Pamoja na matatizo mengi iliyonayo Azam kwa kushindwa kupambana na klabu kubwa za Simba na Yanga licha ya kwamba wana pesa na kila kitu, lakini kwa hili la mikataba ya wachezaji wanafaa kupongezwa.
Ukisikia mchezaji wa Azam anakwenda kwenye klabu nyingine, basi ni wao wenyewe hawamhitaji.
Wala huwezi kusikia mchezaji wa Azam ameingia mkataba na klabu nyingine, halafu anaondoka kwa kushindwa kutimiza baadhi ya vipengele vya mkataba.
Kwa Simba na Yanga hili limetokea sana, mfano, Kelvin Yondani kutoka Simba kwenda Yanga, Ramadhani Singano kutoka Simba kwenda Azam, na hata Bernard Morrison kutoka Yanga kwenda Simba.
Kama utakumbuka 2017, ambapo Simba iliwasajili John Bocco, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Aishi Manula, siyo kwa sababu Wekundu wa Msimbazi walikuwa na ubavu wa kuvunja mikataba, au kugombea mchezaji na timu hiyo, ila uongozi wa Azam wenyewe ulionekana hauwahitaji.
Kulikuwa kama kuna mpango wa kubadilisha mfumo wa klabu kutoka kuwa na wachezaji wakongwe, badala yake kutengeneza wachezaji vijana, mpango ambao nao baadaye ulifeli.
Nina uhakika, kama Azam ingekuwa inawahitaji wachezaji hao wabaki wangeweza kufanya hivyo.
Hata marehemu Patrick Mafisango alipotoka Azam kwenda Simba kulikuwa na mabadilishano ya wachezaji, kati ya klabu hizo mbili, mmoja akimchukua mchezaji huyo, huku Azam ikimtwaa, Abdulhalim Humud.
Juzi tu, Salum Aboubakar 'Sure Boy' amekwenda Yanga, na hii ni baada ya wao Azam wenyewe kuonekana wamemchoka.
Ni mchezaji ambaye aliihitaji Yanga miaka kadhaa iliyopita na klabu nayo ilimhitaji. Lakini kwa sababu Azam haikuhitaji aondoke ilishindikana. Huwa inaziba mianya yote, na hupati hata kipengele kinachoweza kuwabana na kuvunja mkataba mpaka wao waridhie. Hii ndiyo Azam. Huwezi kumchukua mchezaji wao wanayemhitaji kirahisi rahisi.
Hivi majuzi imeingia mkataba wa wachezaji wao chipukizi ambao wamepandishwa Ligi Kuu na wameanza kuwa nyota na kuzungumzwa sana na mashabiki wa soka kutokana na uwezo wao mkubwa.
Wachezaji hao ni Abdallah Kheri 'Sebbo' ambaye ametia kandarasi hadi mwaka 2024, Tepsi Evance na Paschal Mshindo nao wameongezwa mkataba wa mwaka mmoja mmoja, sasa watamaliza mwaka 2025, badala ya 2024.
Azam kama kawaida yake, huwa ina tabia ya kuongeza mikataba wachezaji wake tegemeo kabla haijamalizika.
Wao ukibakisha mwaka mmoja tu, wanakuongeza mwaka mmoja mwingine au miwili. Kama nilivyosema ukiona amebakisha miezi sita yupo Azam, basi huyo hahitajiki na anachotakiwa kufanya ni kutafuta timu nyingine.
Huu ni mfano wa kuigwa na klabu zote nchini ambazo mara nyingi zinasubiri mkataba umalizike na hapo ndipo viongozi wanaanza kukimbizana kukaa na mchezaji kwa ajili ya kusainishana tena.
Na wakati huo zinakuwa zinapata presha kutoka kwa klabu zingine kuwa zinamhitaji, wakati mwingine inakuwa si kweli.
Klabu nyingi za Ligi Kuu, ikiwemo Simba na Yanga zina tabia hiyo. Mfano Simba ililazimika kumsaini Clatous Chama kabla ya kwenda RS Berkane kwa sababu ya presha kuwa anatakiwa na Yanga.
Mohamed Hussein mkataba wake ulikuwa umekaribia kumalizika kabisa msimu uliopita, ndipo Simba ilipomsajili, baada ya shinikizo la uvumi kuwa anakwenda Yanga.
Wakati Azam ikiwaongeza Sebbo, Tepsi na Msindo, Joash Onyango na wachezaji kadhaa wa Simba wanamaliza mikataba yao. Kwa upande wa Yanga Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto nao wako mwishoni mwa mikataba yao, lakini klabu hizo zimekaa kimya.
Azam yenyewe huwa haitaki maneno, mapema tu, inamaliza shughuli. Ndiyo maana huwezi kusikia wachezaji wake au klabu yenyewe imeingia mgogoro kwenye usajili.
Unapomweka mchezaji wako unayemhitaji mpaka kiasi cha miezi sita, anakuwa na ruhusa ya kuanza mazungumzo na klabu nyingine inaonyesha wazi huna mpango naye.
Tatizo la klabu kubwa za Simba na Yanga, wachezaji wakishasajiliwa na kuwa ndani ya timu huwa hawana thamani.
Thamani kwao ni wachezaji wapya, na usajili mpya. Ndiyo maana unaweza kukuta timu imesajili mchezaji kwa mamilioni ya pesa, lakini imeshindwa kumuongeza mkataba mchezaji wake hadi anamaliza mkataba. Labda awe ni staa kweli kweli kwa kuhofia anaweza kuchukuliwa na timu pinzani. Hongereni Azam, lakini klabu zingine ziondoke huko na si vibaya kuiiga Azam FC.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








