utawala wake.
Ikumbukwe kuwa, wakati Mwalimu akiifanya kazi hii ya kusomesha bure watoto wa Kitanzania, alitegemea sana mapato yaliyotokana na mauzo ya mazao ya biashara, kama katani, pamba, kahawa, korosho, chai na mengineyo.
Hakuwa na vyanzo vingi vya mapato kama ilivyo sasa, ambako kuna madini, gesi, mafuta, shughuli za huduma na vyanzo vinginevyo.
Na hata baada ya kung’atuka, bado aliendelea kusisitiza umuhimu wa serikali kuwapatia elimu watoto wa maskini, ili waweze kujikomboa dhidi ya maadui ujinga, umaskini na maradhi.
Alisisitiza hilo kwa sababu ya sera ya uchangiaji iliyokuwa imeanzishwa na serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Muungwana ana maoni kuwa, wakati leo tukiadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, kuna umuhimu wa serikali yetu chini ya Dk. John Magufuli, kuendelea kujipanga zaidi.
Kwamba ijipange zaidi kisera na kimkakati, ili iweze kutoa elimu bure hadi ngazi ya chuo kikuu.
Muungwana anasema hivyo kwa sababu, kwanza ndiyo sehemu ya kukumbuka mazuri aliyoyaamini Mwalimu, wakati wa uongozi wake.
Mojawapo likiwa hilo la kuwapatia elimu watoto wote na hasa wa maskini, ili wajikomboe kutoka si tu kwenye ujinga, bali na umaskini.
Pili, hali ya kiuchumi ya wananchi kwa sasa inawafanya wengi washindwe kusomesha watoto wao elimu ya vyuo vikuu, kutokana na gharama zake kuwa kubwa kwa watu wa kawaida.
Wanafunzi wengi wanakosa mikopo ya kugharimia masomo yao.
Uamuzi mzuri wa sasa wa serikali ya Dk. Magufuli wa kutoa elimu bure hadi kidato cha nne, unamaanisha kwamba, wanafunzi wengi wataishia kidato hicho, na sababu wazi ni ya ile ya kutokuwa na uwezo wa kulipia ada za vyuo vikuu.
Ni kwa msingi huo ndipo Muungwana anapoiasa serikali ya Awamu ya Tano, itanue maamuzi yake ya kutoa elimu bure hadi kidato cha nne, ili sasa iwafikie na wa vyuo vya elimu ya juu.
Muungwana anaona umuhimu wa kuanzisha mfuko maalumu wa kugharimia masomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, na uchangie na sehemu ya mapato yatokanao na mauzo ya rasilimali za nchi, kama vile madini, gesi na mafuta.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







