Hapo waliondolewa na kupelekwa katika masoko makubwa yaliyoandaliwa na serikali, kwa ajili yao. Ni operesheni iliyoleta usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa pembezoni, lakini ikarejesha neema kubwa kwa wenye fremu za maduka.
Tulishuhudia baadhi ya watu hata wasiokuwa wafanyabiashara wakilaumu operesheni hii, lakini baadhi yao walipongeza na kudai kuwa mji sasa unaonekana vizuri na utulivu upo, ikilinganishwa na awali walipokuwa barabarani, maana kulikuwapo msongamano mkubwa.
Operesheni sasa imeonyesha kuzaa matunda ambayo hata waliokuwa wanapinga, wanapongeza japo kimoyo moyo au kimyakimya.
Aina ya operesheni inatoa nafasi kwa fremu za biashara kwenye maeneo zilizokuwa hazitumiki, sasa zinagombewa na wafanyabiashara, tena kule ambako kulitelekezwa kabisa.
Pia, yanakuwa maeneo ambayo yanapandishwa bei sasa, pakiwekewa vitega uchumi vikubwa vinavyolipa ushuru na kuongeza pato la taifa.
Niende na mfano hai wa jijini Dar es Salaam niliko, jirani na Soko la Karume, ingawa ina ujumbe wa kitaifa, maana mustakabali wa mazingira na biashara tajwa yanafanana.
Mahali hapo tumeshuhudia maduka makubwa ya vitambaa yamejengwa na hata katika balaa hili la moto fremu hizo hazijaathirika kutokana na aina ya ujenzi imara wa kisasa.
Tunataka ujenzi wa masoko wa aina ile, ambao hata ikitokea hitilafu ya umeme au aina nyingine ya uhalifu kama kuacha mshumaa kama ule uliosababisha hasara kubwa katika Soko la Karume, hauachi vilio vikubwa na wala hausababishi madhara kwa jamii.
Maeneo mbalimbali ya jiji hili sasa tunashuhudia ujenzi wa maduka makubwa na mazuri katika mpangilio bora, wafanyabiashara nao wanaonekana kuchangamkia fursa hizo, hata pato la taifa litaongezeka.
Hivi sasa maeneo kwa mfano kama Chanika, Mvuti kwa Bwaja, Mwembeni. Msongola, Gongolamboto, Mbagala na mengine mengi yanapendezeshwa na maduka makubwa katika mpangilio bora, ambayo awali yalichafuliwa na vurugu za biashara ndogo nje ya maduka, taka zikatupwa hovyo, mitaro ikajazwa taka na kuziba.
Waache waseme wenyewe!...Mo Nurdin ni mfanyabiashara wa viazi eneo la Chanika, ambaye yuko wazi kumpongeza Rais Samia Hassan Suluhu, kwa kuwa na maono ya usafi wa jiji, kupitia kwa kuelekeza operesheni hiyo, inayoenda mbali kwa matokeo yake, ikitengeneza uhusiano mzuri kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ni wazo linalomfikia hata Philipo Rali, mfanyabiashara wa nguo anayesema operesheni hiyo imepunguza ajali za barabarani na athari zake kwa wafanyabiashara walioko barabarani walioziba njia hata kukawapo msongamano.
Makamu Mwenyekiti wa Soko la Zingizilwa, Hassan Namkwacha, anaipongeza operesheni tajwa, akidai imesababisha kuboreshwa baadhi ya masoko yaliyokuwa tatizo kwa miaka mingi, hata kutelekezwa kabisa.
Anasema, Halmashauri ya jiji la Ilala sasa imeanza kuyafanyia marekebisho masoko mbalimbali yaliyopo katika jiji hilo, kwa kuyajengea mazingira rafiki kibiashara, ikiwamo miundombinu sokoni, akitoa mfano wa Zingizilwa, chumba kilichokuwa Shilingi 15,000 sasa Shilingi 30,000 kwa kuwa wafanyabiashara wameongezeka sokoni hapo.
Mkuu wa Masoko jijini Ilala, Victor Rugemalila, anasema pesa zimetengwa na jiji la Ilala kwa ajili ya kuwezesha uwezo wa kubeba watu 200 hadi 250 katika soko la Zingiziwa.
Rugemalila anasema mradi huo awamu ya kwanza utayagusa masoko ya Zingizilwa, Pugu Kajiungeni, Kigogo Freshi na Tabata Muslim.
Niseme asante Mama Samia kwa operesheni ,watu wameyakumbuka masoko yaliyosahaulika kwa muda mrefu.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








